MwanzoContactsEmail
Home Makala Mchakato wa Katiba Mpya Edwin Mtei: Taifa limepita safari ndefu
BOOKMARK THIS PAGE
Edwin Mtei: Taifa limepita safari ndefu  Send to a friend
Friday, 09 December 2011 12:33

 

 

 

 

 Mussa  Juma, Arusha.
UNAPOZUNGUMZIA historia ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika  huwezi kumsahau, Edwin Mtei, mmoja wa waliokuwa watendaji waandamizi  wa Serikali ya Kwanza ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julias Nyerere.
Edwin Mtei kashika nyadhifa mbali mbali  mara baada ya uhuru, ikiwamo ya kuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu, Katibu Mkuu Hazina, Waziri wa Fedha na Uchumi na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Akizungumza katika mahojiano maalum nyumbani kwake eneo la Tengeru wilayani Arumeru mkoani Arusha hivi karibuni, Mtei ameelezea safari ndefu ya Tanzania kuanzia mwaka 1961 Tanganyika ilipopata uhuru hadi leo ambapo Tanzania Bara inatimiza miaka 50 ya kuwa huru.

Historia ya mwanasiasa huyu, inatoka mbali kwani kabla ya uhuru  alikuwa mmoja wa watumishi katika serikali ya kikoloni katika kitengo cha utumishi wa umma. Anasema baada ya kuacha kazi katika serikali hiyo, alikwenda nchini Kenya ambapo alikuwa akifanya biashara ya sigara.
Mtei anasema baadaye alirejea nchini na kufanyakazi katika Tume ya  Maendeleo ya Afrika  Mashariki (East African High Commission).

Anasema tume hiyo ilikuwa ikifanya kazi ya kuendesha miradi mbali mbali ambayo ilikuwa inaziunganisha nchi za Afrika Mashariki kama bandari, usafiri wa reli, posta na masuala ya ushuru wa forodha.
Mtei anasema mwaka 1962 aliteuliwa na serikali ya Tanzania kwenda kufanya kazi katika taasisi ya East African Common Authority .
Anasema mwaka 1964 hayati Baba wa Taifa alimteua kuwa Katibu Mkuu wa Hazina, 
 
Mtei anasema wakati huo, hayati Nyerere alikuwa kwenye mazungumzo na  viongozi wa nchi nyingine za Afrika Mashariki kuanzishwa shirikisho la nchi hizo.
Wakati huo tulikuwa tunatumia sarafu moja kwa nchi hizi zote za Afrika Mashariki, anasema Mtei.
Mtei anafafanua kuwa mwanzoni mwa mwaka 1965 ilipothibitika hakuna uwezekano wa kuwa na Shirikisho la nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ilianza mikakati ya kuwa na Benki Kuu.

Anasema wakati mchakato huo ukiendelea mwaka 1965 mwishoni aliteuliwa kuwa gavana wa kwanza wa Benki Kuu.
Anasema Juni 14, 1966 waliweza kutoa fedha ya kwanza ya Tanzania. Hata hivyo anasema mwaka 1974 alihamishwa Benki Kuu na nafasi yake kuchukuliwa na Charles Nyirabu baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
 
Kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika ya Mashariki
Mtei anasema mwaka 1977 akiwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilivunjika.
Anasema kuvunjika kwa ku jumuiya hiyo kulitokana na matatizo ya kuichumi yaliyosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta na pia deni kubwa la Jumuiya hiyo katika shughuli zake mbali mbali.

Mtei anasema moja ya taasisi ambazo zilikuwa na deni kubwa na kuchochea kusambaratika kwa jumuiya ni deni la shirika la ndege ya Afrika Mashariki.
Anasema kutokana na deni hilo, Februari, 1977, Serikali ya Kenya ilizuia ghafla safari za ndege za shirika hilo katika nchi nyingine.
Mzee Mtei anasema wakati huo, shirika hilo la ndege licha ya kuwa lilikuwa likifanya kazi katika nchi za Afrika Mashariki, pia ndege zake zilikuwa na safari katika mabara mbali mbali kama Amerika, Ulaya ya Asia.

