|
Na Fredy Azzah SIKU nne zijazo mwaka 2011 utafikia tamati.Nini kimejiri kuhusu elimu kwa mwaka mzima? Makala haya yanadurusu baadhi ya matukio muhimu ya kielimu yaliyotokea kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu.
Januari 26 Matokeo kidato cha pili yatoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilitoa matokeo rasmi ya mtihani wa kidato cha pili uliofanyika mwaka 2010, yakionyesha kushuka kwa ufaulu kwa asilimia 3.52 ikilinganishwa na mwaka 2009. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na wizara hiyo, watahiniwa 171,395 sawa na asilimia 38.20% walishindwa mtihani huo wakiwamo wasichana 87,593 na wavulana 83,802. Januari 27 Wasichana waongoza mtihani wa kidato cha nne Siku moja baadaye, wizara hiyo hiyo ikatangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2010 yaliyoonyesha wasichana kufanya vizuri kuliko wavulana. Hata hivyo, huu ulikuwa mwaka ulioanza na taarifa za kusikitisha kuhusu matokeo hayo, kwani zaidi ya asilimia 80 ya watahiniwa walipata madaraja ya nne na sifuri, hali iliyochochea mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa elimu nchini. Machi 16 Wasichana wote wachaguliwa kidato cha tano Wanafunzi wa kike wote waliofaulu kidato cha nne kwa kupata alama stahiki, walipangiwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za sekondari na vyuo vya Serikali. Aprili 28 Shule za Serikali zangara kidato cha sita Siku hii ilikuwa siku nzuri kwa viongozi wa elimu serikalini baada ya shule zake za sekondari kung’ara katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2011, huku wanafunzi wake saba wakiwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa. Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk Joyce Ndalichako aliwataja wanafunzi 10 bora kuwa ni Muhagachi Chacha (Kibaha Sekondari), Samuel Katwale, George Felix (Mzumbe Sekondari), Amiri Abdalah, Comman Nduru na Kudra Baruti (Feza Boys), Aron Gerson, Shaban Omary na Francis Josephat (Tabora Boys), George Assenga (Majengo Sekondari). Juni 14 UDOM wasababisha taharuki Bungeni Taharuki kubwa ilitawala katika viwanja vya bunge baada ya mabomu kusikika karibu na ukumbi wa bunge ambapo kikao cha tatu katika mkutano wa nne wa Bunge kilikuwa kikiendelea. Hali hiyo ilitokana na kitendo cha askari wa kuzuia vurugu wa Jeshi la Polisi, kupiga mabomu kwa ajili ya kuzuia Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma waliotaka kuvamia ukumbi wa Bunge, ili kuonana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Lengo la maandamano hayo ilikuwa kumshinikiza Waziri Mkuu,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa wajiuzulu kwa kile walichodai kuwa wamewadanganya Julai mosi CWT yaitega Serikali Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba aliipa Serikali mwezi mmoja kuanzia Julai kuwalipa Sh13 bilioni wanazodai walimu vinginevyo ingetangaza mgomo wa walimu nchi nzima. Hatua hiyo ilitokana na kikao cha dharura cha Baraza la Taifa la CWT, kilichofanyika Morogoro ili kujadili matatizo ya walimu. Akizungumza na wanahabari, Mkoba alisema fedha hizo ni madeni yanatokana na malimbikizo ya mishahara na madai mengine. Julai 19 Posho elimu ya juu yapanda Kilio cha wanafunzi wa elimu ya juu kilisikilizwa kwa kiasi fulani na Serikali baada ya kukubali kuongeza kiwango cha fedha za kujikimu kwa wanafunzi hao kutoka Sh5,000 iliyokuwa ikilipwa awali mpaka Sh 7,500 kwa siku. Kauli hiyo ilitolewa bungeni Julai 19 na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa, alipokuwa akisoma hotuba yake ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara yake kwa mwaka 2011/12. Kawambwa alisema kiasi cha Sh77.8 bilioni kitatumika kuwapa posho wanafunzi 91,568 wa elimu ya juu wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.Aidha, alisema kiasi hicho pia kinajumuisha posho kwa wanafunzi wanaosomea shahada za Uzamili na Uzamifu.
Septemba mbili
Maelfu wachaguliwa vyuo vikuu
Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) ilitangaza majina ya wanafunzi 37,924, ambao ni sawa na asilimia 69.3 waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka 2011/12, kati ya wanafunzi 48,477 walioomba.
Wakati TCU ikitoa idadi hiyo ya wanafunzi waliochaguliwa, Bodi ya Mikopo ya Vyuo vya Elimu ya Juu (HELSB), nayo ikatangaza bajeti ya Sh317.8 bilioni zitakazotumika kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi hao ambazo ni ongezeko la Sh 80 bilioni ikilinganishwa na Sh 237.8 bilioni zilizotengwa mwaka 2010/11.
Oktoba Maadhimisho wa miaka 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Sambamba na sherehe za uhuru wa Tanzania bara, Oktoba mwaka huu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kiliadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961. Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, yalifungwa na Rais Jakaya Kikwete pamoja Yoweri Kaguta Museven ya Uganda. Awali tangu mwanzoni mwa mwaka, vitivo, vyuo, shule na taasisi mbalimbali za chuo hicho kikongwe nchini,viliadhimisha tukio hilo kwa kuandaa maonyesho ya aina mbalimbali, mihadhara na mijadala kwa umma.
Desemba 14 Udanganyifu darasa la saba Desemba 14, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitangaza matokeo ya mitihani ya darasa la saba ikieleza kuwa wanafunzi 9000 wamefutiwa matokeo kutokana na kugundulika kufanya udanganyifu. Sambamba na hilo, akitangaza matokeo hayo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema Serikali imeamua kuwapima tena wanafunzi watakaopangiwa katika shule za Serikali ili pamoja na mambo mengine kuwabaini wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu. Mulugo alisema wanafunzi waliofutiwa mtihani huo ni 9,736 na kuwa utaratibu wa kuchuja wale waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza utaanza rasmi Januari mwakani.
|
Comments
Lasivyo Taifa litakua naidadi kubwa ya [NENO BAYA] ambao u[NENO BAYA] ngio chazo cha umasikini.