Uhusiano wa Tanzania na Uturuki ni wa kiuchumi na kirafiki

Muktasari:

Uhusiano huo uliohuishwa mwaka 2009 baada ya kuvunjika mwaka 1984, umekuwa na matumaini baada ya ziara ya siku mbili ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan nchini

Uhusiano wa Tanzania na Uturuki ulioasisiwa mwaka 1979, umefungua ukurasa mpya baada ya mataifa hayo kutiliana saini mikataba ya ushirikiano ambayo itaiwezesha Tanzania kunufaika zaidi katika sekta mbalimbali za elimu, utalii, viwanda, usafirishaji na afya.

Uhusiano huo uliohuishwa mwaka 2009 baada ya kuvunjika mwaka 1984, umekuwa na matumaini baada ya ziara ya siku mbili ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan nchini. Serikali ya Uturuki ilianzisha ubalozi wake nchini mwaka 2009. Tanzania pia imeanza maandalizi ya kuwa na ubalozi nchini Uturuki mwaka huu na tayari Rais John Magufuli amemteua Elizabeth Kiondo kuwa balozi wa Tanzania nchini humo.

Si mara ya kwanza kwa viongozi wa mataifa haya kutembeleana lakini ziara ya Rais Erdogan imekuwa chachu ya kukuza diplomasia ya kiuchumi na kuimarisha maendeleo ya Tanzania kwa kuongeza biashara na uwekezaji.

Uturuki ilikuwa na uwekezaji wa Dola za Marekani 150 hadi kufikia mwaka 2015 lakini imepanga kuongeza uwekezaji mpaka kufikia dola 500 milioni. Fursa ambayo itaongeza nafasi za ajira kwa Watanzania wengi.

Mapema wiki hii, Tanzania na Uturuki zilitiliana saini makubaliano ya ushirikiano mbele ya viongozi wa mataifa hayo, Rais Magufuli na Erdogan. Viongozi hao walisisitiza kuimarisha ushirikiano wao kwa lengo la kukuza uchumi na maendeleo ya mataifa hayo.

 Mikataba tisa yasainiwa

Tanzania na Uturuki zimetiliana saini mikataba tisa katika sekta za utalii, elimu, viwanda, diplomasia, usafirishaji, utangazaji na afya. Mikataba hiyo itaipa nafasi Tanzania kujifunza mambo mbalimbali kutoka Uturuki.

Mikataba iliyosainiwa ni makubaliano ya ushirikiano baina ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na Shirika la Ndege la Uturuki; makubaliano ya Ushirikiano kati ya Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) na Shirika la Utangazaji la Uturuki (TRT) na mkataba wa maendeleo kati ya Tanzania na Uturuki.

Mikataba mingine ni makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya elimu na utafiti; ushirikiano baina ya Shirika la Viwanda Vidogovidogo (Sido) na shirika la kuhimiza viwanda vidogo na vya kati Uturuki.

Vilevile, Tanzania na Uturuki zimekubaliana kushirikiana katika sekta za utalii, viwanda vya ulinzi, afya na ushirikiano baina ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na Chuo cha Diplomasia cha Uturuki.

Akizungumzia ushirikiano katika sekta ya utalii, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe anasema mkataba huo utasaidia Tanzania kutangaza vivutio vyake vya kitalii huko Uturuki na Ulaya kwa ujumla.

Profesa Maghembe anasema wataalamu wa Tanzania watakwenda Uturuki kujifunza na kubadilishana uzoefu katika kusimamia sekta ya utalii kwa kuwa nchi hiyo inafanya vizuri kwenye eneo hilo, hivyo ni nafasi nzuri kujifunza kupitia ushirikiano huo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema Uturuki itaisaidia Tanzania kwa kutoa mafunzo ya kutumia mfumo wa udhibiti wa taarifa za hospitali.

“Mfumo huo utakuwa wa kielektroniki ambao utahifadhi taarifa zote za wagonjwa na takwimu. Kwa mfano, tutajua kirahisi wagonjwa wa kifua kikuu wako wangapi au wagonjwa wa moyo ni wangapi. Pia, mfumo huo utaisaidia Serikali kukusanya mapato kwa sababu uko wazi,” anasema.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage anasisitiza azma ya Uturuki kuongeza uwekezaji nchini kutoka Dola za Marekani milioni 150 mwaka jana mpaka kufikia Dola milioni 500.

“Wenzetu Waturuki wanatengeneza spea za ndege, sasa na sisi tuna Bombadier zetu, kwa hiyo tumekubaliana kuanzisha kiwanda cha kutengeneza spea za ndege hapa nchini kwa ushirikiano na Serikali ya Uturuki,” anasema.

Katika sekta ya elimu, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya anasema makubaliano hayo yatatoa fursa kwa Tanzania kubadilishana taarifa katika masuala ya elimu na nafasi za masomo kwa wanafunzi kutoka Tanzania kwenda Uturuki.

Azma ya Serikali

Rais Magufuli anasema Tanzania kuna miradi 30 ya Waturuki yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 305 ambayo imetoa ajira kwa Watanzania 2,950. Anasisitiza azma ya Serikali yake kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi hasa katika sekta ya kilimo.

Anasema biashara kati ya Tanzania na Uturuki imepanda kutoka Dola za Marekani milioni 66 mwaka 2013 hadi kufikia Dola milioni 190 mwaka jana. Anasisitiza kuwa baada ya ziara hiyo, uwekezaji utaongezeka nchini.

