Jordan yatoa kauli vita ya Iran na Israel

Mfalme wa Jordan na mkewe

Muktasari:

  • Jordan nchi ambayo inapakana na Israel upande wa magharibi na Iran baada ya Iraq kwa upande wa mashariki imetoa kauli hiyo baada ya kunasa makombora na ndege zisizo na rubani katika usiku wa mashambulizi ya makombora ya Iran.

Jordan. Baada ya Iran kurusha makombora zaidi ya 300 mwisho wa wiki hii nchini Israel kwa lengo la kulipa kisasi, hatimaye nchi ya jirani ya Jordan imeibuka na kusema haitaki kuwa uwanja wa vita.

 Jordan nchi ambayo inapakana na Israel upande wa magharibi na Iran baada ya Iraq kwa upande wa mashariki imetoa kauli hiyo baada ya kunasa makombora na ndege zisizo na rubani katika usiku wa mashambulizi ya makombora ya Iran.

Shirika la Habari la AFP limesema Mfalme wa nchi hiyo, Abdullah II amesisitiza nchi yake haipaswi kuwa ‘jumba la vita vya kikanda’ huku mamlaka ikisema lengo lake lilikuwa kujilinda yenyewe badala ya kuilinda Israel.

Jordan inatajwa kuwa miongoni mwa mataifa, yakiwemo Marekani ambayo yaliisaidia Israel kuzuia makombora na ndege zisizo na rubani zilizorushwa na Iran.

Katika hilo, waziri wa zamani wa habari wa Jordan, Samih al-Maaytah, amesema nchi hiyo haikutetea Israel, bali ilitetea mamlaka yake na usalama wa eneo lake.

"Jordan haina uhusiano wowote na mapambano kati yao. Haitaki kujihusisha katika mzozo wa kikanda," aliiambia AFP.

Hayo yalijiri baada ya Iran kuishambulia Israel ikiwa ni kitendo cha kujilinda baada ya shambulio la Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo uliopo Damascus nchini Syria mwanzoni mwa mwezi huu lililoua makamanda wa Kiiran.

Hata hivyo, inaelezwa kwamba vita vya Gaza vinavyoendelea tangu Oktoba 7, 2023 kati ya Hamas na Israel vimeleta changamoto kwa Jordan pia na sasa inakabiliwa na tishio la kuwa katikati ya mzozo kati ya Israel na Iran.

Inaelezwa Jordan, ambayo karibu nusu ya wakazi wake wana asili ya Palestina, pia ni mshirika wa karibu wa Marekani na ilitia saini mkataba wa amani na taifa jirani la Israel miaka 30 iliyopita.