Watanzania watakiwa kuzingatia ubora wa bidhaa

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  •  Kampuni ya Haier iliingia rasmi ubia na kampuni ya GSM Group mwaka 2023 kwa lengo la kuleta bidhaa zenye ubora sokoni sokoni.

Dar es Salaam. Watanzania wametakiwa kuzingatia ubora wanaponunua bidhaa, ili kuepuka hasara kwa kununua bidhaa zisizodumu na zinazotumia nishati nyingi.

 Hayo yameelezwa jana Aprili 19, 2024 katika mkutano wa uzinduzi wa bidhaa za viyoyozi (AC) zinazouzwa na kampuni ya Haier Tanzania.

Kampuni ya Haier iliingia rasmi ubia na kampuni ya GSM Group mwaka 2023 kwa lengo la kuleta bidhaa zenye ubora sokoni sokoni.

“Tangu uanzishwaji wa kampuni ya Haier, Tanzania, tumekuwa tukijitahidi kuangalia matakwa ya soko na kuhakikisha tunaboresha huduma na ufanisi wa bidhaa zetu kwa watumiaji,” amesema Meneja wa Haier Tanzania, Leon Liuchi.

Ameongeza, “Sifa kubwa za bidhaa hizi za AC ni mfumo wake imara na wa kisasa unaosababisha matumizi kidogo ya umeme pamoja na uwezo mkubwa wa utendaji kazi katika kutoa hali ya ubaridi kwa haraka.”

Kwa upande wake, meneja wa biashara wa kampuni hiyo, Ibrahim Kiongozi amesema baada ya kuona mafanikio katika mauzo ya bidhaa za elektroniki, sasa mipango ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na biashara.

“Tuna mipango mikubwa ya kuendeleza biashara, mpaka sasa tuna maduka sita nchini na bado tunapanga kuongeza maduka katika mikoa mikubwa.

“Tanzania ni kituo cha kwanza, GSM na Haier tunaangalia uwezekano wa kuifanya Tanzania iwe kitovu kwa Afrika Mashariki katika uzalishaji na biashara. Hapo namaanisha kukuza biashara na kufungua kiwanda hapa nchini, kwa sasa tuko kwenye hatua za awali,” amesema.

Akizungumzia ubora wa bidhaa zao, Kiongozi amesema lengo ni kupunguza gharama kwa wananchi.

“Kwa mfano hivi viyoyozi vyetu, sio tu kuleta baridi wakati wa joto, vipo pia vya kuleta joto wakati wa baridi, kwa hiyo ile kuwasha kuni, kuwasha mkaa haipo tena, unaweka joto kulingana na hali ya hewa iliyopo.

“Pia teknolojia inayotumika inazingatia mahitaji ya umeme wa Tanzania na Afrika kwa ujumla, kwa baadhi ya maeneo bidhaa zetu zina uwezo wa kupunguza umeme kwa aislimia 70,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa kampuni za GSM Group, Benson Mahenya amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada za kukuza uchumi na kuwezesha uwekezaji.

“Tunaungana na juhudi za kukuza uchumi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, tunajitahidi kushiriki katika shughuli mbali mbali za kijamii zikiwemo udhamini wetu katika michezo,” amesema.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau na watumiaji wa bidhaa za kielekroniki wakiwemo wataalamu wa ujenzi, wasanifu majengo, wafanyabiashara wa vifaa vya kilektroniki, taasisi mbalimbali za kiserikali na wafanyakazi wa kampuni za GSM Group pamoja na Haier.