|
Elias Msuya JITIHADA za kuleta uhuru zilihusisha watu wengi ambao kwa njia moja au nyingine walihakikisha nchi inakombolewa kutoka kwenye kongwa la utumwa. Kati ya watu walioshiriki jitihada hizo ni pamoja na mwanasiasa mkongwe, Job Lusinde alianza utumishi wake tangu wakati wa TANU. Akieleza historia yake hivi karibuni, Lusinde anayeishi mjini Dodoma kwa sasa anasema, Mimi nilizaliwa wa hapa hapa Dodoma, nilisoma shule ya Alliance ambayo kwa sasa inaitwa Mazengo na baadaye nikaendelea na masomo ya sekondari ya Tabora boys” anasema Lusinde na kuongeza, Mwaka 1950 nilijiunga na chuo cha Makerere Uganda ambako nilisomea ualimu. Baada ya hapo nikawa mkufunzi wa walimu hadi mwaka 1954. Lusinde anaeleza sababu ya kuacha ukufunzi katika chuo hicho ili kurudi Tanzania kwaajili ya kuungana na mapambano ya kupata uhuru. Aliporudi mwaka 1955, alijiunga na shule ya Alliance kama mwalimu na wakati huo akajiunga na TANU. Kwakuwa hawakukatazwa kushiriki siasa na serikali ya kikoloni, alijiunga na TANU na kuchaguliwa kuwa katibu msaidizi katika tawi la Dodoma wakati huo ukiitwa jimbo la Kati. Aliendelea kufanya kazi za ualimu na za siasa kwa wakati mmoja. Hata hivyo Lusinde anasema kuwa shughuli za siasa alizianza akiwa bado mwanafunzi wa shule ya Alliance ambapo anasema alishirikiana na wanafunzi wenzake kuanzisha chama kiitwacho ‘Tanganyika Student African Association’. Wakati huo tulikwenda shule na vyuo mbalimbali kama vile Minaki na Tabora kukieneza chama chetu. Tulikuwa tukipinga ubaguzi katika elimu kwani wakati huo kulikuwa na shule za wazungu, wahindi na Waafrika anasema. Vilevile anasema kuwa kupitia chama chao hicho, waliandika barua kwenda Umoja wa Mataifa kueleza unyanyasaji wa wakoloni. Hata ujumne wa Umoja wa Mataifa uliotembelea Tanzania wakati huo ulifika Dodoma kukiona kikundi chao. Kikundi hicho kilichokuwa chini ya mwenyekiti wake Oscar Kambona huku Lusinde akiwa Katibu, kilijihusisha pia na mambo ya elimu na jamii ambapo kilifungua madarasa kwaajili ya wasiojuwa kusoma na kuandika. Kilisaidia pia jamii katika masuala ya afya na umasikini kwa kukusanya nguo kutoka kwenye maduka na kupeleka kwenye vituo vya afya. Ilifika mahali serikali ya kikoloni ilitukataza walimu kushiriki siasa. Mwaka 1958 Lusinde aliachana na ualimu na kujiunga na Serikali za mitaa akiwa kama afisa mtendaji. Mwaka 1959 aligombea udiwani baada ya kuanzishwa kwa mabaraza ya miji ambapo mwaka 1960 alichaguliwa na kuwa Mwafrika wa kwanza nchini kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Dodoma. Baada ya kupata uhuru Mwaka 1961, baada ya kupatikana kwa uhuru, nyota yake katika serikali za mitaa ikaendelea kuwaka baada ya kupewa uwaziri wa Serikali za mitaa kazi aliyoifanya hadi mwaka 1963 alipohamishiwa wizara ya Mambo ya ndani. Alikaa katika wizara hiyo hadi mwaka 1965 alipohamishiwa katika wizara ya Mawasiliano na uchukuzi miundombinu alipofanya kazi hadi mwaka 1969 ambapo wizara hiyo ilibadilishwa na kuwa na kuwa Wizara ya Mawasiliano, uchukuzi na kazi alipofanya kazi hadi mwaka 1975, mwaka ambao aliachana na siasa za ndani. Baada ya hapo alipelekwa kuwa balozi wa China hadi mwaka 1984 aliporudishwa nyumbani na kupelekwa Kenya kwenda kufungua ubalozi uliokuwa umevunjwa kutokana na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alifanya kazi huko kwa muda wa miaka