Tume yatangaza matokeo rasmi ya awali, Faye ashinda kwa asilimia 54.28

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Faye anakuwa Rais wa tano wa Senegal akitanguliwa na marais wanne ambao ni Leopold Sedar Senghor (1960—1980), Abdou Diouf (1981—2000), Abdoulaye Wade (2000—2012) na Macky Sall aliyeingia madarakani mwaka 2012 hadi sasa.

Dakar. Tume ya Uchaguzi ya Senegal imetangaza matokeo rasmi ya awali ya urais nchini humo ambayo yanaonyesha mgombea wa upinzani, Bassirou Faye ameshinda kwa asilimia 54.28 ya kura katika duru ya kwanza.

Faye alimtangulia mgombea wa muungano unaotawala, Waziri Mkuu wa zamani, Amadou Ba ambaye alipata asilimia 35.79 ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi huo uliofanyika Jumapili Machi 24, 2024.

Ushindi wa Faye, ambaye aliachiwa huru kutoka jela siku 10 kabla ya uchaguzi, bado unapaswa kuthibitishwa na chombo cha juu cha kikatiba cha Senegal, ambacho kinatarajiwa kufanya hivyo siku chache zijazo.

Faye (44) ambaye amesema anataka kuupumzisha mfumo wa sasa wa kisiasa, anatazamiwa kuwa Rais mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Senegal.

Mgombea aliyeshika nafasi ya tatu, Aliou Mamadou Dia alipata asilimia 2.8 ya kura, kwa mujibu wa takwimu zilizosomwa katika Mahakama ya Dakar na Rais wa Tume ya Taifa ya Kuhesabu Kura, Amady Diouf.

Wakati ushindi wake katika uchaguzi wa Jumapili ukiwa dhahiri baada ya kuchapishwa kwa matokeo yasiyo rasmi, kiwango cha ushindi wa Faye kilithibitishwa Jumatano na Tume ya Kuhesabu Kura ambayo iko chini ya Mahakama.

Idadi ya waliojitokeza kupiga kura, asilimia 61.3, ilikuwa chini ukilinganisha na mwaka 2019 wakati Rais anayeondoka madarakani, Macky Sall aliposhinda muhula wa pili katika duru ya kwanza, lakini zaidi ya mwaka 2012.

Kutangazwa kwa matokeo rasmi ya awali kunaonekana kusafisha njia ya makabidhiano ya madaraka kati ya Sall na mrithi wake.

Mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na Rais Sall kuahirisha uchaguzi dakika ya mwisho na ratiba ya uchaguzi iliyoharakishwa, ilitia shaka kama makabidhiano hayo yangeweza kufanyika kabla ya muhula wa aliye madarakani kumalizika rasmi Aprili 2.

Lakini makabidhiano ya haraka sasa yanaonekana yatawezekana katika taifa hilo ambalo linajivunia utulivu na misingi ya kidemokrasia katika eneo la Afrika Magharibi lililoathiriwa na mapinduzi.

Wagombea urais wana saa 72 baada ya matokeo kutangazwa na Tume kwa ajili ya kukata rufaa kwenye Baraza la Katiba.

Katiba inasema iwapo hakuna rufaa itakayotolewa katika kipindi hicho, Baraza litatangaza mara moja matokeo ya mwisho ya uchaguzi.

Iwapo pingamizi litatolewa, Baraza lina siku tano za kufanya uamuzi wa ama kumtangaza tena mshindi au kubatilisha uchaguzi.