Ufaransa: Israel haina maamuzi juu ya Gaza

Muktasari:

  • Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Catherine Colonna amesema kwamba Ukanda wa Gaza ni ardhi inayomilikiwa na Wapalestina hivyo hatima yake haipaswi kuamuliwa na Israel.

Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna, amesema kwamba Ukanda wa Gaza ni ardhi inayomilikiwa na Wapalestina, hivyo hatima yake haipaswi kuamuliwa na Israel.

Colonna ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari vya nchini Marekani.

Kwa mujibu wa tovuti ya BBC, kauli yake inakuja baada ya mawaziri wawili wa Israel kupendekeza kwamba raia wa Kipalestina ambao ni wakazi wa Gaza, wahamishwe kwenye maeneo yaliyoko nje ya ukanda huo.

''Israel haina haki ya kuamua hatma ya Gaza, ambayo ni eneo lililopo chini ya himaya ya Palestina. Tunahitaji kurejea sera na maagizo ya sheria za kimataifa, na vile vile kuiheshimu," amesema Collona.

Colonna amesema kwamba, pendekezo hilo kutoka kwa mawaziri hao ni hatua hatari ya watu wasiojali na wanaotaka kulemaza juhudi za kupata suluhu ya kudumu na matamshi kama hayo yanakinzana na mpango wa muda mrefu wa Israel.

Israel na Hamas zimekuwa kwenye majibizano ya mashambulizi tangu Hamas ilipoanzisha mashambulizi katika maeneo ya mpakani na Israel mnamo Oktoba 7, 2023 na kusababisha zaidi ya vifo 1,200 na zaidi ya watu 200 kuchukuliwa mateka.

Israel imeendeleza mashambulizi yake ukanda wa Gaza huku ikiwataka Wapalestina waishio Gaza Kaskazini kuondoka kwa kile ilichodai kuwa ni hatua za kuliangamiza kundi la Hamas.


Imeandikwa na Victor Tullo kwa msaada wa mashirika.