MwanzoContactsEmail
Home Michezo Kandanda Afrika yaomboleza vifo vya mashabiki 74
BOOKMARK THIS PAGE
Afrika yaomboleza vifo vya mashabiki 74  Send to a friend
Thursday, 02 February 2012 21:54

CAIRO, Misri
SHIRIKISHO la Soka Afrika CAF limetangaza dakika moja ya maombolezo kwa mechi zote za robo fainali za Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwishoni mwa wiki ikiwa ni ishara ya kuwakumbua watu waliokufa kwenye vurugu za uwanjani nchini Misri.

Watu 74 wamepoteza maisha na wengine 1,000 kujeruhiwa wakati mashabiki wa timu ya  Masry na Al-Ahly kuvamia uwanja na kuanza kupigana katika mji wa Port Said, nchini Misri, siku ya Jumatano.“Soka ya Afrika imepata msiba mkubwa,” alisema Issa Hayatou, rais wa CAF katika ujumbe wake alioutuma kwa Shirikisho la Soka la Misri.

Mechi za robo fainali za Fainali za Mataifa ya Afrika zitachezwa Equatorial Guinea na Gabon hapo Jumamosi na Jumapili. Misri iliyotwaa taji hili mara tatu mfululizo, mwaka huu ilishindwa kufuzu kushiriki fainali za mwaka huu.

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Ndani wa Misri, Mohammed Ibrahim amemfukuza kazi mkuu wa usalama Essam Samak baada ya tukio hilo.Huu ndio msiba mkubwa zaidi nchini Misri kuwahi kutokea kwenye uwanja wa kandanda, alielezea Naibu Waziri wa afya nchini Misri.

“Huu ni msiba wa kusikitisha mno”, alisema Hesham Sheiha alisema Naibu huyo Waziri wa afya nchini Misri kupitia matangazo ya televisheni.

Kati ya waliokufa ni pamoja na maafisa wa usalama.Mwandishi wa BBC anaelezea kwamba ukosefu wa usalama mkali ambao hudumishwa kwa kawaida huenda ikawa ni jambo ambalo lilichangia kutokea ghasia hizo.

Polisi nchini Misri wametulia mno tangu kufanyika maandamano yaliyomtoa Rais Hosni Mubarak madarakani.

Katika mechi hiyo ya Jumatano, timu ya Port Said, Masry ilipata ushindi wa mabao 3-1.

Walioshuhudia walielezea kwamba kulikuwa na hali ya wasiwasi muda wote wa mechi hiyo, tangu shabiki mmoja wa Al-Ahly alipoinua bango ambalo inadaiwa lilikuwa linawatukana mashabiki wa timu ya nyumbani.

Katika mitandao ya jamii, licha ya kutokuwapo ushahidi, uvumi umekuwa ukienea kwamba maafisa wa usalama walikuwa wanapanga njama ya kupambana na mashabiki wa Al-Ahly.Maafisa wachache wa polisi walijitahidi kuwapa ulinzi wachezaji, lakini hawakufanikiwa kabisa.

Sehemu moja ya uwanja ilichomwa moto.Maofisa wanaohusika wameelezea kwamba vifo vingi vilitokana na watu kupata majeraha makubwa ya kichwa kwa kupigwa au kukatwa, na wengine kuzimia hadi kufa wakati wa mkanyagano.Ndege za helikopta zilitumwa hadi Port Said kuwasafirisha hadi hospitali mashabiki waliojeruhiwa.

"Huu si mpira. Hivi ni vita na watu wanakufa mbele yetu", alisema mchezaji wa Al-Ahly, Mohamed Abo Treika.

Mbunge wa Port Said, Albadry Farghali, aliwalaumu maofisa wa usalama."Walikuwa wapi haya yote yakitokea?"

"Watu wa Mubarak bado wako uongozini. Kiongozi wa utawala ameng'atuliwa, lakini watu wake bado wapo madarakani", alielezea kupitia televisheni.

"Usalama uko wapi? Serikali iko wapi?"

Mjini Cairo, mwamuzi alisitisha mechi nyingine, alipoarifiwa juu ya ghasia za Port Said.Jambo ambalo liliwafanya mashabiki kuchoma moto sehemu fulani za uwanja.Mechi zote za Ligi Kuu zimefutiliwa mbali na bunge jipya la Misri jana lilitakutana katika kikao cha dharura kuujadili msiba huo.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Misri, Kamal el-Ganzouri amewatimua kazi viongozi wote wa Shirikisho la Soka la Misri EFA baada ya kutokea tukio hilo.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner