Korosho za Sh99.5 bilioni zauzwa mnadani msimu wa 2023/24

Muktasari:

  • Zaidi ya Sh99.5 bilioni zimelipwa kwa wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara katika msimu wa 2023/24 ambapo bei ya korosho imeanza kuimarika sokoni kwa korosho kuuzwa kwa bei ya juu 2075 -2070 wakati mnada wa kwanza  korosho ziliuzwa kwa bei ya juu ilikuwa 2,050 hadi 1,900.

Mtwara. Zaidi ya tani 54,689,011 zenye thamani ya Sh99.5 bilioni zimeuzwa katika msimu wa mwaka 2023/24 ambapo zaidi ya kampuni 57 zimejitokeza.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu na Ofisa Masoko wa Bodi ya Korosho Tanzania, Revelian Ngaiza ametoa mwenendo wa mauzo ya korosho ghafi katika soko na mwenendo wa minada iliyoanza Oktoba 20 kupitia vyama viwili vya Tanecu na Mamcu.

Amesema kuwa mwenendo wa minada korosho ghafi 2023/2024 inatokana na mwenendo wa makusanyo ya korosho ghafi kwenye ghala za mnada na hali ya minada inayoendelea kuna uwezekano wa kukaribia kufikia lengo la uzalishaji wa korosho kwa tani 400,000.

Bodi ya korosho inaendelea kufuatilia mwenendo wa bei ya korosho ghafi katika soko la dunia na kuendelea kuwaelimisha wakulima kwenye minada inayoendelea ili wafanye maamuzi sahihi na kwa wakati sahihi.

Hivyo itaendelea kushirikiana na Mamlaka mbalimbali za Serikali katika kusimamia minada inayoendelea pia kutoa wito kwa wadau mbalimbali wa tasnia ya korosho kutoa elimu kwa wakulima juu ya mwenendo wa bei za korosho umuhimu wa kuzingatia ubora wa korosho.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mtwara & Masasi Cooperative Union (Mamcu ) Siraji Mtenguka amesema kuwa wameuza  zaidi ya tani 21,000 katika minada miwili ambapo kwa mnada wa kwanza bei ya juu 2031 na bei ya chini  1,900 huku katika mnada wa pili bei ikiimarika sokoni kwa kuongezeka Sh40.

Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Tandahimba & Newala Cooperative Union (Tanecu), Mohamed Mwinguku  amesema kuwa katika mpaka sasa wameuza tani 14,000 ambazo zimefikishwa mnadani  na kuuzwa zote ambapo zaidi ya kampuni 36 zilijitokeza mnada huo.

“Tumeuza korosho bei juu ni 2,050 na bei ya chini  ni 1,950 katika mnada wa kwanza lakini katika mnada wa pili tumeuza bei ya juu 2,060 na chini 2,050  ambapo mwitiko wa wanunuzi umekuwa mkubwa ambapo wanunuzi 36 lakini waliandika barua za kuomba kununua 46 tofatuti na msimu uliopita ambapo wanunuzi walikuwa chini ya 25” amesema Mwinguku

Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Lindi mwambao Nurdin Said Swallah amesema kuwa wameuza jumla ya kilo 1,897,047 zenye thamani ya Sh3.6 milioni kwa bei ya juu Sh2,000 na chini 1,900, katika mnada wa pili wameuza kilo 3,111,973 zenye thamani ya Sh5.8 milioini kwa bei ya juu Sh2,075 na bei ya chini 1900.

Meneja wa Chama Kikuu cha Runali, Jahida Hassan amesema kuwa mpaka sasa wameuza kilo 14,817,738 zenye thamani ya zaidi ya Sh30 milioni (30,379,777,226) katika minada miwili pekee.