Jinsi Jerusalem walivyoadhimisha Ijumaa Kuu kimya kimya bila mikusanyiko

Muktasari:

  • Kwa mara ya kwanza mji wa Jerusalem umeshuhudia waumini wa Kikristo wakisalia nyumbani baada ya makanisa kufungwa.

Jerusalem, Israel. Kwa mara ya kwanza waumini wa Kikristo mjini Jerusalem, Israel wameadhimisha siku ya kukumbuka kuteswa na kusulubiwa kwa Yesu Kristo maarufu Ijumaa Kuu bila kwenda kanisani.

Wakristo duniani kote juzi waliadhimisha Ijumaa Kuu ambako kwa miaka mingine yote huazimishwa kwa kwenda kanisani na kutafakari kufa na kuteswa kwa Yesu Kristo.

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa mwaka huu ambako waumini wa mji huo walilazimika kusalia nyumbani kutokana na tishio la maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Machi, 2020 Serikali ya Israel ilitangaza kupiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima pamoja na kushiriki ibada ili kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya corona.

Mjini Jerusalem ambako kwa kawaida maelfu ya waumini hushiriki maandamano ya njia ya msalaba ambayo inaaminika Yesu Kristo alipita kabla ya kusulubiwa hali ilikuwa tofauti kutokana na maeneo matukufu kufungwa.

Kwa upande wa mji wa Roma, ibada kama hiyo inayowavutia maelfu ya mahujaji wa kikristo kila mwaka imefutwa.

Aidha, mikusanyiko yote ya umma imepigwa marufuku katika mji huo ambao umerekodi idadi ya vifo vingi vilivyotokana na virusi vya corona.

Italia yenye wagonjwa 147,577 wa corona mpaka jana mchana watu 18,849 waliripotiwa kufariki dunia.

Virusi vya corona viligundulika miezi minne iliyopita vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,716,372 duniani kote.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani ilisema kuwa kufuatia mlipuko huo, Papa Francis ataendesha ibada ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro bila ya kuwapo waumini.

Kilele cha kumbukumbu hizo itakuwa siku leo wakati wakristo wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka, kukumbuka kukufuka kwa Yesu Kristo.

Katika hatua nyingine, makundi ya kihalifu nchini Italia yemeanza kusambaza chakula na kutoa mikopo isiyo na riba kwa watu wenye uhitaji mkubwa ili kutanua ushawishi wake wakati taifa hilo likipambana na virusi vya corona.

Mwandishi mashuhuri wa vitabu, Roberto Saviano ameonya iwapo Umoja wa Ulaya (EU), haitochukua hatua, fedha za makundi hayo zitasambaa bila kizuizi.

Saviano alisema makundi ya kihalifu ya Mafia pia yanalenga kuchukua biashara zilizoyumba wakati Italia inasubiri msaada wa kifedha kutoka EU.