MwanzoContactsEmail
Home Makala Maarifa Bado Watanzania tu watumwa wa kuhusudu lugha za kigeni
BOOKMARK THIS PAGE
Bado Watanzania tu watumwa wa kuhusudu lugha za kigeni  Send to a friend
Tuesday, 31 January 2012 11:53

MIAKA 50 ya uhuru, bado Tanzania haijawa na sera madhubuti kuhusu kuienzi na kuiendeleza lugha ya Kiswahili.
Kwa baadhi ya wasomi akiwamo Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Tataki), Dk Aldin Mutembei, hilo ni doa kubwa kwa Tanzania, nchi iliyoamua kwa makusudi kuyaachia mataifa mengine kuiendeleza lugha ya Kiswahili.


Akihojiwa na mwandishi wetu, Gedius Rwiza, Dk Mutembei anaeleza kwa kina mustakbali wa lugha hiyo anauosema unaelekea siko baada ya viongozi kuamua kuipa kisogo lugha hiyo.

Swali: Hivi karibuni tumesherehekea miaka 50 ya uhuru, tuna kipi cha kujivunia kuhusu lugha ya Kiswahili?
Jibu:  Inasikitisha kuona nchi inafikia hatua ya kuadhimisha miaka 50, lakini bado Watanzania na viongozi wao hawaithamini lugha yao, kiasi cha kushindwa na  Wakenya wanaokuja kwa kasi katika kuiendeleza lugha ya Kiswahili.


Wenzetu wanatumia mwanya unaotokana na dharau ya Watanzania pamoja na viongozi ambao ndio wanaopaswa kuwa tegemeo kubwa katika suala hili.  Hawa ndio viongozi utakaowaona katika  mikutano mbalimbali wakiona aibu kuzungumza Kiswahili.


Ieleweke hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea kwa kutumia lugha ya nchi nyingine. Inasikitisha kuona Watanzania wanaipa kisogo lugha yao na kuzithamini lugha za kigeni, hatuwezi kufika mbali hata kidogo.
Swali: Kuna ushahidi upi unaonyesha Wakenya wana kasi kubwa ya kukithamini Kiswahili kuliko Watanzania?
Jibu: Jambo linaloonekana wazi kwamba Wakenya wamepania kukikuza Kiswahili na hata kukitangaza ni uamuzi wao wa kuiweka Katiba yao katika lugha ya  Kiswahili. Hapa kwetu  ukilizungumzia  hilo utaonekana mtu wa ajabu  au mwenye uwezo mdogo wa kufikiri. Hili ndilo linalosababisha kuendelea kudidimia kwa Kiswahili.


Swali: Ukiitoa Kenya, nchi gani nyingine zinazokithamini Kiswahili?Jibu: Kuna nchi kadhaa  zinazokithamini Kiswahili kama vile Marekani na ni kwa sababu zinaamini lugha hiyo ni utambulisho wa Waafrika. Kwa mfano, Marekani kuna Wamarekani wanaokithamini Kiswahili na  mara nyingi wanapenda kutembelea nchi ambazo zinatumia lugha hiyo.
Unajua, kitendo cha nchi nyingine kuanza kutumia  Kiswahili tena kwa kasi na kukithamini kuliko sisi ni kitu cha aibu,  na ni ishara ya kuwa watumwa wa lugha za wenzetu. Huu siyo uzalendo,  tuanze kutafakari mustakbali  wa lugha yetu, haiwezekani tuzidiwe na nchi ambazo Kiswahili siyo lugha asilia.


Swali: Mtazamo wako ni upi kuhusu mjadala unaoendelea kuhusu lugha inayofaa kufundishia shuleni na vyuoni?
Jibu: Kuna mapendekezo mengi  yamekuwa yakitolewa kuhusu lugha ya kufundishia darasani. Mapendekezo haya yanataka lugha hiyo  iwe  Kiswahili,  lakini viongozi ambao ndio wenye  mamlaka ya kutoa uamuzi hawaoni kama mapendekezo hayo yana maana.


 Matokeo yake wanafunzi hawakijui Kiswahili wala hicho Kiingereza, hali inayochangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.


Kuna tume iliyoundwa miaka ya 1980 kufanya utafiti juu ya lugha ya kufundishia  chini ya aliyekuwa Waziri wa Elimu, Jackson Makweta. Februari 1982,  Makweta alikabidhi ripoti hiyo ambayo ilikuwa imependekeza lugha ya Kiswahili ianze kutumika kwa kidato cha kwanza mpaka cha pili, halafu baadaye iendelee hadi madarasa ya juu, lakini ripoti hiyo iliwekwa kapuni hadi leo hakuna kilichofanyika.


Swali: Una wito gani kwa  viongozi kuhusu kukiendeleza Kiswahili?
Jibu: Viongozi wana uwezo mkubwa katika kukuza Kiswahili, maana viongozi wa nchi nyingi hapa duniani wanapokwenda katika mikutano ya kimataifa, wanatoa mada zao kwa kutumia lugha zao huku pakiwepo na mkalimani, lakini hapa kwetu hata kama kuna wageni watano na wenyeji 100 wenyeji hawatathaminiwi badala yake wageni ndio wanaonekana kuwa na thamani. Matokeo yake walengwa walio wengi ambao ni Watanzania wanashindwa kuelewa  kinachozungumzwa.  


Pamoja na kwamba Kiswahili kimepiga hatua kubwa,  lakini hapa kwetu ambako sisi ndio  wahusika wakuu wa lugha hiyo tunatia aibu. Wakati nchi nyingine mtu akiongea lugha yake anaona fahari kubwa, sisi mtu akiongea Kiswahili katika mkutano anaonekana  mtu mwenye uelewa mdogo.


Hivi sasa hata mawaziri wanashindwa kuongea Kiswahili, Wao  kuongea Kiswahili ni jambo la aibu wakati Kiswahili ndicho kilichowafikisha hapo.


Viongozi wetu wakithubutu na kufanya  kama alivyofanya aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Joachim Chisano aliyethubutu kuzungumza Kiswahili katika mkutano wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU), tutafanikiwa kuiendeleza lugha hiyo.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #2 2012-02-01 18:23
mimi nafikiri kuna umuhimu kweli wakuedeleza swahili lakini tujifunze lugha zinazotuwezesha kuwasiriana na mataifa mengine
Quote
 
 
0 #1 2012-02-01 08:47
Wewe mhariri vipi...?
Ha ha ha ha ukoje wewe..?
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner