Msiba ulivyompa ajira Dj Ally B

Muktasari:

  • Ni Dj ambaye amejipatia umaarufu kutokana na uchangamfu wake kwenye kazi yake ameanza majukumu hayo tangu mwaka 2002 ambapo amethibitisha kuwa hakuwahi kupenda shule.

Ni mchangamfu, muongeaji si mtu wa kujigamba ila ni mfano wa kuigwa kutokana na namna alivyopambana hadi kufikia alipo sasa licha ya  changamoto alizokutana nazo wakati wa kujitafuta, si mwingine ni DJ Ally Suleiman Simba ‘maarufu kama ‘Ally B’.

Ni Dj ambaye amejipatia umaarufu kutokana na uchangamfu wake kwenye kazi yake ameanza majukumu hayo tangu mwaka 2002 ambapo amethibitisha kuwa hakuwahi kupenda shule.
Mwananchi limepata nafasi ya kuzungumza na staa huyo ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga, ambapo amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwanini aliacha na shule.

                        

Shule mmh kipaji tu

Ally B, anasema amemaliza darasa la saba mwaka 2002, ugumu wa maisha ulimfanya aishie hapo pia kwenye maisha yake hajawahi kuwa na ndoto ya kusoma zaidi ya kupambana kwa kufanya kazi.

“Pamoja na kukataa shule kuna muda kuna baadhi ya vitu ni lazima uvisome kwa sababu ni muhimu kama kuzungumza Kiingereza na lugha nyingine hilo ndilo pekee nililoweza kufanikisha hadi nilipofikia sasa,” anasema na kuongeza;

“Nimesoma lugha tatu tu ambazo nimepata nafasi ya kuingia darasani kwa lengo la kuzisomea ili niweze kufikia malengo,” alisema Dj huyo maarufu. 

Anasema baada ya kukataa shule wazazi wake hawakuwa na kitu chochote cha kumwambia kutokana na kutoka familia ambayo haikuwa vizuri kifedha hivyo aliamua kuchagua njia sahihi ya kutafuta fedha kwa kufanya kazi.

                       

Kutoka konda hadi Dj

Anasema kabla ya kuingia kwenye kazi ya U-Dj alifanya kazi nyingi sana hadi sasa amekuwa maarufu mkubwa kutokana na kazi anayoifanya   ambayo amekiri kuwa imemuheshimisha na inamuingizia kipato kikubwa.

“Nilishawahi kuwa fundi gereji, kuuza chipsi, kukata miwa kiwanda cha sukari TPC, kutengeneza barabara, kuwa kondakta wa daladala hadi dereva hii yote ni kupambana kutafuta maisha,” anasema na kuongeza;

“Pamoja na changamoto zote hizo sijawahi kujuta kuhusu kusoma kipaumbele kilikuwa ni kipaji changu kwa sababu nilikuwa napenda sana kucheza muziki, nikaamini kuwa huko ndiyo ningeweza kutoka, unajua wacheza shoo wengi wanajua sana nyimbo nzuri, hivyo mimi nilikuwa kama sehemu ya kuandaa nyimbo nzuri,” anasema.

                       

Msiba ulivyompa ajira

Dj huyo tajiri Bongo anasema alikuwa na rafiki anaitwa Kassim Mukada ambaye alikuwa DJ, akawa anamtumia kama sehemu ya kumuandalia nyimbo nyingi za kupiga sehemu ya kazi yake na ndiyo ukawa mwanzo wa yeye  kuijua kazi hiyo.

“Mimi najifunza kwa kuangalia, nilikuwa namuona jinsi rafiki yangu alivyokuwa anabadilisha muziki na alikuwa ananitumia nimtafutie  nyimbo nzuri mpya za kupiga na hapo ndiyo safari yangu ilipoanzia kwa sababu nilikuwa na nyimbo nyingi, nakumbuka nilitengeneza hadi kitabu cha nyimbo,” anasema na kuongeza;

“Nilikuwa namdanganya kwamba naweza kazi ya Udj nikimsisitiza kabisa kuwa ukiniachia hiyo mashine nitafanya balaa kumbe sina ninachokiweza zaidi ya kuwa na nyimbo nyingi nzuri, alikuwa anapiga Malindi Bar  Moshi.”