Nyerere afunga mpaka na Kenya
Kutokana na kuzuiwa ghafla kwa safari za shirika la Ndege la Afrika Mashariki, Mwalimu Nyerere aliamuru kufungwa kwa mipaka ya Tanzania na Kenya.
Mwalimu alikasirika sana kwani tulikuwa katika maandalizi ya sherehe ya kuadhimisha miaka 10 ya Azimio la Arusha na pia kuzinduliwa wa CCM, hivyo wageni toka mataifa mbali mbali walikwama Nairobi, anasema Mtei.

Anasema serikali ililazimika kuwafuata Nairobi wageni hao kwa magari na kuwaleta nchini ili kushiriki sherehe hizo mbili kubwa wakati huo.
Mtei anasema licha ya kufanyika mazungumzo ya kumaliza mgogoro, ilishindikana na baadaye kupelekea kuvunjika kabisa kwa Jumuiya na mali kuanza kugawanywa.
Mtei awa Waziri wa Fedha na Mipango
Mnamo Februari 12, 1977,  Rais wa Kwanza wa Tanganyika, alimteua Edwin Mtei kuwa Waziri wa Fedha za Mipango.
 
Mtei anasema, alipoitwa na Mwalimu Jijini Dar es Salaam hakutegemea kwenda kuambiwa awe Waziri wa Fedha bali alijua ni kwenda kupata taarifa kuhusu Kenya kuzuia ndege za Afrika Mashariki.
Hata hivyo, anasema alikubaliana na uteuzi huo ambapo miongoni mwa majukumu yake ilikuwa ni kushiriki mazungumzo ya mgawanyo wa mali na madeni ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tulizungumza na mawaziri wenzangu wa Kenya na Uganda na tukabahatika kupata msuluhishi ambaye ndiye alisimamia mgawanyo wa mali na madeni,” anasema Mtei.

Majeshi ya Idd Aman yavamia Tanzania 1978
Mzee Mtei anasema moja ya mambo ambayo hatayasahau katika utumishi wake serikalini ni hatua ya aliyekuwa Rais wa Uganda, Idd Aman kuvamia Tanzania na kuanzishwa vita.
Anasema wakati huo, akiwa Waziri wa Fedha, alifanya kazi kubwa ya kutafuta fedha za kugharamia vita hivyo na baadaye kukarabati miundombinu iliyokuwa imeharibika sana.
 
Mtei anasema pia mara baada ya vita hiyo, uchumi wa nchi ulivurugika sana, masharika ya umma yalianza kudhoofika na maisha ya Watanzania yalianza kuwa magumu.
 Chanzo cha vita na Uganda
Pamoja na uchokozi wa dhahiri wa Idd Amin kwa Tanzania kwa kuvamia maeneo ya mipakani wakati huo, mzee Mtei anafichua sababu nyingine.
 Anasema mwaka 1971 Hayati Mwalimu Nyerere alisafiri na Rais wa Uganda wakati huo, Milton Obote kwenda kwenye mkutano wa nchi za Jumuiya ya madola ambao ulifanyika nchini Singapore.
Anasema Hayati Mwalimu Nyerere na Obote walikuwa marafiki sana na wakati wakirejea nchini ndipo walikuta Idd Aman amefanya mapinduzi na kujitangaza Rais wa Uganda.
Anasema wakiwa njiani kutoka katika mkutano huo, walipofika Nairobi nchini Kenya, Obote aliandamana na hayati Baba wa Taifa mwalimu Nyerere hadi jijini Dar es salaam.

Mtei anasema Obote alipewa makazi Dar es Salaam katika eneo la Msasani na serikali ya Tanzania ilikuwa inamgharamia kwa kila kitu kama rais wa nchi.
Anasema kutokana na mauaji na hali ya usalama kuwa mbaya nchini Uganda, Waganda wengi walikimbilia nchini Tanzania na kuanza kujipanga kurejea nchini kwao kuikomboa nchi yao.

