
| TOC, TPC warumbana | Send to a friend |
| Tuesday, 24 January 2012 20:24 |
|
WACHEZAJI wa timu ya taifa ya michezo ya watu wenye ulemavu 'Paralimpiki', hawatahusiki na kambi ya mwezi mmoja itakayofanyika Uingereza kwa ajili ya maandalizi ya Olimpiki. Kambi hiyo ambayo itagharamiwa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kwa wanamichezo wa Tanzania watakaofuzu kushiriki Olimpiki inalenga michezo ya Riadha, Judo, Ngumi na Kuogelea. Pamoja na kwamba Paralimpiki ni miongoni mwa michezo ya Tanzania inayotazamiwa kushiriki Olimpiki itakayoanza Julai 27, wachezaji wake hawatapata safari hiyo. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema udhamini huo hautowalenga wachezaji wa Paralimpiki ambao wanatakiwa kuhudumiwa na Kamati yao ya Kimataifa (IPC) yenye jukumu la kuwasaidia. Katika hatua nyingine Kamati ya Paralimpiki Tanzania (TPC) imeonekana kuwa tofauti na msimamo huo na kusema kwamba ofa hiyo utolewa kwa wanamichezo wote watakaofuzu kushiriki Olimpiki hivyo na wao ni wajibu kupewa endapo watapata vigezo hivyo. Katibu Mkuu wa TPC, Iddy Kibwana alisema ofa hiyo imetolewa na nchi mwenyeji wa michezo hiyo kwa wanamichezo watakaopata fursa ya kushiriki Olimpiki hivyo na wao Paralimpiki ni haki yao kupewa. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotarajiwa kushiriki Olimpiki licha ya kwamba hadi sasa hakuna mchezo uliojihakikishia kushiriki hadi pale wanamichezo wake watakapofuzu. |














