Miaka 37 toka kifo cha Ahmad Kipande wa Kilwa Jazz Band

Mwaka  1953, Ahmad Kipande aliyekuwa mzaliwa wa Kilwa, aliamua kuja Dar es Salaam kutafuta maisha. Alipofika kati ya mambo aliyoyakuta yaliyomfurahisha  ni teknolojia ya gramafoni, chombo ambacho kiliweza kupiga santuri na muziki ukasikika.

Miaka hiyo kulikuwa na santuri nyingi za vikundi kutoka Cuba, santuri hizi zilikuwa na majina ya bendi na nyimbo ambazo ziliandikwa Kihipanyiola kama vile
Sexteto Habanero, Trio Matamorosna na kadhalika,  lakini pia zilikuwa na namba zilizoanzia herufi GV, Kiingereza ziliitwa GV series. Kupitia gramafoni Ahmad alianza kuzisikiliza nyimbo za wanamuziki wa Cuba, pia akaanza kusikiliza santuri za wanamuziki wa Afrika ya Mashariki kama akina Fundi Konde. Harry Makacha na Frank Humplink na dada zake. Taratibu akaanza kuwa na hamu ya yeye pia kuwa mwanamuziki.

Kwa msisimko alioupata Kipande akaanza kujifunza mwenyewe vyombo mbalimbali, akajifunza gitaa, ukulele, banjo na violin na hatimaye saxaphone ambayo ndio ilikuja kumpa umaarufu mkubwa baadaye. Ahmad alianza muziki kwa kujiunga katika kundi la Tanganyika Jazz Band. Tanganyika Jazz Band lilikuwa kundi la mtu binafsi na wakati huo muziki ulikuwa ukipigwa kama kitu cha kujiburudisha na kuendeleza fani kwa wanamuziki, haikuwa ajira wala njia ya kupata fedha. Bendi hiyo ilikuwa na  magitaa, violin, ngoma, trumpet na saxophone.

Mwaka 1958, Kipande akamua kuunda  bendi yake, na ndipo wazo la Kilwa Jazz Band lilipozaliwa. Taratibu akaanza kununua vifaa vya kuunda bendi, akanunua saxaphone , magitaa ambayo hayakuwa yakitumia umeme, na kisha kutengeneza ngoma , wakati huo ngoma zilikuwa zikitengezwa kwa kutumia mapipa na ngozi ya ng’ombe au mbuzi.  

Kati ya wanamuziki wa kwanza wa bendi hii alikuweko Zuberi Makata ambaye alifundishwa kupiga sax na Kipande mwenye. Mzee Makata alikuja kufariki kwa ajali ya gari uzeeni. Baadaye bendi ikapata wanamuziki wengine akina Duncan Njilima na Omari Omari. Wakati huo bendi ambazo tayari zilikuwepo katika jiji la Dar es Salaam na zilikuwa zikivuma zilikuwa Homeboys Jazz band, Dar es Salaam Jazz band, na Cuban Marimba Branch, hili lilikuwa tawi la Cuban Marimba ya Morogoro.

Bendi hii ya Cuban Marimba ya marehemu Salum Abdallah ilikuwa na matawi mengi kwa mfano kulikuweko pia Cuban Marimba Branch ya Kilosa.

Kilwa Jazz ilianza muziki ikawa inapiga nyimbo zake kwa mitindo mbalimbali ikiwemo rumba, samba, bolelo  na chacha. Bahati mbaya katika zama hizi mitindo hiii yote imebebeshwa jina moja tu la rhumba.

Kilwa ikaja kuwa moja ya bendi tishio jijini Dar es Salaam. Kati ya nyimbo ambazo bado ni maarufu mpaka leo ni ule wenye maneno haya;

Napenda  nipate lau nafasii,
Nipate kusema nawe kidogo aah mamaa aah
Rohoni  inaumiaa,
Hakika lakufanya bado sijaliona,
Nimeona leo bora nikuimbee,
Huenda punde roho yako ikadundaa

Ikaja siku ukaja nipoza moyo ooh mama rohoni naumia…
Huo ni wimbo wa Kilwa Jazz Band, japo muziki waliuchukua kutoka wimbo wa Mokolo Nakokufa wa bendi ya African Fiesta ya Kongo.

Ahmad Kipande na bendi yake ya Kilwa Jazz ilishiriki katika  mambo mengi makubwa ya kitaifa. Kilwa Jazz Band ilikuwa moja ya vikundi vilivyotumbuiza siku Tanganyika inapata Uhuru Desemba 09, 1961, na iliporomosha wimbo maalumu wa kusifia Tanganyika kupata Uhuru. Wimbo huo ulikuwa na maneno haya;

“Ewe mola tunakuomba,
 Uibariki Tanganyika,
 Uhuru tumeshaupata
Lakini nyoyo zinasikitika,
Wenzetu wanateseka,
 Wakoloni wamewashika…”

Kilwa Jazz Band iliheshimika sana,  ndiyo iliyoteuliwa na serikali kushiriki sherehe za Uhuru wa Malawi na Uganda.

Kama ilivyokuwa kwa wanamuziki wa miaka ile, Ahmad Kipande na wenzie walipenda sana kutunga nyimbo zenye maudhui ya uzalendo kwa nchi yao. Wimbo  wao mmoja ulitokana na maneno aliyoyatamka Mwalimu Nyerere, ulipendwa sana wimbo huo ulikuwa una maneno ya Kiingereza, ‘It can be done , play your part’

Kilwa Jazz band ilikuwa na nyimbo nyingi sana zilizopendwa na zinazoendelea kupendwa,  kati ya hizo ulikuwepo wimbo ulioitwa Kifo cha Penzi, ambao kwa kifupi mtunzi anasema kifo cha penzi ni kitu kibaya usijiombee kifo cha penzi, na katika wimbo huo tunakumbushwa mambo mawili ya kihistoria, mstari mmoja unasema, ‘Heri ufe kwa kugongwa na basi la ghorofa liendalo Ilala’, miaka hiyo kulikuweko na usafiri wa mabasi ya ghorofa yaliyokuwa yakipeleka abiria Ilala. Mstari mwingine unasema ‘Heri ufe kwa kugongwa na gari la terela liendalo Zambia’.

Kabla ya kujengwa kwa bomba la TAZAMA Pipeline, na reli ya TAZARA, mizigo na  mafuta kuelekea Zambia yalikuwa yakipelekwa na malori yenye materela.
Mapenzi yananivunja Mgongo, Kifo cha Pesa, Dolly, Nacheka cheka Kilwa, Enyi vijana tujenge nchi yetu, Rose wauwa ni baadhi ya nyimbo za bendi hii iliyokuwa ni ndoto ya Ahmed Kipande.

Mwaka 1973 Kilwa Jazz Band ilialikwa na kutumbuiza kabla ya onyesho la gwiji la muziki wa dansi, Franco  na bendi yake ya  T.P.O.K. Jazz lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mapenzi ya Mungu, Ahmed Kipande alifariki  dunia Aprili 27, 1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa kipindi kirefu. Kipande ataendelea kukumbukwa kwa mazuri aliyoyaacha katika Taifa hili Mungu Amlaze Pema.