Duma afichua sababu ya waigizaji kupotea

Muktasari:

  • "Wasanii wengi wanakuja kwenye sanaa bila ya ‘misheni’ na hawajui jinsi gani ya kufanya majina yao yaendelee kuwepo, hawako tayari kujitoa mhanga maisha  kwa ajili ya sanaa, hakuna kazi ngumu kama kulifanya jina liendelee kutajwa"

Mwigizaji Daud Michael maarufu kama Duma Actor, amesema kati ya sababu inayosababisha baadhi ya wasanii wapya kwenye soko la sanaa ya maigizo kutambulika kwa muda mfupi kisha kupotea kwenye ramani ni kutokuwa tayari kujitoa kwa ajili ya kazi hiyo.

"Wasanii wengi wanakuja kwenye sanaa bila ya ‘misheni’ na hawajui jinsi gani ya kufanya majina yao yaendelee kuwepo, hawako tayari kujitoa mhanga maisha  kwa ajili ya sanaa, hakuna kazi ngumu kama kulifanya jina liendelee kutajwa, wengi hawajajitoa kwa ajili ya sanaa wanataka sanaa ijitoe kwa ajili yao, ndiyo maana wanapote," anasema Duma

Msanii huyo anasema kati ya kitu ambacho hakiamini katika mafanikio ni uongo,  huku akiongezea kuwa mafanikio yanayotafutwa kwa njia hiyo huwa hayadumu bali ya mtu mkweli ndiyo hudumu.

Licha ya kuendelea kutoa kazi mbalimbali za filamu anasema amewahi kukutana na changamoto mbalimbali lakini bado hazikumkatisha tamaa.

"Mwaka 2020, nilipata matatizo makubwa ikafika hatua nikasema hiki ni nini? nikataka kuacha sanaa kwa sababu yenyewe ndiyo ilifanya nipate matatizo, nilifunguliwa kesi na TCRA laini yangu ikapigwa faini milioni 7, lakini kwa kuwa naamini Mungu anaendelea kunilinda kila siku, ndiyo maana nipo hapa," anasema Duma.

Ikumbukwe kuwa mkali huyu alianza harakati za kujitafuta mwaka 2007 akiwa kwenye Kundi la Bahari Artist Group, hadi sasa amefanya filamu mbalimbali zikiwemo Nipe Changu na Kichomi.