
| Mali, Ghana kazi kubwa | Send to a friend |
| Saturday, 28 January 2012 09:24 |
|
MECHI ya watani wa jadi kati ya Mali na Ghana itapigwa leo huko Franciville nchini Gabon katika mechi ya kundi D kuwania kuingia hatua ya robo fainali ya mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika 2012. Timu hizi mbili zinafahamiana, ambapo miaka mitatu iliyopita zilijikuta zikipangwa kundi moja katika hatua ya kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia na Ghana ilishinda mechi ya kwanza, lakini timu hizo ziliporudiana zilitoka sare. Mali wanataka kuitumia mechi hii kulipiza kisasi cha kufungwa na Ghana katika mechi waliyokutana miaka mitatu iliyopita ili kuingia hatua ya robo fainali, huku Ghana inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka huu pia ikitaka kushinda na kuingia robo fainali. Timu zote mbili zina nafasi ya kuingia hatua ya robo fainali kama zikishinda kwa sababu katika mechi ya kwanza ya kundi hilo Ghana iliifunga Botswana bao 1-0 pia Mali iliifunga Guinea bao 1-0 ambao vilevile ni watani wao wa jadi. Ghana inaingia katika mechi ya leo huku ikiwakosa mabeki wake muhimu ambao ni nahodha wa timu hiyo, John Mensah na Isaac Vorsah ambao wote wanatumikia kadi walizopewa, ambapo kocha wa Ghana, Goran Stevanovic anatarajiwa kuwachezesha mabeki wake vijana Jonathan Mensah na John Boye ili kuziba mapengo ya mabeki hao. Naye kiungo wa Mali anyechezea klabu ya Barcelona, Seydou Keita akiizungumzia mechi ya leo alisema: "Ghana itabaki kuwa timu inayopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika kundi letu, lakini siyo kama Ghana haifungiki." Alisema: "Lengo letu ni kuhakikisha tunacheza kwa uwezo wetu na kupata matokeo mazuri kwa sababu Mali kama timu ya Taifa hatujapata mafanikio katika soka kwa hiyo mechi hii dhidi ya Ghana ni muhimu kwetu kufanya vizuri ili tubadilishe historia ya soka letu." Kwa upande wa kocha wa Mali, Alain Giresse yeye alisema: "Ghana ni timu imara na itakuwa kosa tukiidharau, Ghana inao wachezaji wenye kiwango cha juu, lakini lengo letu ni kupata pointi tatu kutoka kwao." Wakati huo huo Waziri wa Michezo wa Ghana, Kofi Humado ametembelea kambi ya timu ya Taifa ya Ghana na kuahidi bajeti ya timu hiyo itaongezwa, ambapo bajeti ya awali ya Ghana iliyotolewa na serikali ilikuwa ni dola 5.5 milioni. Je Unajua? * Ghana inatarajiwa kuwapa zawadi ya dola 90,000 kwa kila mchezaji kama itafanikiwa kutwaa ubingwa wa fainali hizi za Afrika. * Ghana itaingia robo fainali endapo itawafunga Mali na Guinea ikishindwa kuwafunga Botswana. * Ghana imecheza mechi nyingi za kirafiki (9) kabla n ya fainali hizi za Afrika kuliko wapinzani wao Mali ambao walicheza mechi mbili tu za kirafiki. * Mali inafahamika pia kwa jina la The Eagles, wakati Ghana inafahamika pia kwa jina la The Black Stars. * Timu hizi mbili zilikuwa katika kundi moja katika hatua za makundi za kuwania kufuzu kushiriki fainali za kombe la dunia na fainali za Afrika mwaka 2009. |













