MwanzoContactsEmail
Home Michezo Kandanda Poulsen: Tutashambulia zaidi
BOOKMARK THIS PAGE
Poulsen: Tutashambulia zaidi  Send to a friend
Thursday, 02 September 2010 21:50

Samson Mfalila, Algeria na Angetile Osiah

TANZANIA leo inaanza tena harakati za kusaka tiketi ya kushiriki kwa mara ya pili fainali za Mataifa ya Afrika itakapovaana na Algeria mjini Blida huku wenyeji wakionyesha kuwa na wasiwasi dhidi ya wageni.

Stars ilifuzu kwa mara ya pekee kucheza fainali hizo mwaka 1980 wakati zilipofanyika Nigeria, lakini baada ya Mbrazil, Marcio Maximo kujaribu bila ya mafanikio mara mbili, Mholanzi Jan Paulsen anaanza kampeni hiyo ngumu ugenini katika mechi ya kwanza ya Kundi D ambalo pia linashirikisha nchi za Morocco na Afrika ya Kati.

Timu ya Tanzania, Taifa Stars iliwasili mjini Blida juzi na ilitarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho jana usiku kwenye Uwanja wa Mustapha Tchaker ambao utatumiwa kwa mechi ya leo itakayoanza saa 4:00 usiku kwa muda wa Algeria.

Hiyo itakuwa ni moja ya mechi zitakazochezwa wikiendi hii wakati mataifa 44 yatakapokuwa yakipambana kutafuta tiketi 14 za kucheza fainali za CAN 2012 zitakazofanyika Gabon na Equatorial Guinea.

Mshindi wa kwanza katika kila kundi atapata tiketi ya kushiriki fainali hizo, wakati mshindi wa pili wa kundi la Togo pia atafuzu pamoja na timu mbili bora za pili zitakazotoka katika makundi mengine 10, hali inayoifanya mechi ya leo kuwa na umuhimu mkubwa kwa Stars ugenini.

"Algeria ni timu inayocheza soka safi," alisema kocha wa Taifa Stars, Jan Paulsen mara baada ya kuwasili alipoongea na gazeti la Le Soir d'Algerie. "Ni timu iliyoonyesha uwezo mkubwa kwenye Kombe la Dunia. Matokeo yake kwenye mechi dhidi ya Uingereza na Marekani yanatosha kutuonyesha staili yao nzuri.

"Lakini haitakuwa rahisi. Tutafanya kazi kwa umakini mkubwa ili tuweze kupata kile tulichokifuata huku."

Kocha huyo amemuacha mshambuliaji Jerry Tegete kutokaa na kutoonyesha kiwango kikubwa na kipa Juma Kaseja na atalazimika kumtumia Mrisho Ngassa kuwa mshambuliaji pekee katika mechi hiyo ambayo ulinzi utakuwa muhimu sana.

Akizungumza na Mwananchi hapa kwenye , Poulsen alisema: "Tutacheza kwa kushambulia zaidi...hatutahofia majina ya wachezaji wa Algeria na hatutacheza kwa kujihami.

"Nimefuatilia kwa karibu na kuangalia rekodi ya Algeria, hawatishi sana," alisema kocha huyo huku akimtaraji Shaaban Kado kusimama langoni katika mchezo huo.

Nyuma ya Ngassa anatarajiwa kuwa Mussa Hassan Mgosi, wakati kiungo kitaundwa na Nizar Khalfan, Abdi Kassim, Nurdin Bakari na Henry Joseph, huku ngome ikiongozwa na Nadir Haroub "Cannavaro", akisaidia na Aggrey Moris, Shadrack Nsajigwa na Idrissa Rajab.

Kocha wa Algeria, Rabah Saadane amekuwa akisisitiza umuhimu wa kushinda mechi hiyo ili kurejesha matumaini kwa mashabiki baada ya Algeria kufanya vibaya kwenye fainali za Mataifa ya Afrika na baadaye kufungwa mabao 2-1 na Gabon katika mechi ya kirafiki.

Hata hivyo, kocha huyo amekuwa akionya kuwa timu yake haina sababu ya kuidharau Tanzania, akisema kuwa ni timu inayoheshimika na ambayo haitetereki inapokutana na timu kubwa katika soka.

"Tunajua hasa kile tunachotakiwa kukifanya. Wachezaji wote na mimi tutaingia uwanjani Ijumaa kwa ajili ya kuishinda Tanzania," alisema Saadane akikaririwa na gazeti la L'Expression.

Saadane ana kila sababu ya kutegemea ushindi kwa sababu wachezaji wake walio barani Ulaya na Asia na hasa washambuliaji wamekuwa wakifanya vizuri katika mechi za hivi karibuni, kwa mujibu wa L'Expression.

Rafik Djebbour amekuwa kwenye kiwango kizuri kwenye klabu yake ya AEK Athenes ya Ugiriki, wakati Abdelmalek Ziaya alifunga bao lake la tatu msimu huu kwenye klabu yajke ya Ittihad Djeddah wakati ilipocheza na El Hazm mwishoni mwa wiki iliyopita.

Abdelkader Ghezzal alishiriki kwenye mechi ambayo klabu yake ya Baria ya Italia iliishinda Juventus kwa bao 1-0. Kocha Saadane pia atakuwa akimtegemea Karim Matmour ambaye hakucheza mechi dhidi ya Gabon kutokana na kuwa majeruhi. Mshambuliaji huyo wa Borussia Dortmund ya Ujerumani ameeleza kuwa yuko fiti kwa mechi ya leo.

Katika kiungo, Karim Ziani, ambaye anachezea klabu ya Wolfsburg ya Ujerumani na ambaye alipumzishwa kwenye mechi dhidi ya Gabon, anarejea akiwa kwenye kiwango kizuri kutokana na kuchezeshwa mara kwa mara na klabu yake tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

Magazeti mengi ya Algeria yaliwakariri wachezaji wa timu hiyo wakieleza umuhimu wa kushinda mechi ya leo, huku wakionya kuwa hawataidharau Taifa Stars hata kidogo.

"Hii si mechi ya kuamua hatma yetu, lakini ni muhimu. Kwa sasa hakuna tena timu ndogo na tunatakiwa kufanya kazi kubwa ili kujihakikishia ya kuwa washindi kwenye kundi letu," alisema kiungo Karim Ziani.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Zoheir Djelloul alisema: "Wachezaji wetu wana uwezo wa kupata matokeo mazuri. Tunatakiwa tusiidharau Tanzania ambayo ni timu inayoheshimika. Hii ni timu ambayo inacheza bila woga inapokutana na timu za mataifa makubwa."

Kocha Saadane, akiongea na gazeti la Le Soir d'Algerie alisema:"Tanzania ni timu inayoheshimika ambayo haifai kabisa kuidharau. Ni timu ambayo inacheza bila ya wasiwasi inapokutana na timu zilizo juu kwa ubora. Ilipokutana na Brazil licha ya kufungwa  mabao mengi (mabao 5-1), ilionyesha uwezo mkubwa."


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner