Harmonize na mabinti damdam!

Mwanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Harvad, Keith Simonton aligundua moja ya kanuni muhimu katika maisha aliyoipa jina la ‘The rule of equal odds’, linalosema chapisho lolote analotoa mwanasayansi lina uwezekanao wa kufanikiwa sawa na chapisho la mwanasayansi mwingine.

Kanuni hiyo ya Keith Simonton, inaaminika msanii yeyote wa kike atakayemshirikisha Harmonize katika wimbo wake kuna uwezekano kwa wimbo huo, kufanya vizuri sawa sawa na endapo angemshirikisha msanii mwingine. Hiyo imesababisha Harmonize kufanya kazi nyingi na wasanii wa kike Bongo, kwa kipindi cha miaka mwili iliyopita. Hawa ni miongoni mwao;

Queen Darleen

Ndiye First Lady wa WCB Wasafi, alisainiwa mwaka 2017 baada ya Harmonize, Rayvanny na Rich Mavoko, hii ilikuwa ni lebo ya pili kusaini baada ya G Records alipofanya na wasanii kama Alikiba. Juni 2019 alimshirikisha Harmonize katika wimbo uitwao ‘Mbali’ uliofanya vizuri, hadi sasa video yake imefikisha watazamaji zaidi ya milioni 8.9 katika mtandao wa YouTube.

Nandy

Juni 2020 Nandy alimpa shavu Harmonize katika wimbo wake ‘Acha Lizame’ uliofanya vizuri, ni moja ya kolabo za mwanzo kubwa kwa Harmonize baada ya kutoka WCB Wasafi.

Maua Sama

Maua Sama alimshirikisha Harmonize katika wimbo wake, ‘Niteke Remix’ uliotoka Julai 2020 na kufanya vizuri.

Anjella
Wimbo wa kwanza wa Anjella tangu ajiunge na Konde ‘Kama’ ulioachiwa Aprili 11, 2021 ndio wa kwanza kumshirikisha Harmonize, hata hivyo, kabla ya kutambulishwa Konde Music tayari Harmonize alimshirikisha Anjella kwenye wimbo ‘All Night’ uliotoka Februari 16, 2021. Baadaye Harmonize akamshirikisha tena kwenye ngoma ‘What Do You Miss’ toka kwenye albamu yake ya pili, High School iliyotoka Novemba 5, 2021.

Abigail Chams
Abigail Chams ameachia ngoma ‘Closer’ inayofanya vizuri sasa akimshirikisha Harmonize.