MwanzoContactsEmail
Home Michezo Kandanda Yanga, JKT vita kubwa leo
BOOKMARK THIS PAGE
Yanga, JKT vita kubwa leo  Send to a friend
Saturday, 28 January 2012 09:27

Sosthenesn Nyoni
BAADA ya kushindwa kuwaporomosha kileleni mwa msimamo mahasimu wao wakubwa Simba kufuatia sare ya mabao 2-2 na Moro United katika mechi ya kwanza ya ufunguzi wa duru la pili, mabingwa watetezi Yanga, leo wanashuka dimbani kukwaana na 'majeruhi' JKT Ruvu katika mechi ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mbali ya vita hiyo isiyotabirika, patashika nyingine itakuwa kwenye Uwanja wa Mlandizi, Pwani ambapo wenyeji, Ruvu Shooting atakwaruzana na Kagera Sugar, huku Villa Squad ikipepetana na Toto Africans katika pambano litakalofukuta kwenye Uwanja wa Azam Chamanzi.

Lakini ni wazi kuwa macho na masikio ya wapenzi wengi wa soka yataelekekwa kwenye Uwanja wa Taifa yakiwa na shauku ya kujua kipi kitatokea safari hii baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza kushuhudiwa JKT Ruvu ikiilaza Yanga bao 1-0.

Yanga iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 28 nyuma ya vinara Simba wanaoongoza kwa kuwa na pointi 31 na itawalazimu kufanya kazi ya ziada kushinda mchezo huo ili kupunguza pengo la pointi.

Kwa upande wao, Maafande hao wanashika nafasi ya nane wakiwa na pointi 16 kufuatia kucharazwa bao 1-0 na Polisi Dodoma katika mechi yake ya mwisho.

Ni wazi kocha Kostadin Papic atakuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha kikosi chake hakifanyi tena makosa yaliyowanyima ushindi kwenye mechi ya sare ya 2-2 dhidi ya Moro United.

JKT inayoundwa na wachezaji wengi chipukizi, imeonyesha kuwa si timu ya kubeza kutokana na ufundi wa kucheza kwa kasi na bila kuchoka.

Kazi kubwa itakuwa kwa viungo wa Yanga Haruna Niyonzima 'Febregas' na Juma Seif Kijito kutengeneza mipira mizuri kwa washambuliaji, Keneth Asamoah  Davies Mwape na Jerry Tegete.

Kocha wa JKT Ruvu Charles Kilinda, anajivunia kurejea kwa washambuliaji wake waliokuwa kwenye mafunzo ya kijeshi, Hussein Bunu, Bakari Kondo na Amos Mgisa ambao hakuna shaka ndio watakaokuwa wakipanga mipango yote ya kuondoka na pointi tatu.

Kwa upande wa ngome, kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuwa na mabadiliko kidogo, ambapo mlinzi wa kulia Godfrey Taita kwa vyovyote vile ataziba pengo la Shadrack Nsajigwa mwenye adhabu ya kadi nyekundu.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Tanzania(TFF)limesema pambano baina ya Yanga na Ruvu Shooting litapigwa kuanzia majira ya saa 12 jioni badala ya saa 10 jioni.

Afisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mabadiliko hayo ya muda yamekuja kufuatia Uwanja huo kuwa katika ratiba nyingine ya matumizi ikihusisha mazoezi ya timu ya taifa ya wanawake ya Namibia

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner