MwanzoContactsEmail
Home Makala Spoti Mikiki Changamoto za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu
BOOKMARK THIS PAGE
Changamoto za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu  Send to a friend
Monday, 16 January 2012 09:31

Kalunde Jamal
LIGI Kuu Tanzania Bara, iliyoanza Agosti 20, 2011 ilimaliza mzunguko wa kwanza mwishoni mwa mwaka jana kwa Simba kuongoza kwa tofauti ya pointi moja na hasimu wake, Yanga.

Simba ilimaliza ikiwa na pointi 28 wakati Yanga 27. Mzunguko wa pili wa ligi hiyo unaanza kutimua vumbi Januari 21 katika viwanja mbalimbali.

*Dosari
Mzunguko wa kwanza ulimalizika kwa dosari kadhaa. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitupiwa lawama kwa kukosa umakini kwa mambo ya msingi kama waamuzi kutotenda haki na kubadilika ratiba kila mara. Yafuatayo ni mambo yaliyojitokeza kwenye mzunguko wa kwanza:

*Waamuzi
Baadhi ya waamuzi walilalamikiwa kuhujumu baadhi ya mechi kwa kutoa uamuzi tata na wakati mwingine kushindwa kuzitafsiri sheria za soka.

Kushindwa kwa waamuzi kufanya kazi yao, ni wazi hakuweki haki ya utendaji wao kwani matokeo yake, hutoa ushindi kwa timu zisizostahiki na kuziminya nyingine.

Timu zilikuwa zikipeana zamu kulalamikia waamuzi kuchezesha mechi bila kufuata na kupoteza imani kwa mashabiki.

Tulishuhudia klabu tatu za Ligi Kuu za Bara, vinara Simba, mabingwa watetezi Yanga na Azam, wakipeleka malalamiko TFF wakidai kuwa waamuzi hawawatendei haki katika mechi zao na hata wachezaji wao wanapoumizwa kwenye michezo yao lakini hakuna adhabu zinazotolewa.

Kama waamuzi wakiachwa wafanye wanachotaka huku wahusika wanalikalia kimya suala hilo itakuwa hakuna mantiki ya kuwa na waamuzi. Itakumbukwa kuwa mara kadhaa kamati za ligi zinapofanya majumuisho haziachi 'kufa nao' na waamuzi wazembe.

Ili kuleta ushindani katika mzunguko wa pili, ni vema waamuzi wakaonyesha ukomavu wa sheria na kanuni za kuchezesha ili kupata bingwa stahiki.

*Fedha za wadhamini
Ulikuwa wakati mgumu kwa baadhi ya timu kutokana na kukabiliwa na ukata. Timu zilisafiri kimkandamkanda na wakati mwingine ni kutokana na uchelewefu wa fedha za wadhamini ambazo hupunguza makali.

Baadhi ya timu kama Toto African, African Lyon, Villa Squad kimsingi ziko katika hali ngumu ikilinganisha na timu kama Azam FC, Simba au Yanga.

Kikubwa ni kucheleweshwa kwa fedha za nauli kwa timu karibu zote na kimsingi nyingi ya hizo, hazina vyanzo vingine vya mapato zaidi ya kutegemea fedha za wadhamini.
 
TFF kwa upande wake, badala ya kutafuta ufumbuzi wa suala hilo, walikuwa wanazitupia lawama timu zisipokwenda vituoni.

Ucheleweshwaji wa fedha za nauli kwa timu pia ulifanya timu zisijiamini hivyo hata zilipopata nauli ya kuunga unga zilikuwa zinajikuta hazijajiaandaa vya kutosha na hata kufanya vibaya. Kujimudu kwa timu kunaleta msisimko na ushindani.

*Mabadiliko ya ratiba

Miongoni mwa vitu ambavyo vilivyofanya ligi isiwe na msimamo na hata kuwachanganya mashabiki na wadau wa soka ni mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba na wakati mwingine bila kutoa taarifa mapema.

Haikuwa ajabu kuona leo ratiba hii kesho ile, lakini keshokutwa ikawa nyingine na wahusika TFF kuona wapo sahihi kwa kile kinachofanyika.

Ili ligi iwe na mvuto wa kuendelea, ili shabiki na mdau wa soka aweze kupanga vizuri ratiba yake ya kwenda uwanjani ni vema iandaliwe ratiba ya kudumu kw akufuata kalenda za Caf, Fifa kwa mechi za klabu na timu ya taifa.

*Ligi haikutangazwa

Pamoja na kuundwa kwa kitengo cha masoko chini ya Jimmy Kabwe, lakini anaonekana ameshindwa kutumia nafasi hiyo kama Ofisa Mkuu wa Masoko, na kutumika kama MC kwenye shughuli za TFF.

TFF ilitakiwa kuiuza Ligi Kuu kwa kusaka wadhamini kwa faida yake na klabu. Ligi ilikuwa ya kimya kimya hakukuwa na matangazo ya kueleza umma nini kinaendelea au timu gani inacheza na ipo kwenye nafasi ya gani kwenye msimamo wa ligi.

Nafikiri ni busara kama kungekuwa na utaratibu wa kutangaza ligi kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama vile radio, luninga na magazeti lengo likiwa ni kuwavutia mashabiki, kwenda viwanjani. TFF inabidi iache kutegemea waandishi wa habari kuwatangazia mechi kwa kuandika habari na inabidi watoe matangazo katika redio na ikiwezekana kuwa na website.

*Kauli ya kocha wa Mtibwa Sugar
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Tom Olaba anasema, ili kuifanya ligi iwe ya ushindani, baadhi ya mambo yanatakiwa yafanyiwe marekebisho huku akilenga zaidi kwenye suala la waamuzi kwa kudai kuwa wamekuwa ni tatizo.

Kama kuna uwezekano, waamuzi wapigwe msasa na wajue hili tatizo linadumaza ligi na bidii za wachezaji.

Anasema wachezaji wakifanyiwa uonevu na waamuzi na waamuzi wakionyesha kupendelea timu fulani basi wachezaji hushiriki huku wakijua ligi sio yao ila ni ya kina fulani, anasema Olaba.

Kocha wa JKT Ruvu, Charles Kilinda yeye anasema suala la viwanja liboreshwe kwa kuwa kuna baadhi ya viwanja ni duni na miundombinu yake haijakamilika kwa matumizi, lakini hali ya usalama pia izingatiwe.

Naye Katibu wa Toto Africa, Salum Kaguna anasema; ratiba izingatiwe kwa kuwa timu za mbalimbali zinapanga mikakati yake tangu kuanza kwa ligi, lakini kutokana na ratiba kuyumba utekelezaji unasumbua.

Kwa kweli ratiba ni changamoto ifanyiwe kazi kama hiyo haitoshi sisi tunaotegemea fedha za wadhamini kuendeshea timu zetu tupewe fedha hizo kwa wakati ili angalau zitusogeze,anasema Kaguna.

Simba ndiyo inayoongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 28, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 27 na Azam, JKT Oljoro na Mtibwa zinafuatia zikiwa na pointi 22 huku JKT Ruvu na Moro United zikiwa na pointi 17.

Lyon ina pointi 14, Kagera na Toto African zenyewe zimevuna pointi 13 na Ruvu Shooting ina pointi 12. Timu zinazoshika nafasi tatu za chini ni Coastal Union yenye pointi 10, Polisi Dodoma (pointi nane) na Villa Squad ina pointi sita.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
Last Updated on Monday, 16 January 2012 10:19
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner