Mwasiti ajitoa muhanga kuwaepusha wasanii na rushwa ya ngono

Muktasari:

  • Mwasiti mwenye lengo la kuwaepusha mabinti hao na vishawishi vya ngono, amejizolea umaarufu kupitia nyimbo za ‘Nalivua pendo’, ‘Sio kisa pombe’, ‘Serebuka’ na ‘Kaa nao.’ 

Wakati baadhi ya wasanii wa kike wakidai kukutana na changamoto za rushwa ya ngono katika harakati za kujitafuta kimuziki, mwanamuziki wa Bongo Fleva, Mwasiti Almas ameamua kuwavuta mabinti wenye vipaji kwa ajili ya kuwasaidia kupitia taasisi yake ya Kipepeo Mweusi.

Mwasiti mwenye lengo la kuwaepusha mabinti hao na vishawishi vya ngono, amejizolea umaarufu kupitia nyimbo za ‘Nalivua pendo’, ‘Sio kisa pombe’, ‘Serebuka’ na ‘Kaa nao.’ 

Akizungumza na Mwananchi Mwasiti amesema Kipepeo Mweusi haijalenga watoto wa shule bali mabinti wanaojitafuta kimuziki.

“Kipepeo Mweusi ni binti ambaye ana miaka 16 mpaka 30,  yupo kwenye sanaa kijumla, nia kubwa ya kutengeneza kitu kinachoitwa Kipepeo Mweusi ni kusaidia kutoa elimu ya kuwafanya wasogee zaidi kwenye soko letu la muziki, wasanii wa kike ni wachache sana tunataka waongezeke.

"Lakini, chini wanakutana na vitu vinavyowakatisha tamaa, wengine tuliweza ndiyo maana tupo hadi leo; wengine walikutana navyo wakashindwa kupenya, kwa hiyo sisi tunaangalia vitu vingi tunajaribu sana kumsaidia binti aweze kupenya na kufikia kwenye ndoto yake kubwa,”amesema.

“Wakati niko mchanga kwenye muziki kuna vitu nilipitia, kwa njia moja ama nyingine viliniyumbisha, nikasema kuna watu watafurahi nikiyumba nikasema hapana siwezi kuwapa nafasi; na hadi nasema Kipepeo Mweusi ni msichana wa aina hiyo ni kwa sababu kuna vitu hata mimi vilinigusa kwa namna moja ama nyingine.” 

Suala la wasanii kupitia changamoto za kusumbuliwa kingono linaonekana kuwa ndiyo chanzo kikubwa cha wasanii wa kike kutokuwa wengi kwenye gemu ya muziki nchini lakini pia hata wachache wanaopata nafasi wamekuwa hawadumu kwa muda mrefu sokoni.

Lakini kupitia Kipepeo Mweusi, Mwasiti ameweza kukusanya takribani wasichana 200 kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya kuwapatia mafunzo, huku nia yake kubwa ikiwa ni kufikia mabinti wengi zaidi.

Mwasiti amedai kuwa mabinti wengi wanaonekana kupenda umaarufu, hivyo wakiwa wanajitafuta kimuziki hujikuta wakipewa ujauzito na kutelekezwa.

Amesema wakati mwingine hupatiwa magonjwa, hivyo timu ya Kipepeo Mweusi imejipanga kuwasaidia wasichana hao wenye vipaji kwa ajili ya kufanikiwa bila ya kutoa rushwa ya ngono.
Pamoja na kusema hayo Mwasiti ametoa ushauri kwa mabinti wanaojitafuta kwenye soko la muziki nchini.

“Wito wangu mabinti wasijikatie tamaa kwa sababu hivi vitu vinaongeleka, mwili wako siyo malipo, hutakiwi kulala na producer ili aweze kukusaidia kimuziki wewe mwenyewe jizatiti kwanza unaweza kufanya unachokifanya.”