
| Karibu mimba za utotoni kwa heri elimu! | Send to a friend |
| Tuesday, 31 January 2012 11:46 |
|
ELIMU ni haki ya msingi kwa binadamu yeyote. Kila msichana, mvulana, mwanamke na mwanaume, ana haki ya kupata na kunufaika na elimu ili aweze kufikia matarajio na malengo ya maisha yake. Elimu bora ndiyo ufunguo wa haya yote. Elimu inafungua fursa za ajira za kujiajiri na kuajiriwa, ubunifu na fikra za kuthamini na kufanya kazi kwa manufaa ili kuzalisha kipato cha mtu mmoja mmoja, familia na cha Taifa. Ni kupitia elimu bora ndipo mtoto wa masikini anaweza kuitawala dunia inayomzunguka. Ni kupitia elimu ndipo mtoto wa kibarua wa shambani anaweza kuwa Rais wa Taifa kubwa! Ni kupitia elimu ndipo mtoto wa mkulima anaweza kuwa mfanyabiashara mkubwa wa mazao ya chakula duniani! Ni kupitia elimu ndipo yatima anaweza kuondokana na unyanyaswaji na vitendo vya udhalimu. Ni kupitia elimu ndipo binadamu anaweza kutafiti na kuvumbua maarifa na teknolojia mpya. Kwa manufaa haya, elimu inabaki kuwa kitovu cha maendeleo ya binadamu popote alipo. Na zaidi sana, kwa watu masikini kama zilivyo nchi nyingi za Afrika, elimu pekee ndiyo ukombozi wetu. Hili alilisisitiza sana Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wake ambapo alitetea utoaji elimu kwa usawa. Kwa kutambua ukweli huu, hapa kwetu wazazi na wadau mbalimbali wa elimu wamewekeza fedha nyingi, jitihada kubwa na muda mwingi kwenye kuhakikisha watoto wanapata elimu ili wanufaike na elimu hiyo. Hata hivyo, jitihada za wazazi, Serikali, mashirika na taasisi mbali zimeshindwa kuzaa matunda tarajiwa hasa kutokana na kuwepo kwa vikwazo vingi vinavyowazuia watoto wetu kunufaika na elimu kwa usawa na haki. Moja ya changamoto kubwa ni kwamba watoto wengi hasa wasichana, wanashindwa kuhitimu ngazi mbalimbali za masomo yao, hivyo kukatisha masomo na kurudi kwenye jamii kuendeleza duara la umaskini. Kwa mfano, kila mwaka zaidi ya wasichana 8,000 nchini wanaacha shule kwa sababu ya kupata mimba. Maelfu wengine wanaripotiwa kuwa ni watoro, kumbe hawako shule kwa sababu wakipata mimba hawarudi shule kwa kuhofia kufukuzwa. Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi za mwaka 2010 kama zilivyoripotiwa katika Kitabu cha Takwimu za Msingi za Elimu cha mwaka 2011, zinaonyesha wanafunzi waliokatisha masomo katika shule za Serikali walikuwa 66,069. Japo wengi wao wanaripotiwa kuwa ni watoro, ni wazi kwamba mimba za utotoni ndiyo sababu kuu za utoro huo. Kwa upande wa shule za msingi waliokatisha masomo walikuwa wanafunzi 76, 246, huku waliofukuzwa kwa sababu ya mimba wakiwa 1,056. Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini ambako wasichana wengi huacha shule kuliko maeneo ya mijini. Taarifa za kiwilaya zikikusanywa na kunyambuliwa vizuri, zinaweza kubainisha hali ya kutisha kuhusu ukubwa wa tatizo hili, lakini kwa bahati mbaya hili halifanyiki kikamilifu. Mathalani, taarifa kutoka Tanga zilionyesha kuwa katika mkoa huo tatizo la wasichana kukatisha masomo ni kubwa zaidi. Karibu wasichana 300 walikatisha masomo yao mwaka 2009 kutokana na mimba za utotoni (Nipashe: Machi 15, 2010). Mkoani Kagera hali ni ile ile, taarifa zinaonyesha kuwa wasichana 880 walikatisha masomo kutokana na mimba. (Jambo Leo: Januari 12, 2010). Katika mkoa wa Pwani pekee, karibu wasichana 500 walikatisha masomo yao kati ya mwaka 2005 na 2009 kwa sababu hiyo hiyo. Hata utafiti uliofanywa mwaka 2010 na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), ulibaini picha ya kutisha. Kwa mfano, mkoani Tabora pekee, wanafunzi 819 walipata mimba kipindi cha mwaka 2006 hadi 2009. Licha ya ukubwa wa tatizo lenyewe , kuanzia Serikali, wazazi, asasi za kiraia na hata taasisi za kitaifa na kimataifa hakuna taarifa zenye takwimu za idadi ya wasichana waliorudi shule na kuendelea na masomo yao. Takwimu tulizo nazo ni za tatizo lenyewe na sio za ufumbuzi wake. Wote tunafanya kazi kubwa ya kukusanya takwimu za tatizo badala ya kukusanya suluhu ya tatizo ili kulimaliza tatizo lenyewe. Kama jamii hatunufaiki na takwimu hizo za maelfu ya watoto wetu kukatisha masomo kwa sababu ya mimba. Tumeendelea kuwatumbukiza mabinti zetu kwenye dimbwi la umaskini, ujinga, maradhi na fedheha. Hatuna ushahidi wa manufaa tuliyopata kutokana na malumbano ya je, warudi shule au wasirudi. Malumbano miongoni mwetu hayajatusaidia kusonga mbele, maana tunalumbana bila kutafuta suluhu wakati huo watoto wetu wanaendelea kupata mimba. Muda wa malumbano umekwisha. Karne ya 21 siyo ya malumbano ni ya utafiti, uvumbuzi, na ubunifu kwenye kutafuta suluhu za changamoto. Sasa ni muda wa kutafuta suluhu za kivitendo ili kuwasaidia watoto wetu kuendelea na masomo na kunufaika na elimu. Hatutakuwa wa kwanza kutekeleza zoezi la kuwarudisha wasichana wenye mimba shuleni. Nchi nyingi zinafanya hivyo na faida zimeonekana wazi. Hakuna faida ambazo nchi yetu imepata tangu ianze kuwaondoa shuleni mabinti wenye mimba. Nchi za Kenya, Zambia na Rwanda ni mifano mizuri ya mataifa yaliyofanikiwa kuwarejesha wasichana wenye mimba shule na wakaendelea na elimu yao na kunufaika. Jambo muhimu ni kuandaa mazingira rafiki yatakayowafanya watoto wetu warejee shuleni kwa utaratibu mzuri, huku watoto wao nao wakilelewa vema. Tusiogope kuthubutu, maendeleo ni kuthubutu! |














