Mambo mawili yaikwaza Tanzania katika mkataba wa utawala bora

Mawaziri, manaibu waziri na Katibu wa Bunge wakila kiapo cha maadili ya viongozi wa umma baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli kushika nyazifa zao katika hafla iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Kilio hicho cha Katiba kinaendelea huku makundi mengine ya jamii yakiwa hayana habari wala kuona umuhimu huo.

Wimbo wa Katiba Mpya bado unavutia masikio ya sehemu kubwa ya Watanzania. Lengo la wanaotaka Katiba hiyo mpya ili kuboresha utaratibu wa namna ya kujitawala na kuongeza wigo katika masuala ya demokrasia na utawala bora.

Kilio hicho cha Katiba kinaendelea huku makundi mengine ya jamii yakiwa hayana habari wala kuona umuhimu huo.

Kutokana na hali hiyo, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi 16 za Afrika zilizokataa kutia saini na kuridhia mkataba wa Umoja wa Afrika unaohusu demokrasia, uchaguzi na utawala bora (ACDEG) uliopishwa mwaka 2012.

Tanzania ikiwa nchi pekee ya Afrika Mashariki ambayo haijaridhia kabisa mkataba huo, nchi za Kenya, Uganda na Burundi zimeridhia bila kuutia saini.

Rwanda ndiyo nchi pekee ya Afrika Mashariki iliyofanya yote mawili; kuridhia na kutia saini mkataba huo, ikiwa miongoni mwa nchi 10 za Afrika zilizofanya hivyo, huku nchi nyingine 28 zikiwa zimeridhia pekee bila kusaini.

Mkataba huo ni nyenzo ya utekelezaji wa malengo ya Mkakati wa Utawala wa Afrika (AGA) Afrika kuelekea mwaka 2063 unaolenga kuchochea mijadala miongoni mwa wadau wanaotetea utawala bora na demokrasia barani Afrika.

Kutosainiwa kwa mkataba huo kumekuja wakati makundi ya watu vikiwemo vyama vya upinzani nchini yakilalamika kuwapo ukandamizwaji wa demokrasia na uhuru wa kutoa maoni.

Tayari maaskofu wa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) yameshatoa matamko ya kuikosoa Serikali kuhusu namna inavyosimamia masuala ya demokrasia na uhuru wa kutoa maoni, huku vyama vya upinzani vikipinga makatazo ya kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.

Pengine hali hiyo inayoendelea nchini ndiyo ingekuwa fursa muhimu ya kusaini mkataba huo na kuuridhia ili kuondoa mkwamo, lakini Serikali inazo sababu za kusita kufanya hivyo pamoja na kwamba zinapingwa na wachambuzi wa suala hilo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Kikanda na Afrika Mashariki, Dk Susan Kolimba anaeleza sababu za Tanzania kusita kuridhia na kutia saini mkataba huo, akisema kwamba hauendani na sheria, kanuni na taratibu. Pia, anasema unakinzana na Katiba iliyopo.

“Tanzania itaridhia mkataba huo iwapo taratibu zote za kisheria na kanuni za nchi yetu za kuridhia mikataba ya kimataifa zimefuatwa, ikiwemo kutokukinzana kwa mkataba huo na Katiba ya nchi yetu,” alisema Dk Kolimba kwa ujumbe mfupi wa simu alipoulizwa na mwandishi wa makala haya.

Akifafanua zaidi, Dk Kolimba anasema: “Mkataba unatambua masuala ya mgombea binafsi katika nafasi ya urais, kupingwa kwa matokeo mahakamani na mengineyo, wakati Katiba yetu haina masuala hayo,” anasema na kuongeza:

“Kama Tanzania itatafakari na kuamua kuridhia mkataba huo, italazimika kufanya marekebisho ya Katiba na sheria za uchaguzi.”

Maelezo ya Waziri Kolimba yameibua mjadala mpya katika kilio cha Katiba Mpya kutoka kwa wanasiasa na wachambuzi wa masuala ya siasa.

Mbunge wa Temeke ambaye pia ni Naibu Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, Abdallah Mtolea anasema hatua ya Serikali si ajabu, imekuwa ni tabia kwake kuchelewa kuridhia au kutia saini mikataba ya kimataifa bila sababu za msingi.

“Kwanza kuna tatizo kubwa la Serikali kuchelewa kuridhia mikataba ya kimataifa. Utakuta mikataba inachukua miaka sita hadi 10, bila sababu za msingi:

“Pili, kinachozungumzwa kwenye mkataba huo tumekuwa tukikizungumza kwa muda mrefu. Mambo ya kupinga matokeo ya rais yalishazungumzwa na yanazungumzika. Tunapinga matokeo ya wabunge na madiwani, lakini na ya matokeo ya uchaguzi wa rais pia lazima yapingwe.”

