Diamond aitolea uvivu Ziiki Media

Muktasari:

  • Hata hivyo, Diamond amedai kuwa tangu waikatalie kampuni hiyo kununua hisa za umiliki wa lebo ya Wasafi, Ziiki imekuwa ikiwavuruga kwenye utoaji wa nyimbo na kujaribu kuwaua kimuziki wasanii wa Wasafi.

Kwa mara nyingine tena Kampuni ya Usambazaji Muziki ya Ziiki Media, inaingia kwenye mgogoro na msanii wa Bongo Fleva, Diamond ambaye ametoa tuhuma dhidi yao akidai kuwa kampuni hiyo imezuia wimbo wa Lavalava 'Kibango' kutolewa siku ya leo.

"Ni masikitiko kuona kampuni ya Ziiki inauzuia wimbo wa Lavalava Kibango, kutoka siku ya leo na kulazimisha kutoa tarehe wanayotaka wao tena mwezi ujao pasipo sababu ya msingi". Ameandika Diamond kupitia ukurasa wake wa Instagram

Hata hivyo, Diamond amedai kuwa tangu waikatalie kampuni hiyo kununua hisa za umiliki wa lebo ya Wasafi, Ziiki imekuwa ikiwavuruga kwenye utoaji wa nyimbo na kujaribu kuwaua kimuziki wasanii wa Wasafi.


Diamond ameendelea na kudai kuwa kampuni hiyo imewaonya Wasafi kuwa endapo wimbo huo wa Lavalava utatoka leo utashushwa na kuhakikisha watu hawaupati popote.


"Ziiki wameahidi kwamba endapo leo tutapandisha wimbo wa Lavalava Kibango wataushusha kila platform na kuhakikisha watu hawaupati popote," ameandika Diamond.


Aidha Diamond amesema imefanya waone kuwa Ziiki wanachuki na wasanii wa lebo ya WCB, hivyo imewalazimu kushughulikia jambo hilo kisheria.


Mbali na malalamiko hayo Diamond amewatoa hofu mashabiki wa muziki kwa kueleza kuwa wimbo huo wa Lavalava ambao yeye ameshirikishwa utatoka leo.


"Msijali mashabiki zetu Kibango Lavalava x Diamondplatnumz tunaitoa leo na wakiitoa kwa platforms tutawasambazia hata kwa WhatsApp ombi langu support kubwa ili wajue kuwa mashabiki wanataka ngoma sio propaganda waachie ngoma zitoke,"ameandika.


Utakumbuka kuwa kuliwahi kuzuka tetesi zikidai Diamond ni mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo ya usambazaji muziki, hata hivyo tetesi hizo zilikanushwa Septemba 2023 na Meneja wa kampuni hiyo, Camilla Owora kwa kutolea ufafanuzi wa kukanusha uvumi huo na kueleza kuwa Diamond siyo mmiliki, siyo mwekezaji wala hana hisa zozote Ziiki Media.


Mbali na Diamond, mwaka 2023, Harmonize pia amewahi kuwatuhumu Ziiki kutomlipa pesa zake jambo lililopelekea aombe msaada wa kupata haki serikalini na Agosti 2022 mwanamuziki Vanessa Mdee kupitia ukurasa wake wa Instagram aliitolea uvivu Ziiki kwa kutaka alipwe pesa zake.


Vanessa alieleza kuwa amejaribu kutumia njia nzuri kudai pesa hizo lakini imefikia hatua kampuni hiyo kumkalia kimya.


“Tafadhali @mziiki nawaomba mnilipe pesa zangu kwa makubaliano tulionayo. Nimejaribu the professional way na team yangu sasa imefikia hatua ya nyie kutokujibu, aliandika Vanessa Mdee.