Mgombea wa upinzani Senegal aongoza matokeo ya awali ya uchaguzi

Muktasari:

  • Mamilioni ya wananchi wa Senegal walipiga kura Jumapili kumchagua Rais wa tano wa nchi hiyo.

Dakar. Wafuasi wa mgombea urais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye wamejitokeza katika mitaa ya mji mkuu, Dakar kusherehekea matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika jana, Machi 24, 2024, yakionyesha mgombea huyo wa upinzani anaongoza.

Sherehe hizo zilifanyika huku wagombea wasiopungua watano kati ya 19 katika kinyang'anyiro hicho wakitoa taarifa kumpongeza Faye kwa kile walichokiita ushindi wake.

Hata hivyo, mpinzani wake mkuu kutoka muungano unaotawala, Waziri Mkuu wa zamani, Amadou Ba, amesema sherehe hizo zilikuwa kabla ya wakati wake.

“Kwa upande wetu, na kwa kuzingatia mrejesho wa matokeo kutoka kwenye timu yetu ya wataalamu, tuna uhakika kwamba katika hali mbaya zaidi, tutakwenda kwenye duru ya pili,” timu ya kampeni ya Ba imesema katika taarifa yake.

Hakukuwa na maoni ya moja kwa moja kutoka kwa Faye.

Mamilioni ya wananchi wa Senegal walipiga kura Jumapili Machi 24, 2024 kumchagua Rais wa tano wa nchi hiyo.

Hatua hiyo ilitokana na miaka mitatu ya msukosuko wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa na kuzua maandamano dhidi ya Serikali na kuungwa mkono kwa upinzani.

Kuna uwezekano wa kumalizika kwa utawala wa Rais anayemaliza muda wake, Macky Sall ambaye anaondoka madarakani baada ya muhula wa pili uliokumbwa na machafuko kutokana na kufunguliwa mashitaka kwa kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko na wasiwasi kwamba Rais huyo alitaka kujiongezea muda wa kukaa madarakani kinyume cha katiba.

Mgombea huyo hakushiriki kinyang’anyiro hicho kwa mara ya kwanza katika Historia ya Senegal. Muungano wake unaotawala ulimchagua Ba (62) kama mgombea wake.

Sonko, aliyekuwa jela hadi hivi karibuni, aliondolewa kwenye kinyang'anyiro hicho kwa sababu ya kukutwa na hatia ya kosa la udhalilishaji.

Anamuunga mkono Faye, mwanzilishi mwenza wa chama kilichovunjwa cha PASTEF, ambaye pia aliwekwa jela kwa takribani mwaka mmoja uliopita kwa tuhuma, zikiwamo za kukashifu na kudharau Mahakama.

Sheria ya msamaha iliyopitishwa mwezi huu iliruhusu kuachiwa kwake kabla ya kupiga kura.

Yeye na Diomaye wamefanya kampeni pamoja chini ya kaulimbiu isemayo: “Diomaye ni Sonko.”

Takribani watu milioni 7.3 walijiandikisha kupiga kura katika nchi hiyo yenye watu wapatao milioni 18. Waliojitokeza walikuwa karibu asilimia 71, kwa mujibu wa televisheni ya Taifa (RTS).

Siku ya uchaguzi ilienda vizuri bila matukio makubwa yaliyoripotiwa.

Awamu ya kwanza ya hesabu zilizotangazwa kwenye televisheni ilionyesha Faye alikuwa ameshinda kura nyingi.

Umati wa watu wenye furaha walikusanyika katika Kitongoji cha Sonko huko Dakar, huku wakifyatua fataki, wakipeperusha bendera za Senegal na kupuliza vuvuzela.

"Huu ni uchaguzi usio wa kawaida," amesema Nicolas Haque wa Al Jazeera, akiripoti kutoka nje ya nyumba ya Sonko.

"Watu wanasherehekea nje ya nyumba ya mwanasiasa ambaye hata hayumo kwenye kinyang'anyiro - Ousmane Sonko,” amesema na kuongeza:

“Kwa watu wa hapa, ukweli kwamba uchaguzi huu ulifanyika ni sababu ya kusherehekea. Kumekuwa na hisia nyingi zilizowekwa chini zinazotolewa. Katika mitaa hii wiki chache zilizopita, kulikuwa na ghasia, waandamanaji wakipinga uchaguzi huu usifanyike.”

 “Hakuna aliyedai ushindi. Shughuli ya kuhesabu kura bado inaendelea, lakini kuna  wagombea mashuhuri ambao wote wamempongeza Faye."

Mmoja wa wagombea wakuu, Anta Babacar Ngom alimtakia mafanikio Faye kama kiongozi wa Senegal katika taarifa.

"Hongera kwa Bassirou Diomaye Faye kwa ushindi wake usio na shaka," alisema kwenye X.

Haijabainika ni vituo vingapi kati ya 15,633 ambavyo vimehesabiwa kufikia sasa.

Matokeo ya mwisho ya kura yanatarajiwa kutangazwa kesho Jumanne Machi 26.

Duru ya pili ya upigaji kura itafanyika tu ikiwa hakuna mgombeaji atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zitakazopigwa.