Aliendelea kusema hata suala la mgombea binafsi lilishazungumzwa na kufikishwa mahakamani, kwa hiyo si jambo geni.

“Kusema Katiba inazuia siyo sababu ya msingi kwa sababu inarekebishika. Lakini, pia inatoa fursa ya kufanya mabadiliko ya Katiba, kwani hicho ndicho kilichokuwa kilio cha wananchi wakati wa mchakato,” anasema.

“Unaposema nchi nyingi za Afrika hazijaridhia wala kutia saini mkataba huo, ndiyo kuonyesha kuwa hawapendi utawala bora wala demokrasia, bado tuna safari ndefu,” anaongeza Mtolea.

Akijadili suala hilo, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Hebron Mwakagenda anasema mkataba wa kimataifa unapaswa kuwa juu ya Katiba ya nchi pindi ukishapitishwa na jumuiya husika.

“Kunapokuwa na mkataba wa kimataifa, Katiba inakuwa chini, kwa sababu walishakubaliana kuupitisha. Sasa unapokuja kusema hauendani na Katiba utaelewekaje?” anahoji Mwakagenda na kuongeza:

“Nadhani wanajaribu tu kukwepa jukumu lao. Kwanza hivyo vipengele vya mkataba vimeshajadiliwa wakati wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba wakati katika kipindi cha Rais mstaafu, Jakaya Kikwete. Suala la mgombea binafsi, Mchungaji Christopher Mtikila alishinda kesi. Kwa hiyo hicho kisingizio cha Katiba hakina mashiko.”

Mkataba wenyewe

Kifungu cha 3 cha mkataba huo kinafafanua kanuni zake ambazo ni pamoja na demokrasia na haki za binadamu na kuimarishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Katika kifungu cha 4(1) mkataba huo unazungumzia utawala wa sheria kwa lengo la kuimarisha demokrasia, haki za binadamu na utekelezaji wa sheria katika nchi za Afrika.

Pia, mkataba huo katika kifungu cha 4(2) unaelea haja ya wananchi kushiriki haki za msingi kama kupiga kura wakati kifungu cha tano kikizungumzia kuheshimiwa kwa Katiba katika ubadilishaji wa madaraka.

Kana kwamba haitoshi, kifungu cha sita kinazungumzia haki ya wananchi kutumia haki ya msingi ya Uhuru na Haki za Binadamu huku kifungu cha 8 (1) kikikataza unyanyasaji wa haki za wanawake na kile 8(2) kikitaka wanawake na makundi madogo ya kikabila na walemavu wahakikishiwe kisheria kufurahia hai zao.

Vifungu cha 10, 11 na 12 vinataka Katiba kama sheria mama ziheshimiwe katika nchi zitakazosaini mkataba huo, huku pia vikitaka kuwapo kwa mfumo wa sheria na sera utakaosimika utamaduni wa demokrasia na amani.

Vifungu cha 13, 14 na 15 vinaeleza na kufafanua haja ya kuimarisha mijadala ya kijamii, maendeleo ya umma na uwazi. Vilevile vinataka kuimarishwa na kuwezeshwa kwa wananchi kitaasisi kulidhibiti jeshi na majeshi ya usalama ili kuhakikisha demokrasia inatawala.

Vinataka pia taasisi za umma kama vile Bunge, Mahakama na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kutetea demokrasia.

Kuhusu uchaguzi, kifungu cha 16 kinaeleza umuhimu wa kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki ikiwa pamoja na kuwa na vyombo huru vya kusimamia uchaguzi, mkakati wa kitaifa wa kutatua malalamiko ya uchaguzi, nafasi sawa kwa wagombea kwa vyombo vya habari na mazingira yote kwa ujumla ya uhuru wa uchaguzi.

Kuhusu utawala wa kisiasa kiuchumi na kijamii, mkataba huo unataka kuimarishwa kwa Bunge na vyama vya siasa na vya kiraia vinavyotambuliwa kisheria na Serikali inapaswa kuwa na mijadala ya nguvu kati yake na vyama vya kiraia na sekta binafsi.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sera, Utawala na Uchumi, Moses Kulaba alieleza kuishangaa Tanzania kuwa licha ya kukubali kuwa makao makuu ya Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika bado haitaki kusaini mkataba huo.

“Inashangaza kuona Tanzania imeridhia kuwa makao makuu ya Mahakama ya Umoja wa Afrika, lakini haitaki kusaini mkataba wa uchaguzi huru, demokrasia na utawala bora,” anasema Kulaba.

Hata hivyo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Nguruma alisema bado mkataba huo ni mpya hivyo elimu zaidi inahitajika kwa wadau ili kuishinikiza Serikali iuridhie.