Tanzania kushirikiana na China masuala ya uhamiaji

Muktasari:

  • Akizungumza leo Jumatatu Desemba 18, 2023  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini, Jumanne Sagini, amesema makubaliano hayo ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassani aliyoifanya nchini China

Moshi. Nchi ya China imesaini mkataba wa makubaliano na Tanzania kwa ajili ya kuimarishwa uhusiano kati ya Jeshi la Uhamiaji la Tanzania na la China.

Makubaliano hayo yamefanyika katika Chuo cha Uhamiaji Moshi na kuhudhuriwa na maofisa wa Jeshi la uhamiaji kutoa China na Tanzania.

Akizungumza leo Jumatatu Desemba 18, 2023  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini, Jumanne Sagini, amesema makubaliano hayo ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassani aliyoifanya nchini China.

Amesema makubaliano hayo, yatasaidia Tanzania kujifunza nchini China, kutokana na nchi hiyo kufanya vizuri katika idara ya uhamiaji, pia itasaidia kukuza viwanda kutokana na nchi hiyo kufanya vizuri katika sekta ya viwanda duniani

"Makubaliano hayo yataimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo, hivyo idara ya uhamiaji katika nchi ya China,’’ amesema.

Amesema nchi ya China inafanya vizuri katika teknolojia hivyo mategemeo ya  makubaliano hayo yatakwenda kuimarisha utendaji  hasa uhamiaji ambapo watakuwa wakibadilishana uzoefu.

Kamishna wa Jeshi la uhamiaji nchini, Dk Anna Makakara, amesema makubaliano hayo yataimarisha sekta ya utalii kutokana na wageni wengi kuingia nchini ikiwemo China na mataifa mengine duniani.

Amesema makubaliano hayo walioingia yatasaidia kutoa mafunzo na taarifa katika nchi hizo mbili za Tanzania na China.

Kamishna wa uhamiaji nchini China, Li Junjie amesema makubaliano yaliyoingiwa ni kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya  Tanzania na China.