Rose Ndauka mwanadada mwenye kofia tatu za heshimu

Naweza kumlinganisha mwanadada Rose Ndauka na jiwe moja linalopiga ndege watatu, hii ni kutokana na mwigizaji huyu kuzama katika tasnia tatu tofauti kwa ajili ya kujipatia kipato. Utakumbuka Rose alijipatia umaarufu mwaka 2007 baada ya kufanya filamu iliyoitwa ‘Swahiba’ akiwa na Jacob Stephen ‘JB’ na Single Mtambalike ‘Rich’.

Awali mashabiki walimkubali kutokana na uigizaji wake, kisha Aprili 8, 2021 akatangaza rasmi kuingia kwenye muziki wa hip-hop na kutambulisha ngoma yake ya kwanza iliyoenda kwa jina la ‘Sijali’ ambayo hadi sasa ina wasikilizaji 71k na watazamaji 246k (YouTube).

Mbali na kuonyesha vipaji vyake hivyo viwili Rose aliendelea kuwashangaza mashabiki kwa kuwaonyesha uwezo wake mwingine kwenye upande wa ushereheshaji (MC), ambapo kwa mara ya kwanza  Februari 11, 2024 kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha video yake akisherehesha na kuandika ujumbe unaohusu kufanya kazi hiyo.

“Allhamdulilah kwa mara ya kwanza ni kazi yangu ya kwanza, namshukuru Mungu wangu muumba lakini pia namshukuru sana mume wangu kwa kuniaminisha naweza.

“Bila kusahau mabosi zangu walioniamini bila kujua uwezo wangu na kunipa kazi ya kusimamia shughuli yao, new MC in town mimi sasa huyo”. Aliandika Rose.

Kutokana na hayo, ameliambia gazeti hili kuwa  amezaliwa kwenye familia yenye watu wenye vipaji tofauti tofauti ndiyo maana hata yeye amekuwa akionyesha uwezo wake kwenye vitu mbalimbali.

“Mimi nimezaliwa kwenye familia ya watu wenye vipaji, tumekuwa tukifanya vitu tofauti tofauti, nimekuwa nikitamani kazi ya ushereheshaji, aliyokuwa anafanya baba yangu mdogo ambaye ni marehemu sasa hivi, lakini pia kaka zangu wanafanya kwa hiyo nikaona kwa nini na mimi nisifanye. Mtu wa kwanza kumfanyia kazi aliniomba,” anasema.

Rose anasema siku ya kwanza kufanya kazi ya ushereheshaji aligundua kuwa kazi hiyo siyo nyepesi na siyo ngumu kutokana na changamoto alizokutana nazo kama vile kuishiwa maneno.

“Niwe muwazi siku ya kwanza siyo maneno tu hadi mapozi yaliniisha, kiukweli ilifika muda kwa sababu muvumenti ni nyingi na makelele unakuta unataka kuongea hivi watu wengine wanapiga makelele kiukweli siyo kitu kirahisi na siyo kitu kigumu pia,” anasema Rose.

Kutokana na changamoto na nguvu ambayo inahitajika kwenye ushereheshaji msanii huyu ameeleza kuwa bei zake zinaanzia Sh2 milioni hadi Sh5 milioni kulingana na wingi wa watu waliopo kwenye sherehe husika. Huku akitaja Sh2.5 milioni kama kiasi kikubwa cha fedha ambacho amewahi kulipwa tangu aanze kazi hiyo.

Ule msemo wa mshika mawili moja humponyoka kwa Rose unaweza ukawa hauna maana, kwani anadai kuwa mashabiki wake wategemee kumuona popote kwa sababu yeye ni mpambanaji kwa hiyo popote atakapoitiwa pesa ataenda kuifanya ili mradi kisiwe kitu haramu.

Utakumbuka kuwa kazi ya ushereheshaji na uimbaji Rose Ndauka ameanza kufanya akiwa ndani ya ndoa, ambayo amefunga na mumewe Haffiy Mkongwa, Aprili 2020.
Hivyo basi kutokana na mafanikio hayo ambayo ameendelea kuyapata akiwa ndani ya ndoa, amesema ili wanandoa waweze kushirikiana na kufanikisha malengo yao ni muhimu kuhakikisha wanakuwa marafiki kwanza.

“Mwanamke hakikisha unaolewa na rafiki yako ambaye anatamani kuona unafanikiwa zaidi ya pale ambapo alikukuta, mimi nafanikiwa kufanya vyote kwa sababu mume wangu anatamani kuniona mbali zaidi ya hapa nilipo.

Kwa hiyo inakuwa ni rahisi kunisapoti kila sehemu ninayokanyaga kama nilivyosema ili mradi tusimkosee Mungu kwa hiyo inakuwa rahisi sidhani kama kuolewa unakuwa umekatisha ndoto zako au unashindwa kupambana na kufanya vitu vingine, ndoa isiwe sababu ya kukukatisha tamaa,” anasema

Hata hivyo, ngoma ya mwisho ya msanii huyu ilitoka miezi minne iliyopita ikienda kwa jina la ‘Rapper Mama’. Rose anasema kwa sasa hajafikiria kuachia kazi nyingine japo kuwa zipo ambazo tayari zimekamilika.

Huku kwa upande wa filamu amesema kuna kazi nyingi ambazo anaziandaa zitakapokuwa tayari mashabiki watazipata.


Kiki na kupati siyo vitu vyake

Licha ya kuwa baadhi ya watu maarufu wamekuwa wakiamini kiki ndiyo msingi wa kusukuma kazi zao na kuwafanya wasipotee kwenye gemu, msanii huyu anasema kwa upande wake haamini katika kiki.

“Kiukweli kwanza namshukuru mama yangu kwa malezi na miongozo aliyonipa lakini kikubwa naweza kutofautisha kati ya kazi na vitu vingine ukiweza kutofautisha kazi na maisha binafsi vitakufanya uepukane na vitu vingi sana kwa sababu mimi nimetambulishwa na kazi zangu kwa hiyo napenda niendelee kutambulishwa kwa kazi zangu na siyo mambo ya kiki.

Kiukweli kiki ni vitu ambavyo sijafokasi navyo na sijawahi kutamani kuvifikisha kwenye jamii kwa sababu naamini jamii inatamani kuona zaidi kazi zangu kuliko mambo ya kiki,” anasema.

Mbali na hilo msanii huyu ameeleza kinachofanya awe tofauti na watu maarufu wengine, hasa kwenye suala la kuonekana kwenye sherehe mbalimbali.

“Mimi nadhani eventi zinahusisha zaidi watu wako wa karibu, sasa mimi unakuta siyo watu wangu wa karibu na ndiyo maana sitokei lakini wakiwa watu wangu wataniona,” anasema Rose.


Kusimamia wasanii

Imekuwa kawaida kwa baadhi ya wasanii kushusha lawama kwa watu ambao wanawasimamia mara baada ya kuacha kufanya nao kazi, na kwa upande mwingine wasimamizi wamekuwa wakitoa lawama kwa wasanii kuwa wakipata majina huanza dharau na hili pia mwigizaji huyu ambaye aliwahi kusimamia msanii amelizungumzia.

“Nimewahi kufanya kazi ya kusimamia msanii lakini kwa sasa sijioni huko biashara inanikaba kwa kweli, usikivu wa watu wanaosimamiwa wanapokea maneno ya pembeni ambayo siyo mazuri.

Rose ambaye alikuwa akisimamia msanii wa muziki  aitwaye Casso, mwaka 2015 chini ya lebo yake iliyoitwa  ‘Ndauka Music’ amesema inahitaji hekima na busara kwa msanii anapotoka kwenye usimamizi.

“Mimi ushauri wangu ni kwamba inahitaji hekima kwa sababu kumsimamia mtu ni kama biashara unakuwa unawekeza, nashauri wanaosimamiwa wakati wa  kuondoka wawe wanatumia hekima na busara.

“Kwa sababu mwanzo ulikuwa haujulikani lakini anayejitolea kukusimamia anakuwa anajitoa ili ufahamike hata kama atakuwa amekosea wewe unayekuwa umesimamiwa uondoke kwa hekima na busara,” amemalizia.