Hivi hapa vikwazo, fursa ubanguaji wa korosho

Tanzania ina malengo makubwa ya kukuza tija katika zao la korosho, miongoni mwa mipango yake ni kuzalisha na kubangua tani milioni moja ifikapo mwaka 2030.

Kuelekea malengo hayo, Tanzania imepanga kubangua tani laki saba kufikia mwaka 2026, hata hivyo malengo yote hayo mawili yanahitaji juhudi za makusudi ili kuyafikia.

Kwa sasa wastani wa uzalishaji wa korosho ni tani 300,000, huku ubanguaji ukiwa ni asilimia chini ya 20.

Katika mahojiano yake na Mwananchi, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho (CBT) Francis Alfred alieleza mipango ya Serikali ya kuhakikisha mipango hiyo inatimia kwa kipindi hicho kifupi kilichobaki na mustakabali mzuri wa zao hilo muhimu kiuchumi.

“Wanunuzi wakubwa wa korosho ghafi ni India na Vietnam kwa sababu nchi hizo mbili zinabangua zaidi ya asilimia 90 ya korosho zote ulimwenguni. Sisi kwetu changamoto kubwa ya ubanguaji ni upatikanaji wa malighafi, wa ndani wana changamoto ya ushindani katika minada,” alisema Alfred.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kukosekana kwa mitaji ya uhakika na ya gharama nafuu, kwani mbanguaji ili ubangue tani 2,500 lazima uwe na walau Sh5 bilioni, kiasi ambacho wengi hawana.

“Tunahitaji kuwa na soko pana, korosho ghafi ni soko finyu, tukifanya ubanguaji tunalitanua, hivi sasa hatuwezi kuuza Marekani wala Uingereza kwa kuwa hamna viwanda vya kubangua lakini walaji wakubwa,” anasema.

Akisisitiza umuhimu wa kuweka nguvu katika ubanguaji wa ndani, Alfred anadokeza kuwa nchi ya Cambodia hivi sasa imeweka nguvu kubwa katika kilimo cha korosho na nchi hiyo ni jirani na wanunuzi wakubwa, hivyo kwa siku zijazo wanaweza kuacha kununua kwetu kwa sababu ya umbali.

“Tukibangua tunakuwa na soko endelevu, tukitegemea soko ghafi linakuwa finyu, wanaonunua sasa kwetu wakipata malighafi za karibu hawatanunua tena huku,” alisema Alfred, huku akizitaja nchi za India na Vietnam kama wanunuzi wakubwa wa korosho ghafi.

Mwenyekiti wa Shirikisho la wabanguaji wa korosho nchini (TACP), Bahati Mayoma anasema wao wanaunga mkono kwa vitendo nia ya Serikali ya kuhakikisha korosho yote inabanguliwa hapa nchini.

Hata hivyo, anasema ili waweze kufanikisha hilo ni muhimu kulilinda na kuliimarisha soko la awali, kwani uwepo wake ndio umeleta uwekezaji mwingi katika ubanguaji, tofauti na ilivyokuwa kabla ya mwaka 2021.

“Baada ya muda mrefu, 2021 Serikali iliridhia kuanzishwa kwa soko la awali, jambo ambalo lilikuwa linatunyima ushindani, baada ya hapo viwanda vingi vikaanza kujengwa. Changamoto kubwa iliyokuwepo ilikuwa ni upatikanaji wa malighafi, tulikuwa tunashindwa kushindana na wanunuzi wa nje kwa kuwa wao wanapata mikopo watokako kwa asilimia ndogo,” anasema.

Anaongeza kuwa soko la awali liliibua fursa nyingi: “Lilifuta kangomba ambao hawalipi kodi, sisi hatununui bei ya chini, mara nyingi haipishani na mnadani na kama ingekuwa ni kweli hilo wangekuwa wanauza mnadani.”

Mayoma anaongeza kuwa ukiachilia mbali changamoto ya malighafi, wabanguaji nchini wanakabiliwa na changamoto ya mtaji kwa kuwa wanakopa kwa riba kubwa ya asilimia 10 hadi 16 kulingana na kiwango huku wabanguaji katika mataifa mengine wakipewa nafuu maalumu ya mitaji.

“Wenzetu wanapata mkopo kwa asilimia tatu hadi tano, tungetamani kuwe na mfuko maalumu wa wabanguaji ili tupate kwa nafuu, pengine tungekuwa mbali zaidi katika ubanguaji,” anasema kiongozi huyo wa TACP, ambayo ina wanachama zaidi ya 25.

Meneja uzalishaji wa kiwanda cha Organic Growth kilichopo Tandahimba, Aldina Fakir Production yeye anasema wabanguaji wa ndani changamoto yao kubwa ni mtaji na upatikanaji wa malighafi.

“Tuna fursa ya kununua kupitia soko la awali, ‘organic’ inaanzia shambani, nikitumia soko la awali naweza kupata hiyo, sasa ipo katika ushindani, soko la awali liimarishwe zaidi au kama ni kwenda mnadani sisi wa ndani tutengewe fungu fulani,” anasema Fakir.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda cha Prosperity Agro, Haroun Maarifa naye anasisitiza umuhimu wa kuwajengea wabanguaji wa ndani uwezo wa kifedha ili kufikia malengo hayo, akisema gharama za kuendesha kiwanda cha kabangua korosho ni kikubwa kuliko cha kuanzisha.

