Wafanyabiashara Kariakoo watakiwa kuhakiki taarifa

Muktasari:

  • Waliokuwa wafanyabiashara kwenye soko la Kariakoo wameombwa kuendelea kuhakiki taarifa zao wakati ambao soko hilo linaelekea kukamilika.

Dar es Salaam. Wakati ukarabati wa soko la zamani umefikia asilimia 85 na ujenzi wa soko jipya kufikia asilimia 71, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Masoko ya Kariakoo imewahimiza waliokuwa wafanyabiashara kuendelea kuhakiki taarifa zao.

 Akizungumza leo na vyombo vya habari baada ya ukaguzi wa maendeleo ya soko hilo, Mwenyekiti wa Bodi, Hawa Ghasia amesema wanatekeleza zoezi hilo kwa ajili ya mchakato wa kuwapatia maeneo ya biashara pindi soko litakapo kamilika Oktoba mwaka huu.

Ghasia amesema hadi sasa wameshawahakiki wafanyabiashara 1,404 kati ya 1,662 hivyo wanawaomba wale wote ambao bado waendelee na zoezi.

“Tunawahakiki kwa lengo la kuwapatia nafasi kwa wale watakaopenda tena kurudi hapa. Hivyo tunawaomba ambao bado wahakiki ili tujue kuwa wapo tusije kumpa nafasi mtu mwingine,” amesema Ghasia.

Akifafanua kuhusu utaratibu wa kugawa nafasi za biashara kwa watu sokoni hapo amesema mchakato utakuwa wa wazi ili kila mwananchi mwenye sifa aweze kupata.

“Tumeshaweka mfumo wa Tehama na wakati ukifika tutawatangazia utaratibu wa jinsi ya kuomba na jinsi tutakavyogawa. Tunawakikishia mchakato wote utakuwa ni wa wazi ili hata mtu akikosa ajue ni kwanini amekosa,” amesema Ghasia.

Naye Meneja wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Sigsibert Kaijage amesema baada ya mradi huo uliogharimu Sh28 bilioni kukamilika utachukua wafanyabiashara 2,300 ikiwa ni ongezeko kutoka wafanyabiashara 1,662 hivyo zitatengenezwa ajira zaidi ya 4000.

“Hii ni faida kwa Watanzania na serikali kwa ujumla kwani itaingiza mapato ya kutosha. Kama bodi tunapenda kumshukuru Rais Samia,” amesema.

Akizungumzia mazingira ya ufanyaji biashara na shughuli zingine sokoni hapo ameweka wazi kuwa soko litakuwa na mpangilio wa biashara wa kisasa kuwezesha urahisi wa bidhaa kupatikana na miundombinu rafiki kwa kina mama na wenye mahitaji maalum.

Kaijage vilevile amefichua kuwa, kwa namna soko lilivyojengwa na kukarabatiwa limebaki na muonekano wake uleule wa zamani hivyo litaweza kuvutia watalii.

Soko la Kariakoo lilipata ajali ya moto Julai 10, 2021, na kusababisha hasara ya mali za wafanyabiashara na serikali.

Januari 7, 2022 Serikali iliamua kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kimkakati utakaokarabati na kujenga soko jipya la kisasa na kimataifa la ghorofa nane ambazo mbili za chini (Basement) na sita za juu.

Majukumu haya ya utekelezwaji yako kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na.36 ya mwaka 1974 iliyoanzisha shirika.