
| Tanzania: Nchi ya mstari wa mbele kwa ukombozi wa bara la Afrika | Send to a friend |
| Friday, 09 December 2011 12:10 |
|
Na Matern Kayera Katika ardhi ya Tanzania, Serikali iliamua kulitumia eneo la Kongwa Mkoani Dodoma kama kituo cha mafunzo ya kijeshi kwa wapigania uhuru wa kutoka vyama vya FRELIMO (Msumbiji), SWAPO (Namibia), MPLA (Angola), PAC na ANC (Afrika ya Kusini), pamoja na ZANU PF kutoka Zimbabwe. Wazee, Tito Fungo (90) na Ozmanda Boma (74) ambao ni wenyeji wa Kongwa, wanasema kabla ya kuja kwa wapigania uhuru katika mji wao, Mwalimu Julius Nyerere alifika kwanza na kuwaomba wawapokee wageni hao ambao nchi zao zilikuwa bado zinatawaliwa na wakoloni. Baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka, baadaye mwaka huo huo (1963), aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi, Mh Oscar Kambona alifika Kongwa na kuendelea kuwasisitiza wananchi juu ya umuhimu wa kuwapokea wageni hao kutoka nchi za kusini mwa Afrika. Kambona aliwaambia wenyeji wa Kongwa katika mkutano wa hadhara aliofanya katika Jengo la TANU kuwa, waafrika wenzetu wa nchi za Msumbiji, Namibia, Angola, Afrika ya Kusini na Zimbabwe bado wanateswa na wanahitaji kupata uhuru, na uhuru wao wataupata kwa mtutu wa bunduki; Kufuatia maombi ya viongozi wa Kitaifa, wazee hao wamesema kwa kuwa asili ya watu wa Kongwa ni ukarimu, maombi yao yalikubaliwa na hivyo wageni wakafika na kuanza mafunzo ya kijeshi kwa muda wote waliokuwepo pale. Mradi huo pia ulikuwa umelenga kuwapatia ajira wanajeshi wa Uingereza waliorudi kutoka vitani. Baada ya utafiti kukamilika, kilimo cha karanga kilianzishwa rasmi mwaka 1948 na kuipa Kongwa umaarufu mkubwa. Kwa kuwa mashamba yalikuwa yakimilikiwa na wazungu, waafrika walitumika kama vibarua tu katika mashamba yale. Watu wa kutoka Mauritius walikuwa wakifanya kazi za udereva na ufundi; watu wengine waliokuwa wakifanya kazi katika shirika hilo ni Wahindi na Wasomali. Kutokana na ukosefu wa mvua kwa miaka mitatu mfululizo, Shirika la OFC liliamua kufunga mradi huo wa kilimo cha karanga. Katika eneo hilo la Stesheni ya Kongwa ndipo walipokuwa wakikaa wapigania uhuru waliotoka Kusini mwa Afrika. Mzee Boma anaweka wazi kuwa wakati huo yeye ndiye alikuwa mpiga picha wao na aliyekuwa akizisafisha pia. Anaongeza kuwa Samora Machel alikuwa mchangamfu sana na alielewana na watu wengi hata kufikia kujifunza na kuzungumza kigogo. Kwa upande wake Mzee Fungo anasema wageni wao walikuwa watulivu na hawakuwa na vurugu zozote; walishirikiana nao vizuri. Amesema kwa mfano ukumbi wa polisi Kongwa ulijengwa na Wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini. Kushiriki kwao ilikuwa katika kucheza michezo mbalimbali kwa kushirikiana na wananchi; baadhi ya michezo hiyo ilikuwa mpira wa pete na mpira wa miguu. Lakini pia walishiriki katika ujenzi wa Jumba la Maendeleo Kongwa mwaka 1967. Baadhi ya wanafunzi waliohudhuria katika somo la Kiswahili ni Sam Nujoma, David Ushona, Limo, na Samora Machel; kwa mujibu wa wenyeji wa Kongwa, wanafunzi hawa pia walijifunza lugha ya Kigogo. Kuwepo kwa wapigania uhuru katika mji wa Kongwa, kulitoa fursa kwa wenyeji kuanzisha shughuli mbalimbali za kibiashara. Biashara kubwa iliyofanyika ilikuwa ni ya vyakula. Wananchi walipata nafasi ya kuwauzia vyakula wapigania uhuru na hivyo kuwa na chanzo cha uhakika cha mapato kutokana na uhusiano mzuri uliokuwepo miongoni mwao. Aidha, hali ya mahusiano ilienda mbali zaidi hata kufikia hatua ya kuoana kati ya mabinti wa Kongwa na wapigania uhuru. Kwa mujibu wa Mzee Fungo baadhi ya wapigania uhuru wa kutoka Namibia waliondoka na familia zao, yaani wake zao pamoja na watoto. Usimamizi kwa wapigania uhuru Mafunzo ya kijeshi Anasema wapigania uhuru walikuwa wakipita kwenda kwenye mazoezi saa tatu asubuhi na kurudi saa kumi na mbili jioni. Anaongeza kuwa mafunzo hayo yalisimamiwa vyema na wanajeshi wa Tanzania kwani Mkuu wa Kambi alikuwa Meja Chongambele akisaidiana na askari wengine kama vile Kanali Mwisongo. Amesema walikuwa na hatari kwani Wareno walishawahi kukamatwa Kongwa kwa kupotea njia kwani walipoulizwa walisema wametoka Singida na kuelekea Dodoma, lakini walikuwa hawajui Dodoma ni sehemu gani. Ujenzi wa handaki Ameongeza kuwa pembeni kidogo mwa nyumba hiyo kuliwekwa rada ambayo ilikuwa ikimulika pande zote ili kubaini kama kuna adui yeyote aliyekuwa akiwanyemelea. Handaki ambalo Samora Machel alikuwa akilitumia bado lipo mpaka sasa, ingawa uchakavu unashika kasi. Pia katika eneo la Morisheni kuna makaburi ya wapigania uhuru waliofariki kutokana na maradhi mbalimbali. Wageni wengi hupenda kutembelea maeneo hayo kwa ajili ya kupata historia.
|