“Ili nizalishe tani 6,000 nahitaji kuwa na bilioni 16 mbali na malipo ya wafanyakazi na gharama nyingine za uendeshaji. Gharama za uendeshaji kwetu ni kubwa kuliko hata kuanzisha kiwanda chenyewe,” anasema.

Anasema ombi la wabanguaji kwa Serikali ni kusaidiwa kupitia vyama vya ushirika, Serikali idhamini malipo ya wakulima, kisha iweke kituo kimoja ambacho kila mbanguaji anaweza kuchukua.

“Ni muhimu kuwajengea uwezo wa kifedha kununua malighafi zinazowatosha kulingana na uwezo wao, tuliomba kuwe na motisha kama mfuko maalumu wa maendeleo ya ubanguaji wa korosho. Kila mtu kulingana na uwezo wake wa kubangua anapewa fedha fulani au mfuko ule utumike kama dhamana, lakini sasa tunalazimika kujidhamini wenyewe.

“Tuliwafikia BoT (Benki kuu ya Tanzania) wakasema watatushika mkono katika shughuli zetu kwa kuwa zinaleta fedha za kigeni, lakini wakasema watafanya hivyo kupitia benki za kiashara, jambo ambalo linaleta ugumu kidogo katika eneo hilo.”

Anasema Serikali ikifanyia kazi mapendekezo yao ambayo wamekuwa wakiyatoa, lengo kubwa lililopo katika sekta hiyo litafikiwa na Watanzania wanaotegemea mnyororo wa thamani wa korosho watahakikishia ajira na kipato sanjari na kuongeza fedha za kigeni.

Akizungumzia ubanguaji wa ndani na manufaa yake kwa jamii zinazolima korosho, anasema maisha yao yamefungamanishwa na korosho, ndiyo maana watu zaidi ya laki 3.5 katika mikoa hiyo wanajihusisha na kilimo cha korosho kwa kurithi au kuchangamkia fursa.

“Ubanguaji wa ndani unachokifanya ni kuimarisha upatikanaji wa ajira. Katika mwaka mzima korosho inavunwa miezi minne tu kuanzia mwezi wa 10, baada ya mavuno wengi wanakuwa hawana kazi nyingine, ubanguaji unawapa kazi kwa kipindi kirefu mwaka mzima,” anasema Maarifa.

Kutokana na umuhimu huo, Maarifa anasisitiza Serikali kutoa motisha kwa wabanguaji hao na kufanyia kazi mapendekezo yao mbalimbali, hata kama ni kwa kuwekeana masharti ya ufanisi “performance based incentives.”

Miongoni mwa wabanguaji wa ndani wa korosho ni Maria Verschoof Co-founder ambaye anamiliki kiwanda cha Mama Cashew, alisema kwa sehemu kubwa uendelevu wa biashara yake utatokana na uwepo wa soko la awali.

“Tulianza shughuli zetu kutokana na uwepo wa soko la awali, tulikuwa tukiuangalia uwekezaji huo miaka ya nyuma lakini hatukuvutiwa nao hadi pale utaratibu wa soko la awali ulipoanza,” alisema Verschoof, mwekezaji kutoka Uholanzi.

Mwekezaji huyo alisema korosho yake anauza soko la Ulaya na kama mwenendo wa biashara utakuwa mzuri anatarajia kupanua uwekezaji wake kwa kuongeza kiwanda kingeni cha kubangua chenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5 (Sh12.5 bilioni).

“Hata hivyo, mipango yangu yote itategemea uwepo wa soko la awali, hata kiwanda nilichonacho sasa soko la awali likisitishwa nami nitafunga biashara,” anasema Verschoof ambaye ametoa ajira kwa zaidi ya watu 500, asilimia 90 wakiwa ni wanawake.

Akijibu hoja za wabanguaji, Alfred anasema wana mipango ya kuhamasisha uwekezaji wa viwanda nchini ili kufikia malengo yaliyopo na kama kuna changamoto ambazo zipo wataendelea kuzitafutia ufumbuzi na kurekebisha maeneo yote ambayo mambo hayaendi sawa.

“Soko la awali ni miongoni mwa vivutio na hilo hatufanyi sisi tu, Msumbiji hawaruhusu mnunuzi wa nje kabla viwanda vya ndani havijashiba. Ivory Coast ndiyo inayoongoza kwa ubanguaji, hamna usimamizi wowote madhubuti isipokuwa mbanguaji anaruhusiwa kununua moja kwa moja kwa mkulima,” anasema.

Anasema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine lazima kuwa na sera za kuvutia ubanguaji ili waendelee kuja, kwani kwenye kubangua ndiyo kuna maslahi endelevu kwa wakulima, ikizingatiwa kuwa korosho ghafi imekuwa haina mwenendo mzuri duniani.

“Miaka mitatu iliyopita tangu soko la awali lianze tumetoka asilimia 10 sasa tunaelekea asilimia 20, lakini bado haijatosheleza, watu wanaendelea kuja baada ya kuanza kwa soko la awali, tunauza sana Uholanzi na Marekani,” anasema.

Anasema mpango mwingine mkubwa ni kuanzishwa kwa kongani za viwanda vya korosho eneo la Maranje, ili kuzikusanya korosho sehemu moja kuweka urahisi wa viwanda kuzipata, mradi huo unakusudia kubangua tani laki tatu.