Ally B anasema hadi alipofika hakuna mtu aliyemfundisha kazi hiyo zaidi ya kujifunza kwa kuangalia kwa rafiki yake. Anasema siku moja jamaa huyo alipata msiba akamuomba amuachie kazi ndiyo akaibuka shujaa kwa kufanya vizuri na kupata umaarufu mkubwa.

“Kupiga muziki ni kubadilisha nyimbo kilichonisaidia mimi nilikuwa nacheza muziki ambao upo kwenye chati kipindi hicho mwaka 2015 hivyo watu wengi wakawa wanafurahi, baada ya kurudi nilimuachia kazi yake kwa sababu wazazi walikuwa hawajapenda niifanye kwa kuwa nilikuwa narudi usiku,” anasema na kuongeza;

“Siku mbili baada ya Kassim kurudi na kumuachia kazi yake, boss wake alinipigia simu akinitaka nirudi kazini, nikamhoji narudi vipi wakati mwenye ajira yake yupo, akasema hawamtaki wananitaka mimi, ilikuwa mbaya kwangu nikasema huyo ndiye aliyenileta basi tubaki wote, akakubali tukawa tunafanya wote mshahara ulikuwa 35 elfu tukawa tunagawana 17 kila mmoja.”


Dj Said alivyomleta Dar

“2010 nilikuja Dar es Salaam na kufikia kwa Said ambaye naomba kukiri kuwa nilipitia wakati mgumu na kunifanya nijitume zaidi. Kuna siku nilitoka kazini narudi geto nikakuta kumefungwa, nampigia simu ndugu yangu ananiambia yupo kwa demu wake.

“Nilimsikilizia kuanzia saa nne hadi saa kumi usiku alinipa hasira ya kupambana na kuamini kuwa kila kitu lazima kiwe na mwanzo na mwanzo ukiwa mbaya lazima mwisho wake uwe mbaya.”

“Aliporudi alinikatisha tamaa zaidi aliponiambia  Dar es Salaam siwezi kupata kazi natakiwa kurudi Dodoma, nikamwambia kama hutaki nikae kwako niambie niondoke, akanitimua, nikatoka nakumbuka ilikuwa saa moja nikaenda sehemu inaitwa Manyanya nikiwa nimesimama nilipigwa kibao na kuporwa kila kitu niliumia sana,” anasema.

Dj huyo maarufu Bongo kwa sasa anasema alienda kwa rafiki yake Mandazi Road nyumba ilikuwa na choo kimejaa akawa anakwenda choo cha kulipia lakini anasema changamoto alizozipitia  ndizo zilizomfanya awe Ally B, ambaye ni maarufu sasa na ana mshukuru Said kwa kumfukuza kwani alimsaidia.

Ally B, anasema rafiki yake huyo ambaye alimfukuza kipindi hicho, alishawahi kumkaribisha kwake baada ya kufanikiwa na alimuona akiwa anakasirika kutokana na mafanikio yake, akamwambia hii yote ni kwasababu alichomfanyia kilimpa hasira ya maisha na anamshukuru sana.


Kipaji siyo kitu

Anasema kuna vipaji vingi lakini pia kuna watu wanaojituma sana hivyo anaamini wanaopambana ndiyo wenye faida kubwa tofauti na wale wanaoringia vipaji vyao.

“Tanzania imejaliwa vipaji vikubwa na vingi kama muziki, soka na vitu vingine vingi lakini wanashindwa kujiuza wakiamini vipaji yao vitawapa kila kitu lakini kuna mtu hana kipaji ni mpambanaji anajiuza mwenyewe kutokana na namna anavyojituma.

“Mimi naamini katika kupambana na ndiyo maana nimefika hapa nilipo, napambana sana nimepitia mengi nimepanda na kushuka hii yote ni kuhakikisha nakiuza kipaji changu kinachoonekana sasa kila mmoja anamfahamu Ally B ni juhudi zangu wala siyo kipaji” anasema.


