Zuma, Ramaphosa katika vita mpya kusaka urais Afrika Kusini

Johannesburg. Chama cha ANC cha Afrika Kusini kimeendelea kupata pigo baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma kukibwaga tena mahakamani katika kesi ya kupinga chama kipya cha mwanasiasa huyo cha uMkhonto we Sizwe (MK) kutumia jina hilo.

Katika kesi hiyo, ANC kilidai kuwa jina na nembo hiyo ilikuwa ni la jumuiya za chama hicho, hivyo Zuma alikuwa amevunja sheria ya majina ya biashara.

Jina la MK na nembo yake vinahusisha alama kubwa ya kisiasa kwa sababu ndiyo iliyokua ikiwakilisha kitengo cha kijeshi cha ANC katika kupinga utawala wa wazungu wachache nchini humo.

Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Durban imetupilia mbali madai hayo na kumpa ushindi Zuma kuendelea kutumia jina hilo linalomaanisha Mkuki wa Taifa.

Huo ni ushindi muhimu kwa Zuma kuelekea uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika Mei 29, 2024.

Kufuatia ushindi huo, wafuasi wa Zuma waliokuwepo mahakamani hapo wamelipuka kwa furaha.

Visvin Reddy ambaye ni kiongozi wa MK jimbo la KwaZulu-Natal ambalo ndiyo nyumbani kwa Zuma likiwa na wafuasi wengi wa chama hicho, amesema ushindi wa kesi hiyo ni habari njema kwa chama hicho kilichoanzishwa Desemba 2023.

Alikiambia kituo cha televisheni cha Newsroom Afrika nje ya mahakama kuwa hatua ya ANC kukifungulia chama hicho kesi ni dalili kuwa inakiogopa.

Hata hivyo, ANC imesema itaukatia rufaa uamuzi wa huo wa mahakama.

Mwezi uliopita ANC ilishindwa kesi nyingine waliyofungua ili kukizuia chama cha MK kisishiriki uchaguzi mkuu kwa madai kuwa hakijatimiza masharti ya usajili.

Chama hicho kipya hakikutarajiwa kushinda uchaguzi mkuu ujao, lakini kwa kesi hizi kinaweza kupoteza idadi kubwa ya wabunge kwa mara ya kwanza tangu kiliposhika madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 1994 baada ya utawala wa makaburu.

Zuma mwenye umri wa miaka 82, alikuwa mpigania uhuru na baadaye Rais wa tatu wa nchi hiyo kwa miaka tisa tangu mwaka 2009.

Aliingia madarakani baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Thabo Mbeki kujiuzulu urais mwaka 2008.

Kama ilivyo kwa mtangulizi wake, Zuma naye aliondolewa madarakani kwa madai ya rushwa na nafasi yake kuchukuliwa na Rais wa sasa, Cyril Ramaphosa.

Mapema mwezi huu, mahakama ya uchaguzi ilizuia katazo la Tume ya Uchaguzi dhidi ya Zuma kugombea urais.

Katiba ya nchi hiyo inazuia watu kugombea urais kama atakuwa ameshitakiwa na kuhukumiwa kifungu cha zaidi ya miezi 12 jela.

Zuma alihukumiwa kwenda jela kwa miezi 15 mwaka 2021 kwa kushidwa kujitetea kwenye uchunguzi wa rushwa, hata hivyo, alitumikia kifungo kwa miezi mitatu tu, baada ya kubainika kuwa na matatizo ya kiafya na alitolewa kwa msamaha wa Rais Ramaphosa.

Mahakama ya Uchaguzi haikueleza sababu katika hukumu yake, lakini wanasheria wa Zuma wamesema kuwa msamaha huo ulimaanisha kuwa hukumu ilikuwa imefutwa.

Tume ya Uchaguzi sasa imekata rufaa mahakama ya juu ya kikatiba kwa lengo la kupinga uamuzi wa wa Mahakama ya Uchaguzi.