Rais Magufuli anasema amekubaliana na Rais Erdogan kushirikiana katika sekta mbalimbali na hilo litafanyika kirahisi zaidi baada ya Tanzania kuanzisha ubalozi wake nchini Uturuki. Anasisitiza kuwa uchumi ni uhusiano; uchumi ni urafiki na kuwa nchi hizo zitaendelea na urafiki huo.

Ijue Uturuki

Uturuki ni nchi iliyo kati ya Bara la Asia na Ulaya, sehemu kubwa iko Asia ya Magharibi lakini sehemu ndogo ya eneo lake upande wa Magharibi wa Bosporus, Ulaya.

Sehemu kubwa ya mipaka yake ni bahari: Mediterranean upande wa Magharibi na Kusini; na Bahari Nyeusi upande wa Kaskazini. Kwenye nchi kavu imepakana na Ugiriki na Bulgaria upande wa Kaskazini Magharibi na Mashariki imepakana na Georgia, Armenia na Azerbaijan na imepakana na Iran, Iraq na Syria na upande wa Kusini.

Sehemu kubwa ya eneo lake ni Anatolia inayoonekana kama rasi kubwa kati ya Mediterranean na Bahari Nyeusi. Hali ya nchi ndani ya Anatolia mara nyingi ni yabisi na kilimo kinategemea umwagiliaji.

Sehemu ya Mashariki ya Uturuki kuelekea Uajemi ina milima mingi. Maeneo ya Pwani yanapokea mvua na huwa na rutuba.

Uturuki iliundwa na kuwa taifa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Waturuki waliwahi kuwa kiini cha milki ya Osmani (Ottoman Empire) iliyounganisha mataifa mengi chini ya Sultani wa Konstantinopoli.

Jamhuri ya Uturuki ilianzishwa mwaka 1923 na Jenerali Kemal Atatürk.

Atatürk alileta mabadiliko mengi yaliyolenga kuondoa utamaduni wa kale wa Waosmani na enzi za utawala wa sultani.

Mji mkuu wa nchi hiyo ni Ankara. Mji mkubwa wa kibiashara ni Istanbul ambao zamani ulikuwa ukijulikana kama Konstantinopoli ambao ndiyo uliokuwa mji mkuu wa Dola la Uturuki hadi mwaka 1923. Uturuki ina wakazi zaidi ya milioni 76.

Uchumi

Uturuki inatafsiriwa kuwa ni nchi ya uchumi wa soko linalochipua. Ni miongoni mwa nchi zilizoendelea duniani kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Pato la Taifa la nchi hiyo ni la 17 kwa ukubwa duniani. Ni miongoni mwa nchi wazalishaji wakubwa wa bidhaa zitokanazo na kilimo na pia ni mzalishaji wa vyombo vya moto kama vile magari, meli na vifaa vingine vya aina hiyo. Pia, vifaa vya ujenzi na vifaa vya elektroniki. Uturuki ilijiunga na umoja wa forodha wa Umoja wa Ulaya (EU) kuanzia Desemba 31, 1995.

Wakati nchi nyingi zikishindwa kujikwamua kutokana na mdororo wa kiuchumi, Uturuki imeongeza ukuaji wake wa kiuchumi kwa asilimia 9.2.

Wachumi na wanasiasa wanaiweka uturuki katika kundi la nchi mpya za viwanda na ni miongoni mwa nchi zenye uchumi wa soko unaochipua.

Kwa mujibu wa ripoti maalumu iliyotolewa na Financial Times kuhusu Uturuki, wafanyabiashara wakubwa wa nchi hiyo na maofisa wa serikali, wanaamini kwamba njia ya haraka ya kukua katika biashara ya nje ni kuondokana na masoko ya asili ya nchi za Magharibi.

Kuanzisha ushirikiano wa kibiashara na nchi za Afrika ni miongoni mwa mkakati wa Uturuki wa kupanua soko lake.

Hata hivyo, mwaka 2016 fedha yake (Lira) ilishuka thamani kwa asilimia 20 dhidi ya dola ya Marekani na uchumi wa nchi hiyo uliporomoka kwa asilimia 2.5.

Kisiasa

Mfumo wake wa kisiasa ni wa kisekula. Waziri Mkuu ni kiongozi wa Serikali na rais ni kiongozi wa nchi.

Muundo wa kisiasa umejikita katika kutenganisha mamlka za utendaji (serikali) ambayo kazi zake zinasimamiwa na Baraza la Mawaziri, utungaji sheria unafanywa na Bunge na utekelezaji wa sheria unafanywa na mahakama. Kila mhimili unajitegemea.

Rais anachaguliwa kila baada ya miaka mitano. Rais anapaswa awe na miaka zaidi ya 40 na angalau awe na elimu ya shahada ya kwanza katika fani yoyote. Rais Erdogan ameshika wadhifa huo tangu mwaka 2014 na kabla ya hapo alikuwa waziri mkuu (2003 – 2014).

Kuanzia 1994 hadi 1998, Erdogan alikuwa Meya wa Istanbul. Kabla ya kuwa meya, Erdogan alikuwa mchezaji mpira wa kiwango cha kati. Mwaka 2001, alianzisha chama cha siasa kinachoitwa Justice and Development Party (AKP) ambacho kwa mara tatu kiliongoza katika matokeo ya uchaguzi mkuu (2002, 2007, 2011).

Waziri mkuu anateuliwa na rais na kupigiwa kura ya imani na bunge. Waziri mkuu ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali na na muungano wa vyama na kiongozi wa baraza la mawaziri. Waziri mkuu wa sasa ni Binali Yildirim aliingia madarakani Mei 23 mwaka jana.