MwanzoContactsEmail
Home Makala Maarifa Mitihani ya majaribio inapogeuzwa miradi ya walimu shule za msingi
BOOKMARK THIS PAGE
Mitihani ya majaribio inapogeuzwa miradi ya walimu shule za msingi  Send to a friend
Tuesday, 31 January 2012 11:26

  Na Fredy Azzah

MAJARIBIO na mitihani ni sehemu muhimu ya mchakato wa utoaji taaluma shuleni.Kwa wanasaikolojia na wataalamu wa elimu, vitu hivyo pia ni vichocheo vikubwa vya wanafunzi kusoma.

Ni kwa sababu hii, mifumo  ya elimu katika  nyakati zote za historia ya mwanadamu, imekuwa ikichagizwa na uwepo wa dhana kuhusu majaribio na  mitihani, japo katika miundo tofauti.

Kwa Tanzania mfumo wa elimu hasa katika elimu ya msingi, unatambua kuwepo kwa mitihani ya taifa, mitihani ya majaribio ya wilaya, mkoa na kanda (mock exams), mitihani ya muhula shuleni na mazoezi ya darasani.

Ukitoa mitihani na majaribio hayo kuwa kichocheo kwa wanafunzi kusoma, lengo lingine kubwa la mitihani hiyo ni kupima uelewa wa masomo wanayofundishwa wanafunzi shuleni.

Hata hivyo, kwa jamii na hata shule, mkazo mkubwa umekuwa ukiwekwa katika mitihani ya taifa, na ndiyo maana wazazi na  walimu kwa pamoja huhakikisha watoto wao wanafanya vema katika mitihani hiyo.

Ushindani wa shule ipi inafaulisha, ipi inafelisha umetamalaki kwa muda mrefu nchini, hali inayozisukuma shule nyingi kubuni kila njia zikiwamo zisizo halali, kuhakikisha zinakuza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wao katika mtihani wa darasa la saba.

Mojawapo ya mikakati ya kukuza kiwango cha ufaulu iliyobuniwa na shule nyingi nchini ni mitihani ya majaribio ambayo aghlabu imekuwa ikitolewa kwa wanafunzi wa kuanzia darasa la nne.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini utaratibu wa uendeshaji mitihani ya majaribio katika shule kadhaa za msingi hasa katika jiji la Dar es Salaam, umegubikwa na tamaa kubwa ya walimu kujipatia kipato cha ziada, hali inayolalamikiwa na wazazi na wanafunzi.

Kwa mfano, wazazi wa shule ya Mabibo wanasema watoto wao wanalazimishwa kwenda na Sh 200 kila siku na Sh 600 kila Jumamosi kwa ajili ya kulipia mitihani ya majaribio. Kwa wanafunzi wanaoshindwa kwenda na fedha hizo, wanakumbanna na adhabu ya kuchapwa viboko.

 “Tumechoshwa na michango isiyoeleweka, maana haiwezekani wazazi tukalazimishwa kulipa fedha  kila siku na kwa wiki lazima tulipe Sh1600 bado sijaweka mahitaji mengine ya mwanangu ya kila siku, kweli tunaumia,” anasema mzazi mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wanasema pamoja na umuhimu wa mitihani hiyo, wanajikuta katika wakati mgumu pale wanapokosa fedha za kuwapa walimu wanaodai hutumika kugharimia mitihani husika.

 “Kila Jumamosi lazima tulipe Sh600 kwa ajili ya mtihani, lakini mimi wazazi wangu wakati mwingine wanakosa hela. Ukija ukiwaeleza walimu  hawakuelewi,” anasema Salome John (jina siyo lake) anayesoma darasa la tano shuleni hapo.

Pamoja na uongozi wa Shule ya Msingi Mabibo kukataa kuzungumza na Mwananchi kuhusu madai ya wanafunzi kutozwa kiasi hicho cha fedha, baadhi ya wanafunzi na walimu walithibitisha kuwapo kwa mitihani hiyo na kiasi cha fedha kinachotozwa.

Uchunguzi umebaini shule nyingi zimekuwa zikiendesha mitihani kila siku asubuhi, mchana na  mwisho wa wiki kwa gharama zinazotofautiana, huku walimu wakisema fedha zinazolipwa zinatumika kugharimia vifaa vya mitihani.