Kesi za rushwa

Zuma alianza kuandamwa na kashfa za rushwa kabla hata hajawa rais. Mwaka 2018, Zuma alikabiliwa na kesi ya mkataba wa silaha wenye thamani ya dola za Marekani 2.5 bilioni ambao ulisainiwa mwisho wa mwaka 1990.

Hata hivyo, Zuma alikanusha tuhuma zote. Mambo hayakuishia hapo, kutoana na kuandamwa rushwa, Zuma aliondolewa madarakani mwaka 2018 na alikutwa na mashitaka 16 ya kujibu.

Mashtaka hayo ambayo Zuma aliyakataa kuhusika yalijumuisha udanganyifu aliofanya ili kujipatia fedha na utakatishaji wa fedha.

Juni 2021, Mahakama ya Katiba nchini Afrika Kusini ilimhukumu kifungo cha miezi 15 jela Zuma, baada ya kukutwa na hatia ya kukaidi agizo la kufika mahakamani baada ya kutoonekana katika kikao cha uchunguzi wa kesi ya ufisadi wakati alipokuwa rais.

Mwenyekiti wa kamati maalum ya uchunguzi wa mahakama, Raymond Zondo iliyokuwa ikichunguza madai hayo, aliiomba mahakama itamke kuwa rais huyo wa zamani alidharau mahakama na imhukumu kifungo cha miaka miwili.


Alivyoanzisha chama chake

Licha ya kupewa msamaha na Rais Ramaphosa, Zuma alisema itakuwa ni usaliti kuifanyia kampeni ANC inayoongozwa na rais huyo.

"Siwezi na sitaifanyia kampeni ANC ya Ramaphosa," amesema Zuma katika taarifa aliyoitoa kwa umma na kuripotiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Januari mwaka huu, chama cha ANC, kilimsimamisha uanachama Zuma baada ya mwanasiasa huyo kuunga mkono chama chake cha MK.

Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula alisema kuwa Zuma, alipaswa kuchunguzwa na kamati ya nidhamu na chama kitachukua hatua za kisheria dhidi ya chama hicho kilichokuwa kikitumia jina la Zuma.

Zuma ni mmoja ya wapigania ukombozi wa Afrika Kusini, hususan kwa kujitoa kwake katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi uliokuwa umekithiri nchini humo.

Kama mmoja wa vijana waliokulia ndani ya ANC, Zuma amefanya kazi mbalimbali hadi kuwa Rais wa ANC na Rais wa nchi na ni mmoja kati ya wapigania ukombozi wachache wa Afrika Kusini waliobaki hai.



Anafuata njia ya Malema?

Kujiengua kwa Zuma ndani ya ANC kunaweza kuwa mwanzo wa chama hicho kumeguka na hatimaye kusambaratiba siku za usoni.

Zuma ameondoka akifuata njia aliyoondokea Julius Malema aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya ANC na ambaye sasa ni mwenyekiti wa chama cha Upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF).

Malema aliyekulia ndani ya ANC alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa vijana mwaka 2008 katika uchaguzi wenye utata. Alikuwa mtu wa karibu wa Zuma wakati huo, huku akiendesha kampeni yaupigania haki za rasilimali za madini kwa wazawa.

Hata hivyo urafiki wa Malema na Zuma uliyumba kutokana na madai ya utovu wa nidhamu uliodaiwa kufanywa na kijana huyo kwa mwenyekiti wake.

Kutokana na mvutano huo, mwaka 2012 Malema alianzisha kampeni ya kutaka Zuma ang’olewe kwenye uenyekiti wa chama kuelekea mkutano mkuu wa 53 wa chama hicho.

Hata hivyo, alifukuzwa uanachama kwa kosa la kukiingiza chama kwenye mgogoro.

Baada ya hapo alianzisha chama cha EFF na mwaka 2014 aligombea ubunge na kushinda, huku chama hicho kikipata viti 25 vya ubunge