Kutoka elfu 35 hadi 2milioni

Anasema alianza kazi akiwa Arusha ambayo kwa mwezi alikuwa analipwa  shilingi 35 elfu  ambayo walikuwa wanagawana wawili kwa mwezi,  elfu 17 kila mmoja lakini baada ya kuja Dar es Salaam maisha yalibadilika na kumfanya aifurahie zaidi kazi hiyo anayoifanya.

“Nafanya kazi yangu saa moja na nusu na naweza kufanya kazi tatu hadi nne kwa siku na inategemeana na makubaliano na mtu aliyenipa kazi lakini ni kuanzia Sh 2 milioni hadi Sh 4 milioni kwa hiyo saa moja na nusu,” anasema na kuongeza;

“Namshukuru sana Mungu kwa hatua hii niliyofikia sasa nilikuwa naitamani sana na nimepiga goti kumuomba sasa nimefikia kile nilichokuwa nakitamani.
 

“Kwa hapa Dar es Salaam naweza nikapiga shoo 4 hadi 5 kwa siku, ukiangalia mkwanja ni mkubwa naupata, hii kazi inalipa,” anasema.

Hana mpango wa kujenga

“Mpango wa kujenga nyumba ya kuishi sina, nisiwe mnafiki fedha yangu nyingi ni kula bata kwa sababu maisha yenyewe ni mafupi hapa duniani, nitapanga hadi siku ya mwisho.

“Ni kweli nina familia lakini wanangu nimewajengea nyumba ambazo nimezipangisha, hizo ndiyo   zitawasaidia kwenye maisha yao ya baadaye lakini kwangu mimi sina mpango wowote wa kujenga nyumba yangu ya kuishi.”

Ally B anasema walio na nyumba mjini watanufaika sana kupitia yeye kwa sababu anataka kufurahia maisha yake na siyo kitu kingine.

Ukimuita mtarajie tena

Amethibitisha kuwa akipata nafasi ya kuitwa sehemu yoyote kufanya kazi yake ya U-Dj basi wanatakiwa kumtarajia kumuona tena na tena hii ni kutokana na kufanya kazi kwa ubora zaidi ili kukidhi kiwango anachopewa.

“Nikienda kwenye shoo ni lazima niitwe tena na tena, kwa sababu nafanya kazi kwa usahihi napewa hela ya kutosha natakiwa kufanya kwa ukubwa.

“Hii kazi yangu ni sawa na wasanii ambao wamekuwa wakiandaa matamasha na baadaye kujikuta wanalalamikiwa na mashabiki waliojitoa kuwapa sapoti kwa kutoa fedha za viingilio na kukutana na vitu ambavyo hawakutarajia, hata mimi
nimeshawahi kulalamikiwa, hivyo nimeiva, nafanya kitu kwa usahihi hali inayonifanya nipate madili mengi,” anasema.


Sababu vijana wengi kufeli

Anasema anazungumza kitu ambacho ameshawahi kukutana nacho na ndicho kilichompa mwanga wa kuingia kwenye mafanikio baada ya kutokuwa na heshima na kitu ambacho alikuwa anakifanya alijikuta anaishia kukwama kila anapotaka kujaribu kufikia mafanikio.

“Vijana wengi wanashindwa kufikia malengo kwa sababu ya kukosa nidhamu ya kazi kutambua nini kinaweza kuwatoa walipo na kwenda hatua nyingine kitu ambacho mimi nilikisoma kwangu nimechelewa kupata mafanikio kwa sababu ya nidhamu ya kazi.
“Nilipojisoma nikajipata nikagundua mimi nakosea hapa natakiwa kujirekebisha ili niweze kusonga hatua moja hadi nyingine.

“Naomba kuthibitisha kuwa kila mmoja ambaye amepata fursa ya kipaji au kujiajiri kwa chochote fedha ipo nyingi sana,” anasema.

Ally B anasema kuna watu wanavipaji vikubwa lakini wanashindwa kupata nafasi ya kufanya kazi kwa sababu wanajifanya wanaweza kila kitu.