MwanzoContactsEmail
Home Michezo Michezo ya Kimataifa Barca majeruhi kibao
BOOKMARK THIS PAGE
Barca majeruhi kibao  Send to a friend
Saturday, 28 January 2012 09:21

BARCELONA, Hispania
BARCELONA ikiwa bado na furaha ya kuwatupa nje ya mashindano ya Kombe la Copa del Rey mahasimu wao wakubwa, Real Madrid sasa inakabiliwa na majeruhi kibao, huku leo ikishuka dimbani ugenini kwa Villarreal katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania.Andres Iniesta na Alexis Sanchez wote waliumia katika mechi ya sare ya 2-2 dhidi ya Madrid iliyowapa ushindi wa jumla mabao 4-3.

Hii ina maana, Barca watashuka kwenye Uwanja wa El Madrigal bila wachezaji sita akiwamo David Villa, Ibrahim Afellay na Andreu Fontas, ambao tayari ni majeruhi, huku Seydou Keita akiwa na timu ya taifa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.Lakini pia imethibishwa kuwa Iniesta ana matatizo ya misuli na huenda akawa nje ya uwanja kwa muda wa wiki tatu.

"Kwa sasa, hatuna wachezaji wengi, lakini ni lazima tusonge mbele," alisema Pep Guardiola.
Pamoja na kwamba Villarreal wako nafasi ya 17 kwenye msimamo wakiwa sawa kwa pointi na Granada katika mstari hatari, lakini kwa kiwango walichoonyesha kwa siku za hivi karibuni kinatia hofu.

Timu hiyo ilisogea juu kidogo ya mstari wa hatari kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sporting Gijon, huku kiungo mkongwe Marcos Senna akijiandaa kuikabili vilivyo Barca.Katika mechi nyingine, Atletico Madrid ambayo imekuwa na mwanzo mzuri tangu kujiunga kwa Diego Simeone, itakuwa nyumbani kwa Osasuna.

"Ni lazima tuifikirie mechi dhidi ya Osasuna kwa sababu tumepita kwenye wakati mgumu na sasa tunaendelea kuonyesha kiwango kizuri, muhimu ni kutorejea tena nyuma," alisema Simeone.

"Osasuna ni timu ngumu lazima tucheze kwa kujiamini na kupata ushindi ili tuendeleze mwanzo mzuri."
Atletico imepanda mpaka nafasi ya nane kwenye msimamo, ikiwa pointi moja nyuma ya wanaoshika nafasi ya sita Osasuna.

Valencia, wakiwa kwenye nafasi ya tatu watakumbana na Racing Santander wakitarajia kuendeleza pengo lao la pointi nne dhidi ya Levante watakaokuwa nyumbani kwa Getafe.

Espanyol, katika nafasi ya tano watakuwa na mshikeshike dhidi ya Real Mallorca katika mechi itakayochezwa leo.
Pia mechi ya leo itashuhudia Rayo Vallecano wakiwa nyumbani kuikaribisha Athletic Bilbao, huku kesho Sporting watakuwa nyumbani kwa Real Sociedad na  Sevilla watakwenda kupambana na Malaga.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner