
| Msanii wa muziki wa dansi afariki | Send to a friend |
| Wednesday, 28 December 2011 22:02 |
|
MWANAMUZIKI mahiri nchini, Andy Swede amefariki jana alfajiri na anatarajia kuzikwa leo kwenye Makaburi ya Sinza jijini Dar es Salaam.Kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa marehemu, Lugano Mbwina, alisema marehemu alifariki baada ya kuugua ghafla ugonjwa wa pumu. "Ni kweli, mwenzetu amepatwa na mauti wakati akipewa matibabu kwenye Hospitali ya Maria Stopes," alisema Mbwina kuongeza kuwa ugonjwa huo umekuwa ukimsumbua muda mrefu. "Hakuonekana kuwa na tatizo lolote kubwa, lakini ghafla hali ilibadilika baada ya kushindwa kupumua vizuri na alipofikishwa Hospitali alifariki," alisema Mbwina. Kifo cha Swede maarufu kama 'Ambassador' kilithibitishwa pia na mwanamuziki mkongwe Mafumu Bilali aliyemuelezea marehemu kama mchapakazi hodari. Bilali alisema marehemu ameshiriki kikamilifu katika kukuza sanaa ya muzuki nchini, na hivi karibuni alikuwa nchini Marekani kwa ziara ya muziki akiongozana na King Kiki. "Tulikuwa wote bendi ya Makassy, tukatoka na kuanzisha bendi za MK Group, Bicco Stars, Zanzibar Sound, Twanga Pepeta, Kilimanjaro Connection, kabla ya kuanzisha African Band ambayo alikuwa akiitumikia mpaka kifo chake. Bilali alisema kesho wanamuziki mbalimbali nchini watakusanyika Sinza unapofanyika msiba na kuimba nyimbo mbalimbali kama sehemu ya kumuenzi kabla ya safari ya kwenda makaburini kuzika. |














