MwanzoContactsEmail
Home Makala Mchakato wa Katiba Mpya Tujipime kwa kujilinganisha na wenye afya
BOOKMARK THIS PAGE
Tujipime kwa kujilinganisha na wenye afya  Send to a friend
Friday, 09 December 2011 12:20

Na Salim Said Salim
TUMETIMIZA miaka 50 tokea Tanganyika kupata uhuru. Huu sio tena muda mfupi wa kusema nchi yetu bado ni changa, labda unaweza kusema bado haikupevuka.
Tujiulize na tusiridhike mpaka tupate jawabu ya maana. Tujiulize tumepiga hatua mbele au tumerudi nyuma? Tuwe wakweli kwa nafsi zetu na nchi yetu. Ni vibaya na hatari kwa mtu kuukataa ukweli anaouona.

Kwa lile jambo ambalo tunaamini kwa dhati kuwa tumepata mafanikio ni haki yetu kujipongeza, lakini pale ambapo tumeboronga tunao wajibu wa kuukubali ukweli na tufanye juhudi za kujirekebisha. Tuachane na utamaduni wa kuridhika kwa sababu tuna amani na utulivu katika nchi yetu, tofauti na hali tunayoishuhudia katika nchi nyingi za Kiafrika.

Hapa tukumbuke wosia wa baba wa taifa,
Mwalimu Nyerere alipowataka Watanzania siku zote kujipima kwa kujilinganisha na mtu ambaye ni mzima kiafya na sio mgonjwa kwa kusema “mie maradhi yangu ni afadhali kuliko yale ya mwenzangu.
Hizi sio tena zama za kudanganyana kwa kauli zenye ladha nzuri na bashasha ambazo hazimpi shibe mtu mwenye njaa na badala yake zinamuongezea mzigo wa matatizo.

Tuachane na kupeana ahadi ambazo hazitekelezeki kutokana na uwezo au utaalamu mdogo tulionao kwa wakati ule. Vile vile tabia ya kutoa visingizio hivi na vile, ikiwa pamoja na bahati mbaya, kwa makosa tunayoyafanya na kuyarudia.
Hizi ni zama za ukweli na uwazi na mwenendo huu ni mhimili muhimu wa huo tunaouita utawala bora, wa haki na wa sheria.
Kwa mtazamo wangu, kwa vile nilikuwa na akili timamu wakati tunapata uhuru, hali tuliyokuwa nayo hivi sasa, kwa kiasi fulani inakatisha tamaa.

Niliwalaumu sana vijana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati ule ndio chuo kikuu pekee nchini, walipotoa tamko mwishoni mwa miaka ya 1960 waliposema afadhali wakati wa ukoloni.
Hii leo, kwa shingo upande, naona kauli yao ilikuwa na mantiki  kwa kiasi fulani na waliona mbali, ijapokuwa jazba na ukiritimba wa kisiasa uliokuwapo wakati ule ulipelekea baadhi yetu kuwaona si wazalendo.

Ukweli ni kwamba hali ya maisha hivi sasa nchini ni ngumu, tena unaweza kusema kwa baadhi ya watu ni zaidi kuliko wakati tulipopata uhuru. Huo ndio ukweli.
Hapana ubishi kuwa tumepata mafanikio katika maeneo mengi, kama ya ujenzi wa barabara mijini na vijijini. Lakini hali ya kiuchumi na huduma za ustawi wa jamii hasa umeme na maji safi na salama sio nzuri katika maeneo mengi ya nchi yetu.

Hii leo watu wengi wanapata shida ya kupata angalau mlo mmoja kwa siku huku tukijipongeza kuwa uchumi wetu unakua. Wakati tulipopata uhuru shilingi zetu saba zilikuwa sawa na dola moja ya kimarekani na shilingi 20 sawa na pauni ya Kiingereza.
Leo thamani ya shilingi inazidi kuporomoka na kufikia Sh1700 kwa dola na kwa kasi ya kuanguka kwake si ajabu tukamaliza mwaka kwa shilingi 2000 kuwa sawa na dola moja.
 
Bei za vyakula zipo juu sana na kwa kiasi fulani mfumo wetu wa utozaji viwango vya juu vya kodi kuliko majirani zetu wote unachangia hali hii ya kukatisha tamaa. Kwa mfano, Rwanda inapata sehemu kubwa ya petroli na mafuta yake ya taa kupitia Dar es Salaam, lakini bado bei ya mafuta kwao ni chini kuliko kwetu.
Jambo jengine ambalo huenda linaifanya hali yetu ya uchumi kuwa mbaya kiasi hiki ni gharama kubwa za utawala za serikali yetu.

Tulipopata uhuru idadi ya mawaziri na manaibu wao haikuzidi 15, lakini leo hii baraza limekuwa ukumbi wa mawaziri wenye watu karibu 70.
Vile vile kila baada ya muda mfupi tumekuwa tukiongeza idadi ya viongozi kwa kuongeza idadi ya wilaya na mikoa.
Magari yanayotumiwa na viongozi wetu ni ya kifahari licha ya serikali kudai inabana matumizi.  Baaadhi ya magari haya yanatumika zaidi kwa shughuli za kibinafsi na sio za kiserikali, hasa wakati wa mwishoni mwa wiki.

Tumefanikiwa kuongeza kwa zaidi ya mara tano idadi ya shule na zahanati, lakini huduma zilizopo haziridhishi na labda ndio maana watoto wa wakubwa wanasoma katika shule binafsi au nje ya nchi.
Vile vile wakubwa hukimbilia India, Afrika Kusini na Ulaya kwa matibabu na hiki ni kielelezo kinachoonyesha kwamba hata viongozi wetu wanajua kwamba huduma za matibabu hapa kwetu sio nzuri.

Kumekuwa na malalamiko mengi juu ya namna tulivyozitoa rasilimali zetu, kama machimbo ya dhahabu, kwa wawekezaji kutoka nje. Karibu kila kukicha tunawasikia wananchi wa maeneo mbali mbali wakilalamika kwamba hawafaidiki na uwekezaji uliofanywa kwenye maeneo yao. Badala yake, wawekezaji wanadaiwa kuwanyanyasa Watanzania.

Katika suala la uwekezaji tunashuhudia vichekesho. Hapa kwetu, tokea kutamka lile neno “rukhsa”, kumaanisha biashara huria, nchi yetu imekuwa kama jaa la kutupia taka.
Hivi leo tunashuhudia wageni wakiuza karanga, shanga, kufanya kazi za kupaka rangi magari na hata kuongoza wageni katika mbuga zetu za utalii.

Wakati sisi ni wakarimu wa kutoa ajira kwa wageni, vijana wetu huwa hawaruhusiwi kufanya kazi katika nchi ambazo watu wake tumewapokea na kuwaachia wafanye watakavyo.
Matokeo yake hii leo maelfu ya vijana wetu hawana ajira. Sijui hali itakuwaje pale soko la ajira litapokuwa huru katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ukizingatia kwamba kiwango cha elimu Tanzania ni cha chini ukilinganisha na ilivyo katika nchi tunazoshirikiana nazo katika Jumuiya.

Wakati huu tukiwa tnaaadhimisha miaka 50 ya uhuru. ni vyema tukazipitia upya sheria zetu za uwekezaji vitega uchumi, biashara, utalii, elimu, afya, biashara na sekta nyengine ili tufanye marekebisho yatakayowapa afueni wananchi wetu kiuchumi.
Hivi sasa tupo katika mchakato wa kufanya mageuzi makubwa ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kutafuta katiba mpya itakayowaridhisha na kuwatumikia Watanzania vizuri zaidi.

Mchakato kama huu wa mageuzi unahitajika ili tuanze safari ya kuanzia mwaka wa 51 wa uhuru tukiwa na matumaini ya kuwa  na hali bora ya maisha na kujenga msingi mzuri kwa vizazi vijavyo vya nchi hii.
Inawezekana kuleta mabadiliko makubwa na watu kusahau shida wanazopata hivi sasa, lakini panahitjika nia ya kweli, uaminifu na uadilifu na kuweka mbele maslahi ya nchi.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner