Simulizi za madereva matumizi ya mafuta, gesi kwenye magari

Dar es Salaam. Utumiaji gesi asilia katika vyombo vya moto vya biashara hausaidii tu kupunguza gharama za uendeshaji, bali pia inaongeza kiwango cha fedha kwa waendeshaji.

Hiyo inawasaidia madereva wasiomiliki vyombo vya moto kuona faida ya kile wanachokifanya kutokana na kutoyumbishwa na panda shuka ya bei ya mafuta inayoendelea kushuhudiwa kwenye mataifa mbalimbali duniani.

Kwa sababu, kipindi ambacho wenzao wanalalamika makali, wao wanaendelea kununua kilo 1 ya gesi kwa Sh1,550, jambo ambalo linawapa ahueni kwa kuwa wanapata nishati wanayotumia kwa takribani nusu gharama, ikiwa wangetumia petroli au dizeli.

Petroli ambayo inatumika katika uendeshaji wa vyombo vingi vya moto kwa sasa Februari mwaka huu inauzwa kwa bei elekezi ya Sh3,051, iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Mafuta (Ewura).

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, madereva wanaofanya shughuli za usafirishaji ndani ya Jiji la Dar es Salaam licha ya kulia na uhaba wa vituo vya kujazia gesi katika magari, lakini wanafurahia faida wanazozipata.

“Nina mtungi wa kilo 15, natumia Sh15,550 kujaza na ninaweza kutembea hadi kilomita 200, ikiwa ni sehemu ambayo haina foleni ila ndani ya Jiji Dar es Salaam natumia kilomita 180 hadi 170,” anasema Heri Hemed, ambaye ni dereva wa Little Ride.

Anasema uwepo wa mfumo wa gesi kwenye gari lake ni msaada mkubwa, kwani sasa anaweza kuona faida ya kile anachokifanya kwa kutengeneza faida ya zaidi ya Sh70,000 kwa siku.

“Siku kukiwa na mzunguko mkubwa au nikiamua kukesha naweza kulala hadi na Sh150,000,” anasema Heri.

Akiwa anatumia mtungi huo kwa mwaka wa tatu sasa, panda shuka ya bei za mafuta kwake si kikwazo wala jambo linalompa hofu, bali kero pekee anayokutana nayo ni wakati wa kujaza gesi.

“Foleni kwenye vituo, wengine wakilia bei ya mafuta sisi tunalia na foleni, huwezi kusema uko na mteja upite mara moja ujaze muendelee na safari, ni ngumu.

Maneno yake yanaungwa mkono na Leah, ambaye pia ni dereva wa usafirishaji abiria ndani ya jiji hili anayesema kwake Sh23,250 inatosha kumruhusu kufanya safari zake za usafirishaji abiria kwa siku takribani tatu bila mawazo.

Ikiwa ni siku yenye wateja wengi, hutumia siku mbili au moja na nusu, bado akionyesha ahueni akilinganisha na utumiaji wa mafuta.

“Katika Sh23,250 ni kama lita 8 kasoro kidogo, huwezi zunguka hata siku mbili na nusu, labda uwe unaenda umbali mfupi na si muda wote uwe barabarani,” anasema.

Akiwa na miaka miwili akitumia mfumo huo, amefanikiwa kupata mafanikio ya haraka ambapo badala ya kuendelea kuendesha gari ya bosi wake pekee na yeye ameweza kupata bajaji inayomletea kipato.

“Nilipohama kwenye mafuta niliona mabadiliko makubwa, gharama ya uendeshaji ilishuka, nikawa nabaki na kiwango kikubwa cha fedha, baada ya kumaliza deni la bosi nikaona nami nijiwekeze,” anasema Leah.

Kwa sasa anajisikia fahari juu ya uamuzi alioufanya, kwani amewawezesha vijana wawili kupata sehemu za kuendeshea maisha yao baada ya mmoja kumpa bajaji na mmoja pikipiki.

“Nilikopa lakini najivunia kwa sababu nimepiga hatua mbele zaidi kuelea mafanikio,” anasema.

Unufaikaji wa matumizi ya gesi katika vyombo vya kusafirishia abiria haukuishia katika magari tu, bali hata bajaji nao wamefikiwa na sasa wanafurahia kuondokana na adha ya mabadiliko ya bei za mafuta.

Bajaji ambazo siku za hivi karibuni nazo zimeanza kunufaika na mifumo hiyo imekuwa mkombozi kwa madereva na wamiliki, licha ya awali kutakiwa kuumia ili kupata fedha za kufunga mfumo huo.

“Mimi ndiye nilipeleka wazo la kubadili mfumo kwenye bajaji kuweka gesi, bosi akasema hana hela, nilifanya utafiti nikagundua kuna kampuni inakopesha na unakuwa unalipa kiwango fulani cha pesa, basi niliongea na bosi tukakubaliana kuchangia gharama,” anasema Boaz Msakuzi, dereva wa bajaji.

Anasema kupitia Sh10,000 waliyotakiwa kupeleka kila siku katika sehemu waliyokopeshwa kufungiwa mfumo huo, mmiliki wa chombo chake cha moto alikubali kutoa Sh5,000 na akiongeza fedha inayobakia hadi walipomaliza deni.

“Nilipomaliza deni ndani ya miezi mitatu tulikaa chini na bosi tukaweka makubaliano, ila ukweli mimi ndiyo mnufaika zaidi maana sasa nusu ya fedha niliyokuwa nikiitumia katika mafuta inabaki kwangu,” anasema.

Akiwa na mtungi wa kilo 4 katika bajaji yake amekuwa akitumia Sh6,200 pekee kufanya safari zake za siku nzima na wakati mwingine hadi siku mbili bila hofu.

“Lakini kwenye mafuta hiyo hela ungepata lita ngapi? Yasingetosha kufanya safari za siku nzima bila kupumzika, labda wakati wa kula pekee maana ukiwa unafanya biashara ya usafirishaji mtandaoni unakuwa na wigo mpana wa kupata abiria,” anasema Msakuzi.

Alichokizungumzia Msakuzi juu ya ukopeshwaji wa mifumo ya gesi kwenye bajaji, Mwananchi ilifuatilia na kubaini kuwa huduma hiyo inatolewa pia hata kwa wamiliki wa magari.

Baadhi ya kampuni zinafunga huduma hiyo na kumruhusu mmiliki wa gari kulipa kiwango fulani cha fedha ndani ya mwaka mzima, huku kwa bajaji zikipewa siku kati ya 120 na 150 kumaliza deni lake.


Wanaotumia mafuta



Wakati wanaotumia gesi wakifurahia kile wanachokifanya kwa watu wanaotumia mafuta, bado wanayo maumivu kidogo, huku wakieleza kuwa upatikanaji wao wa fedha za ziada unategemeana na bei za mafuta.

Ikiwa bei zitapanda, ni ngumu kwao kuongeza kiwango cha nauli kwa wateja, kwani hawapangi wao na badala yake wanafanya kazi kwa hasara.

“Kwa siku naweza kutumia kati ya Sh40,000 hadi Sh70,000 ikiwa nataka kufanya kazi kwa saa nyingi, sasa hapo niingize kiasi gani ili niione faida, watu wa gesi wana ahueni kubwa sana,” anasema Hafidh Hassan.

Licha ya kuugulia maumivu ya bei za mafuta kila mwezi ikiwa zitaongezeka, lakini bado hana utayari ya kubadili gari yake kuingia katika mfumo wa gesi.

“Siyo kwamba sina hela, pia kama sina kuna kampuni zinakopesha, lakini wafungaji wengi wa kubadili hii mifumo Tanzania bado nina shaka nao, endapo watafanya si kwa kiwango cha ubora unaotakiwa unaweza kufanya gari ikose nguvu,” anasema Hassan.

Wakati yeye akiyasema hayo kwa Adrian Msangi ni tofauti, kwani kukosa fedha ndiyo kunamfanya aendelee kutumia mafuta hadi leo.

“Kila nikipanga kubadilisha mambo yanaingiliana, nakosa namna ila ningekuwa na hela ningebadili tangu 2022, maana kila mafuta yakipanda bei tunazidi kuumia,” anasema Msangi, ambaye aliamua kujiajiri katika usafirishaji baada ya kumaliza chuo.

Endelea kufuatilia ukurasa huu kila siku kufahamu zaidi kuhusu gesi asilia na mifumo yake kwenye magari hapa nchini na harakati za Serikali katika kukabiliana na bei za nishati, hasa petroli na dizeli ili kuleta nafuu kwa wananchi.