|
LONDON, England MKURUGENZI wa Liverpool, Ian Ayre amesema angependa kuona upinzani wa kweli kati ya klabu yake na Manchester United badala ya chuki kuelekea mechi yao leo.
Liverpool 'The Reds' wanakuwa wenyeji wa United kwenye Uwanja wa Anfield katika mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA.
Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza tangu Luis Suarez alipoadhibiwa kutocheza mechi nane kufuatia kudhalilisha kibaguzi beki wa United, Patrice Evra katika mechi ya sare ya 1-1 Oktoba mwaka jana.
Ayre alisema: "Tusishawishike kusikiliza kelele na maneno ya kishabiki na kutufanya kujenga chuki badala ya kuonyesha ushindani wa kweli."
Kuna hofu ya kukosekana kwa mahusiano mazuri kati ya mashabiki wa timu hizo tangu Suarez kupewa adhabu hali iliyoongeza msuguano wa kishabiki.
Liverpool na Manchester United zimeshacheza mara 10 katika michuano ya Kombe la FA, huku United ikishinda mara saba ikiwemo fainali mbili za mwaka 1977 na 1996.
Kufuatia kufungiwa Suarez, ambaye adhabu yake ya kutocheza mechi nane inamalizika Feebruari 11, Chama cha Soka England, kimezitaka klabu hizo kuweka mazingira mazuri ya mahusiano ya kishabiki kabla ya mechi hiyo.
Kocha wa United, Alex Ferguson ameandika walaka mashabiki wake akitaka wajiheshimu watakapokuwa kwenye dimba la Anfield kushuhudia mechi hiyo.
Lakini akawataka mashabiki wake kutochoka kuishangalia kwa nguvu timu yao muda wote wa mchezo huo wa upinzani mkubwa.
Ayre anaamini kuwa mechi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa katika mazingira mazuri.
"Ni Kombe la FA, ni mashindano makubwa England yenye historia ndefu na kila mtu anaelekeza mawazo yake kwenye mechi hii."
"Tuna upinzani mkubwa na Manchester United, lakini wale wenye kujiheshimu pia wanapaswa kuwaheshimu wengine, kwa sababu ni timu kubwa mbili katika soka la England. Ni timu zenye mafanikio makubwa.
"Ni mechi ya ushindani kati ya timu mbili, lakini si yenye kujenga chuki. Hakuna nafasi ya chuki na visasi kwenye soka."
Mshambuliaji wa Liverpool, Dirk Kuyt amesema nia yake kubwa leo ni kuona Manchester inatupwa nje ya michuano ya Kombe la FA kama walivyofanya kwa timu nyingine ya jiji la Manchester, Manchester City. Baada ya kufanikiwa kusonga mbele na kucheza hatua ya nusu fainali ya Kombe la Carling kwa kuwatupa nje City, sasa wanajiandaa kulivuruga kabisa jini la Manchester. "Liverpool wako tayari kwa mechi zaidi ya inavyoweza kuonekana," alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi. "Ni furaha siyo tu kuiondoa nje ya mashindano City, lakini ni zaidi kama tutaiondoa Manchester United kwenye michuano ya Kombe la FA."Tuliweka mikakati mizuri dhidi ya City Jumatano na kupata ushindi, sasa ni lazima kuhakikisha kuwa tunacheza kama tulivyofanya awali na nina hakika tunaweza. "Tunaweza kuwa na furaha kwa kile tutakachokipata kwenda Uwanja wa Wembley, kuna mechi ngumu inakuja ni lazima kuwa makini. "Tumeshazoea kucheza kila baada ya siku tatu toka tulipocheza Ligi ya Mabingwa."Tunacheza dhidi ya timu kubwa kila baada ya siku mbili, hivi ndivyo Liverpool inapaswa kuwa. "Inapendeza kuwa na michezo miwili mikubwa ndani ya wiki moja, na tayari tunajindaa kwa mechi nyingine mbele. Katika mechi nyingine, Chelsea itakumbana na QPR katika mechi yenye mvuto wa kiushindani ikishindikizwa na mzozo wa beki wa Chelsea, John Terry kumbagua kwa asili mchezaji wa QPR Anton Ferdinand.
|