Shule nyingine ambayo wazazi na wanafunzi wanailalamikia ni Shule ya Msingi Tumaini iliyopo Tabata. Katika shule hiyo, wanafunzi wa darasa la nne hadi la sba hutakiwa kwenda shule na Sh 100 hadi Sh 250 kila siku kama ada ya mitihani ya majaribio.

 “Huwa tunaambiwa tuje na Sh150 kila siku, lakini kuna siku nyingine wanasema hakuna umeme kwa hiyo tutoe Sh250,” anasema Peter Ilonga (jina siyo lake) anayesoma darasa la sita.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo  ambaye wanafunzi walimtaja kwa jina la mwalimu Shauri, anasema mitihani hiyo ni utaratibu uliowekwa na wazazi wenyewe.

“Mimi siwezi kuzungumza kwa undani, lakini mwalimu mkuu kwa kuwa ndiye katibu wa vikao vya wazazi angeweza kukueleza zaidi. Wewe njoo siku nyingine utamkuta akuambie,” anaeleza.

Mkazi wa Ilala, Mwanaisha Athumani, anasema  ingawa mitihani hiyo inawasaidia watoto, malipo ya kila wiki kwa ajili ya kuchangia mitihani husika yanawachosha wazazi hasa wenye kipato kidogo.

Anasema kama mitihani hiyo haina budi kufanyika, ingekuwa vema ikafanywa kila baada ya mwezi mmoja ili kutoa fursa kwa wazazi kutafuta fedha za kugharimia mitihani hiyo.

Kwa upande wake,  Mkuu wa Idara ya Saikolojia ya Elimu na Masomo ya Mitalaa ya Shule Kuu ya Elimu  katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,  Dk Kitila Mkumbo anasema mitihani ya majaribio ina umuhimu kwa kuwa inachangia kuwasukuma  wanafunzi kujisomea.

“Mitihani ya kila wiki, kwa mfano, kila Jumatatu, kila mwezi ni ya kawaida  na inamfanya mtoto  awe na sababu ya kusoma ili aweze kukumbuka. Mtoto mdogo hasa wa shule ya msingi, hasomi kwa future (kwa ajili  ya maisha ya baadaye),hivyo inabidi kuwe na kitu cha kumfanya apende kusoma ama alazimike kusoma,’’anasema.

Kauli ya Wizara ya Elimu

Naibu  Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mulugo, anasema suala la michango katika shule za umma, lazima lipate baraka ya bodi ama kamati za shule ambazo zinawawakilisha wazazi.

“Kwa hiyo kama kuna uamuzi wowote unaotaka wazazi wachangie kitu fulani,  lazima hivyo vyombo vipitishe na baada ya kupitishwa ufanyike mkutano wa wazazi ama shule iwaandikie wazazi barua kuwaeleza juu ya michango hiyo,” anafafanua.

Aidha, anasema mitihani inayotambulika na wizara yake unajumuisha mtihani   wa robo muhula ambao hufanyika mwezi wa tatu, mtihani wa nusu muhula unaofanyika katikati ya mwaka,mtihani wa robo muhula wa Septemba na ule wa kufunga mwaka.

“Kwa hiyo, kwa mwaka mzima kuna mitihani mitatu ambayo sisi tunaitambua, na hii ndiyo inayohitajika na Baraza la Mitihani. Mitihani mingine kama ile ya mock (majaribio) ni utaratibu wa shule, walimu na vyombo vingine huko,” anasema Mulugo.

Hata hivyo, anasema  kwa kuwa lengo la mitihani ya majaribio shuleni ni kuimarisha taaluma, ni vema ikafanyika katika hali ya uwazi bila kuwashurutisha wazazi, na kama kuna michango, stakabadhi zitolewe sambamba na malipo ya fedha

“Fedha zinazotolewa ziwe na risiti na pia kusiwe na hali ya kulazimishana, wazazi waelimishwe juu ya malengo na faida ya mchango wowote kama kutaonekana kuna utata,” anabainisha.

Januari 25 mwaka huu, Waziri Mulugo alifanya ziara katika Shule ya Msingi Mabibo na kubaini madudu kadhaa ikiwamo ufisadi wa mamilioni ya fedha zinazotokana na michango wanayotozwa wazazi ikiwamo mchango wa mitihani ya majaribio.

“ Nimekuja hapa kuona malalamiko ya wazazi wanayotuletea kama ni kweli na ukweli umeonekana....kumbe kuna mradi unaoendelea bila Serikali kufahamu wala kuwashirikisha wazazi!, alisema.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
Last Updated on Tuesday, 31 January 2012 11:39
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner