
| Sekondari ya Fidel Castro Ilijengwa kwa maandamano ya wanafunzi mwaka 1960 | Send to a friend |
| Tuesday, 31 January 2012 11:43 |
Na Elias MsuyaMOJA kati ya vivutio vikubwa kisiwani Pemba ni Shule ya Sekondari Fidel Castro, iliyoko jimbo la Wawi karibu na kambi ya Jeshi la Wananchi ya Alhamisi katika barabara inayoelekea kijiji cha Vitongoji wilayani Chake Chake. Shule hiyo ni moja kati ya shule kongwe visiwani Zanzibar na yenye historia iliyotukuka, kwani viongozi na wataalamu wengi wa Zanzibar wamesoma au kufanya kazi katika shule hiyo. Hata hivyo, kwa sasa shule hiyo iko katika hali mbaya baada ya miundombinu yake kuanza kuchakaa. Ingawa iliyokuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inaifanyia ukarabati mkubwa, bado zoezi hilo linaweza lisiirudishe historia iliyokuwepo awali. Akizungumza na mwandishi wetu Elias Msuya, Mkuu wa shule hiyo Salimu Kitwana Suruhu, anaeleza historia ya shule hiyo na hali yake kwa sasa. Swali: Tueleze historia ya shule hii japo kwa ufupi? Jibu: Shule hii ilijengwa mwaka 1960 baada ya maandamano na migomo ya wanafunzi wakitaka ijengwe shule ya sekondari kisiwani hapa. Kati ya wanafunzi hao, alikuwepo Katibu Mkuu mstaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya nchi huru za Afrika (OAU) Dk Salim Ahmed Salim. Wanafunzi hao kwa sauti moja walimtaka Mfalme wa wakati huo, Jamsheed ajenge shule kisiwani Pemba, badala ya wanafunzi kwenda kusoma kisiwani Unguja. Hapo ndipo jitihada zikafanyika na Jumuiya ya Madola ikajitolea kujenga shule hii. Wanafunzi wa kwanza waliingia mwaka 1963 wakati huo ikiitwa Sayid Abdallah Secondary school. Lilikuwa ni jina la wanafamilia wa Mfalme Jamsheed. Swali: Umesema shule ilianza kwa kuitwa jina la Sayid Abdallah, ilikuwaje tena jina hilo likabadilika na kuwa Fidel Castro? Jibu: Jina la Fidel Castro ni la kimapinduzi na lilitokana na mapinduzi ya Januari 12, 1964 baada ya Wazanzibari kuipindua serikali ya Sultan Jamsheed. Ni wakati huo pia Fidel Castro alikuwa amefanya mapinduzi nchini Cuba. Siyo shule hii tu, kuna shule nyingine iko Unguja nayo ina historia kama hii. Shule hiyo inaitwa Lumumba Sekondari. Jina hilo lilibadilika kutoka lile la awali la King George lililotolewa na Waingereza walioijenga. Lumumba naye alikuwa mwanamapinduzi wa iliyokuwa Zaire, sasa DRC. Swali: Je, Fidel Castrol aliwahi kuitembelea shule hii? Jibu: Hapana, isipokuwa aliwahi kutuma misaada ya vifaa kwa ajili ya kuisaidia hasa mwaka 1980. Swali: Umemtaja Dk Salim Ahmed Salim kama mmoja wa waanzilishi wa shule hii, je kuna viongozi wengine wa Serikali waliopitia shule hii? Jibu: wako wengi tu, lakini nitakutajia wachache. Baadhi yao ni pamoja na Omar Yusuf Mzee ambaye ni Waziri wa Fedha wa Serikali ya Zanzibar, Juma Hamad Omar aliyewahi kuwa Waziri wa Utalii Tanzania Bara. Makamu wa kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad amewahi kufundisha shule hii, Mratibu wa vyura wa Kihansi Dk Fadhila Himid Ally naye amewahi kuwa mwalimu. Wengine ni wataalamu mbalimbali walioko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama vile Nassoro Suleiman, Abdallah Fakhi na Mahir Mohamed. Wapo wengi tu waliopitia shule hii hata kama hawakuwa watu maarufu. Swali: Je, watu hao kwa sasa wanatoa mchango gani kwa shule? Jibu: Mchango wao siyo mkubwa sana, japo kwa sasa tunataka kuunda umoja wa watu waliosoma na kufanya kazi hapa. Tunatarajia kufanya Jubilee ya miaka 50 ya shule hii mwaka 2013 ambapo tutawaalika wote waliosoma na kufanya kazi hapa kuchangia maendeleo ya shule yetu. Swali: Changamoto gani zinaikabili shule hii kwa sasa? Jibu: Zipo changamoto nyingi. Kwanza tunakabiliwa na ubovu wa majengo, kama unavyoona sasa yanakarabatiwa na ndiyo maana tumewahamisha wanafunzi hapa kwa muda. Ukarabati huu umelenga kuboresha vyumba vya madarasa na ofisi zilizopo, lakini hakutakuwa na ongezeko la vyumba vingine. Wakati ule shule ilijengwa kulingana na idadi ya wanafunzi waliokuwepo ambapo kila darasa lilitakiwa kuwa na wanafunzi 35. Kwa sasa shule ina wanafunzi zaidi ya 635, vyumba vya madarasa viko vinane tu, havitoshi kabisa. Vilevile tuna uhaba wa vifaa vya maabara kama vile kemikali na vifaa na walimu wa masomo ya sayansi. Hata hivyo, tatizo la walimu tumeshaanza kulitatua na tumefanikiwa kupata walimu wa vidato vya chini hasa wa masomo ya Fizikia na Kemia. Tuna uhaba pia wa mabweni ya kulala wanafunzi. Wanafunzi hasa wa kike hawana nafasi ya kulala. Lipo bweni ila halina kitanda hata kimoja. Vyoo pia ni vichache kwenye malazi hayo. Tatizo jingine ni usafiri, hatuna gari la kusaidia usafiri hapa shule. Ikitokea mwanafunzi kaugua ghafla hatuwezi hata kumkimbiza hospitali. Swali: Hizo ni changamoto, vipi kuhusu mafanikio? Jibu: Tunayo pia mafanikio. Kwanza shule yetu inafanya vizuri kwenye mitihani. Kama nilivyokwambia, hii ni moja kati ya shule za Zanzibar zinazofanya vizuri. Hapa mpinzani wetu ni shule ya Lumumba tu ya Unguja. Kwa mfano, matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2010, tulipata daraja la kwanza wanafunzi tisa, daraja la pili walikuwa 13, daraja la tatu walikuwa 52, wachache walifeli. Shule yetu inapokea wanafunzi ambao ni wenye vipaji maalum kwa hiyo tunawawezesha kufanya vizuri. Hata hivyo, matokeo ya kidato cha sita kwa kweli ni mabaya. Hii ni kutokana na mchanganyiko wa wananfunzi wanaotoka shule nyingine kuja hapa, huwa na wakati mgumu kumudu ushindani wetu. Wanafunzi wetu hufanya vizuri kwa kuwa wana msingi mzuri, lakini hawa wengine tunapata wakati mgumu kuwanyoosha kwa kipindi kifupi, ndiyo maana matokeo yanakuwa mabaya. Swali: Unatoa wito gani kwa wadau wa shule hii? Jibu: Natoa wito kwa wadau wote waliosoma na kufanya kazi katika shule hii, kujitolea kikamilifu kuisaida ili isije kupoteza historia yake. Tunashukuru wapo waliojitolea vifaa kama vile kemikali na vifaa vinginevyo, lakini bado tuna upungufu mwingi. Tunawaomba wajitokeze kwa wingi kwenye jubilee ya miaka 50 itakayofanyika mwaka 2013 huko Unguja. Pia tunaiomba Serikali iiboreshe shule hii kwa kuongeza majengo na mahitaji mengine kulingana na wakati uliopo. Normal 0 false false false EN-US X-NONE X-NONE MicrosoftInternetExplorer4 /* Style Definitions */ table.MsoNormalTable {mso-style-name:"Table Normal"; mso-tstyle-rowband-size:0; mso-tstyle-colband-size:0; mso-style-noshow:yes; mso-style-priority:99; mso-style-qformat:yes; mso-style-parent:""; mso-padding-alt:0in 5.4pt 0in 5.4pt; mso-para-margin:0in; mso-para-margin-bottom:.0001pt; mso-pagination:widow-orphan; font-size:11.0pt; font-family:"Calibri","sans-serif"; mso-ascii-font-family:Calibri; mso-ascii-theme-font:minor-latin; mso-fareast-font-family:"Times New Roman"; mso-fareast-theme-font:minor-fareast; mso-hansi-font-family:Calibri; mso-hansi-theme-font:minor-latin; mso-bidi-font-family:"Times New Roman"; mso-bidi-theme-font:minor-bidi;} |



Na Elias Msuya