tisa na kustaafu. Baada ya hapo amekuwa akiongoza bodi za mashirika mbalimbali kama vile Hifadhi za Taifa (Tanapa), Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na mjumbe wa bodi ya Tanzania Parent Association. Ameendelea pia kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM. Je, malengo ya kupata uhuru yamefikiwa? Kwa mujibu wa Lusinde, madhumuni makubwa ya TANU yalikuwa ni kuwatayarisha Watanganyika kujitawala, kuondoa ubaguzi, ukabila na mambo yote yanayozuia umoja yaliyokuwepo kwenye serikali ya ukoloni. Kulikuwa pia na lengo la kuwatia wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara kwa kuanzisha vyama vya ushirika kama vile NUTA, Juwata na vinginevyo. anasema. Miaka 50 baada ya Tanzania kuwa huru, Lusinde anasema kwa ujumla malengo yamefanikiwa licha ya kuwepo kwa kasoro kadhaa. Tumefanikiwa kudumisha umoja na uhuru, tumedumisha heshima, tumeondoa umasikini kwa kuwainua wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara. Ukiyachukua kwa ujumla, tumefanikiwa mno. anasema Lusinde. Pamoja na mafanikio hayo, Lusinde anasema kuwa kuna changamoto nyingi zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na kuharibika kwa ushirika na kuporomoka kwa misingi ya Azimio la Arusha. Kama kuna mambo ambayo yamevurugika ni kuanguka kwa misingi ya Azimio la Arusha. Nadhani bado ni njia ya kuwasaidia wananchi kwa sasa. Hakuna wakati ambao hifadhi yetu ya fedha ya nje ilikuwa kubwa kuliko wakati wa ujamaa na kujitegemea. Wakati ule mazao ya biashara kama vile pamba, kahawa na chai yalikuwa na bei ya juu tofauti na sasa anasema. Licha kutoa sababu ya kuanguka kwa sera ya ujamaa na kujitegemea kuwa ni kutoka na kubadilika kwa mfumo wa kidunia, anasema mfumo wa sasa wa soko huria unahitaji nguvu zaidi ya kufuata tu sheria, Rais Jakaya Kikwete amejitahidi kuongoza nchi kwa kufuata utawala wa sheria, lakini ujue sheria zinachukua muda mrefu. Si ajabu ukiwashitaki wahujumu uchumi watatokea mawakili kuwatetea hadi washinde, rais anapaswa kuchukua hatua kali zaidi, anasema Lusinde na kuongeza, Pakistan ilipopata uhuru, ilifika mahali wakakithiri kwa rushwa. Kuna kiongozi mmoja wa majeshi aliamua kuipindua nchi na kuwakamata wale wote waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi na kuwatupa jela. Hata Marekani inayosifika kwa demokrasia duniani ina weka watu vizuizini huko Guantanamo Cuba na kwingineno ili tu kulinda usalama wake. Ni lazima rais achue hatua za haraka ili kulinda usalama wa nchi. Akizungumzia uzoefu alioupata wakati wa Mwalimu Nyerere, anasema utawala wa sasa umepwaya, Huko nyuma tulitumia sheria ya kizuizini tukawanyoosha watu. Baadaye sheria hiyo ikabadilishwa, ikawa ya uhuijumu uchumi. Sheria tunazo za kupambana na hali hii, lakini sijui serikalini kuna nini. Nayazungumza haya kwa umakini mkubwa. Anasema na kuongeza, Tatizo letu ni kuachia biashara huria, huku vyombo vya kudhibiti vikiwa na meno butu, hata sheria zetu nyingi ni butu. Ewura, Takukuru vyoteni butu. Halafu watendaji wa serikali wamekuwa wakilumbana kwenye vyombo vya habari, badala ya kukutana na kushauriana alisema. Hata hivyo Balozi Lusinde anasifu mkakati wa CCM wa kujivua gamba akisema kuwa utakirudisha chama kwenye mstari. Tusubiri tuone, mimi naamini kabisa CCM itaimarika kama yale waliyokubaliana kujisafisha watayatekeleza” anasema Lusinde
|