Nadhani kupewa hifadhi kwa Obote na kuwapo harakati hapa nchini za kwenda kupigana Uganda, kulimuudhi Amin na ndipo alipoanza uvamizi katika mipaka yetu, anasema Mtei.
Anasema katika uvamizi huo, hali ilifikia hatua mbaya pale majeshi ya Uganda yalipomteka na kumuua aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, aliyetambulika kwa jina la Hans Pop na kuuchukua mwili wake hadi Kampala na kuuweka hadharani wakidai ni jasusi toka China.
 
Nakumbuka yule kamanda alikuwa ni mwenyeji wa Iringa ila alikuwa ni mchanganyiko wa mwafrika na mtu mweupe, hivyo ilikuwa ni rahisi kwa Amin kuendesha propaganda kama ni mchina, anasema Mtei.
Kutokana na kukithiri kwa uvamizi na propaganda hizi na Amin ndipo Hayati Mwalimu, alipotangaza vita dhidi ya Uganda.

Mtei atangaza kujiuzulu Uwaziri
Desemba 1979, Edwin Mtei, alitangaza kujiuzulu nafasi ya Waziri wa Fedha na Mipango baada ya kutofautiana na Mwalimu Nyerere.
Anasema alitofautiana na hayati Nyerere pale alipotaka kwenda kuomba mikopo nje ya nchi ili kujenga uchumi na pia kushusha thamani ya shilingi kwa shilingi 30.

Wakati ule dola moja ilikuwa ni sawa na shilingi 9 na senti 60 hivyo nikapendekeza ifike shilingi 12 na senti 40 kwa dola, kwani fedha yetu ilikuwa inashuka thamani, anasema Mtei.
Anasema pia alikuwa ameshauri kuingia ubia na sekta binafsi na mashirika ya nje katika uendeshaji wa mashirika ya umma ambayo yalikuwa yameanza kufilisika.

Baada ya ushauri huu ambao mimi niliamini ungesaidia Taifa kujiondoa katika kuyumba kwa kiuchumi hasa baada ya kuathiriwa sana na vita ya Uganda, Mwalimu alisema ushauri huo hautaki na ni bora afe kuliko kuutekeleza, anasimulia Mtei.
Anasema baada ya kauli hiyo ya Nyerere, aliona hakuna sababu ya kuendelea kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, hivyo akajiuzulu.

Nakumbuka mwaka 1978/9 hali ilikuwa mbaya sana kiuchumi, tulikosa fedha za kununua vitu nje, bei ya vyakula ilipanda, tukakosa vitu vingi muhimu, anasema Mtei.
Mtei anasema baada ya kujiuzulu aliamua kuuza nyumba yake ya jijini Dar es Salaam kuhamia   Arusha, ambapo alinunua shamba na kujenga nyumba ambayo anaishi hadi sasa.

Anasema mwaka 1986 aliteuliwa na Rais wa Awamu ya pili kwenda kuiwakilisha Tanzania na Afrika katika Shirika la Fedha dunia(IMF).
Anasema alihamia Washington nchini Marekani na kufanya kazi za ushauri wa masuala ya uchumi kwa miaka minne.
Yale yale niliyomshauri mwalimu Nyerere yaliletwa tena na IMF na tukaanza mashauriano ya kuboresha uchumi wa nchi, nilikuja kuzungumza na Rais, anasema Mtei.

Anasema baadhi ya mambo aliyoshauri yalianza kutekelezwa na serikali katika mkakati wake wa kuboresha uchumi na kukabiliana na umasikini.
Mtei anasema baada ya kukamilisha kipindi chache cha kazi, IMF alirejea nchini 1989 ambapo aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa tume ya kutazama masuala ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali na masuala ya matumizi ya serikali.
tume yangu ndio ilipendekeza kuanzishwa kwa malipo ya ongezeko la thamani(VAT) na masuala mbali mbali ya kudhibiti matumizi ya serikali,” anasema Mtei.

 Anasema taarifa ya tume hiyo ilitolewa mwaka 1991 na muda mfupi baadaye taarifa ya tume ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi ilitolewa na yeye kuwa mmoja wa waasisi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
 
 


 


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
Last Updated on Friday, 09 December 2011 12:47
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner