MwanzoContactsEmail
Home Makala Spoti Mikiki Matola: Wachezaji jitumeni mwende Afcon
BOOKMARK THIS PAGE
Matola: Wachezaji jitumeni mwende Afcon  Send to a friend
Monday, 30 January 2012 11:40

Kalunde Jamal
KOCHA wa timu ya Simba B, Suleiman Matola amesema wakati umefika kwa wachezaji wa Tanzania kujituma ili kupata nafasi ya kucheza Fainali za Afrika, Afcon, ili kuwapa faraja Watanzania.

Matola aliyezungumza na Spoti Mikiki, alisema kuwa wachezaji wa sasa wana kila sababu ya kucheza Fainali za Afrika kwa kuwa wanapata huduma nzuri ikilinganisha na enzi zao walipokuwa timu ya taifa.

Enzi zetu kambi ilikuwa Salvation Army, uwanja ni Uwanja wa Taifa, leo hii wachezaji wana uwanja mzuri, wanalala hoteli kubwa, wanacheza mechi hadi na wachezaji wakubwa Brazil, Ghana, Ivory Coast, New Zealand lakini wanashindwa kujitambua, anasema Matola beki wa zamani wa Simba na Jomo Cosmos ya Afrika Kusini.

Matola anaeleza masikitiko yake kwa timu ya Tanzania kushindwa kushiriki Fainali za Afrika kila mara na kusema kwa kiasi fulani inawapunguzia uzalendo kwa kuwa watajenga tabia ya kushangilia timu za nje na hata timu yao itakapoingia watakuwa tayari wameshalemaa.

Anasema: Hiki ni kitu kibaya sana kama mtu atakuwa kila mwaka anaishangilia timu ya Brazil, Ghana, Zambia na nyingine ambazo zitakuwa zimefanikiwa kuingia ni ngumu baadaye kuja kumshawishi kuishangilia timu ya nyumbani kwanza ataiona haiwezi kwa kuwa hajazoea kuishangilia tangu mwanzo.

Matola anasema; Tanzania imebarikiwa kuwa na wachezaji ambao walitandaza kabumbu safi enzi zao na sasa wameamua ama kuwa washauri au makocha wa timu mbali mbali hii yote ni kutokana na uzowefu walionao.

Kama kungekuwa na mtu au watu wanathamini mchango wao na kuufanyia kazi si ajabu saa hizi tungekuwa tunashangilia timu yetu kwenye michuano hii kuliko ilivyo sasa ambapo tumeishia kugawana nchi za kushangilia.

Naziomba taasisi husika kuelekeze nguvu kwenye michuano mikubwa kama hii na zifanye juhudi za makusudi kuhakikisha timu yetu ya taifa inakwenda bila  ya hivyo kila siku tutakuwa watazamaji na kujinyima wenyewe haki yetu ya msingi, anasema Matola.

Kuhusu mtazamo wake kwa michuano ya mwaka huu, Matola anasema; imepoteza mvuto na hii inatokana na  wachezaji wanaocheza Ulaya kucheza chini ya kiwango kwenye timu zao wakihofia kuumia.

Anasema na hilo tatizo sio kwenye hiyo michuano tu bali hata kwa wachezaji wa nyumbani wakija kutoka kwenye timu za kulipwa hucheza chini ya kiwango na hilo siku za hivi karibuni limejidhihirisha.

Wewe mwenyewe ni shahidi hata kwa wachezaji wetu ambao wanacheza soka la kulipwa wakija hawachezi vizuri kama ambavyo wanafanya wakiwa kwenye vilabu vyaoalisema Matola na kuongeza Kwa mtazamo wa haraka haraka kulitatua hili ni ngumu na inawezekana wakija wanaambiwa wawe makini na kupewa vitisho ingawa sina uhakika na hilo, anasema.

Aliendelea kueleza kuwa kitu kingine kinachochangia michuano hii kuwa haina mvuto ni kukosekana kwa timu kubwa kama vile Nigeria, Cameroon, Algeria, Afrika Kusini ambazo zimeshindwa kufuzu safari hii.

Matola anayeitabiria Ivory Coast kutwaa ubingwa, aliiongoza timu ya vijana ya Simba kutwaa ubingwa wa Michuano ya Vijana ya U-20 iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana jijini Dar es Salaam.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
Last Updated on Monday, 30 January 2012 13:58
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner