Miaka 11 bila Bi Kidude

“Yalaiti napenda pasi kifani tofauti sikutilii moyoni sikuachi leo na kesho peponi…” ni sehemu ya mashairi yaliyopo kwenye wimbo uitwao Yalaiti, wa Fatma Binti Baraka ‘Bi Kidude’.

Hivi sasa yapata miaka 11 tangu nafsi ya msanii huyu mkongwe wa Zanzibar ifikwe na umauti. Utakumbuka alifariki dunia Jumatano Aprili 17 2013, saa sita mchana. Kifo chake kiliacha pigo kubwa kwa wapenzi wa muziki wa Taarab na unyago.

Bi Kidude alifariki akiwa na umri wa miaka 103 na kuzikwa katika Kijiji cha Kitumba, kilichopo Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.


Matukio kabla ya kifo chake

Kati ya tukio la msanii huyu ambalo hukumbukwa ni lile la 2012 kabla ya umauti wake baada ya Baraza la Sanaa Zanzibar kupiga marufuku kwa promota au muandaaji wa tamasha lolote kumsimamisha Bi Kidude jukwaani kutokana na afya yake.

Lakini mapenzi yake kwenye muziki yalijidhihirisha baada ya kukaidi kauli na kuonekana jukwaani akisalimia mashabiki wake kwenye tamasha la Sauti za Busara.

Hata hivyo, baada ya kusalimia alianza kuimba nyimbo kwa lugha ya Kiarabu na zile za unyago ambazo inasemekana yeye ndiye alikuwa akizitumia kuwafundisha mabinti wanaojiandaa kuolewa.

Bi Kidude alikuwa gwiji katika muziki wa mwambao, alitunga, kuimba na kushiriki nyimbo nyingi akiwa na kikundi cha Culture Musical Club cha Zanzibar pamoja na vikundi mbalimbali.

Kati ya nyimbo zake maarufu ni Muhogo wa Jang’ombe ambao baadaye aliimba Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Msondo, Ahmada na Off Side Trick, Kijiti, Uzuri wa Mwanaume si sura na Alaminadura.

Iliwahi kuelezwa kuwa katika enzi za uhai wake, alionana na Malkia Elizabeth nyumbani kwake nchini Uingereza.


Sababu za kuitwa Bi. Kidude

Jina Kidude lilitokana na yeye kuzaliwa ‘njiti’, ambapo jina hilo lilipata umaarufu zaidi kuliko jina lake halisi la Fatma.


Alipojifunzia muziki

Enzi za uhai wake Bi Kidude aliwahi kueleza kuwa alijifunza muziki kupitia mwanamuziki wa zamani aliyeitwa Sitti binti Saad. Hivyo kutokana na ukaribu uliokuwepo kati yao ikapelekea ajifunze kuimba Taarab.

Kwa kipindi hicho umahiri na umaarufu wa Sitti binti Saad kisiwani Zanzibar, ulisababisha wageni wengi waliofika kisiwani humo kupata shauku ya kutaka kumuona kila wanapotembelea kisiwa hicho kisha Bi Kidude alikuwa akiwapokea na kuwapeleka moja kwa moja kwa Sitti binti Saad.

Mbali na kuimba taarabu, Bi Kidude alikuwa mahiri katika ngoma ya unyago ambayo lengo lake ni kuwafunda wasichana ili kuelewa masuala ya ndoa na kuishi na waume zao vizuri.

Bi Kidude alikuwa maarufu Zanzibar, lakini umaarufu wake ulivuka mipaka baada ya mwaka 1984 alipofanyiwa mahojiano  maalumu katika Televisheni Zanzibar na aliyekuwa Mkurugenzi wa televisheni hiyo, Abdallah Mwinyi Khamis.

Kama watoto wa kawaida alianza kuimba kwa sauti isiyo na mpangilio. Ilipofika mwaka 1920 alianza kuwa kinara wa kuimba na kucheza kwa ustadi ngoma ya unyago.

Bi Kidude alianza kuimba rasmi  alipokuwa na umri wa miaka 10. .


Tuzo alizowahi kutunukiwa

Mwaka 2012 alitunukiwa Tuzo ya ‘Michezo na Sanaa’ na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, na mwaka 2005 huko Gateshead, Newcastle nchini Uingereza, alitwaa tuzo ya heshima kutoka World Music Expo (WOMEX) na kuzawadiwa Euro 5,000.

Pia alipata Tuzo ya Maisha ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999.