‘Acheni dhana potofu kuhusu tohara’

Madaktari wakimfanyia mtoto tohara.

Muktasari:

  • Wito huo umetolewa leo Ijumaa Mei 10, 2024 na Mratibu wa Upimaji wa VVU na Huduma za Tohara Kinga Mkoa wa Mara, Felix Mtaki

Musoma. Wakazi wa Mkoa wa Mara wametakiwa kuachana na dhana kuwa mtoto wa kiume akifanyiwa tohara katika umri mdogo uume wake utakuwa mdogo, badala yake wafanye tohara mapema ili kujiepusha na magonjwa vikiwamo Virusi vya Ukimwi (VVU).

Wito huo umetolewa mjini hapa leo Ijumaa Mei 10, 2024 na Mratibu wa Upimaji wa VVU na Huduma za Tohara Kinga Mkoa wa Mara, Felix Mtaki alipozungumza na Mwananchi Digital kuhusu hali ya tohara kwa wanaume mkoani humo.

Mtaki amesema miongoni mwa sababu za baadhi ya wavulana kuchelewa kufanyiwa tohara ni dhana, akisema imesababisha baadhi ya vijana kuanza vitendo vya ngono mapema kabla ya kufanyiwa tohara.

"Kinachofanyika pale ni kuondoa ngozi ya juu inayofunika uume na hii haivurugi kabisa mfumo wa ukuaji wa hicho kiungo, mtu kuwa na uume mdogo au mkubwa hayo ni maumbile tu wala hakuna uhusiano na tohara katika umri mdogo," amesema.

Amesema kitendo cha baadhi ya vijana kuanza kujihusisha na vitendo vya ngono kabla ya tohara ni moja ya sababu inayosababisha uwepo wa maambukizi ya VVU.

"Kwa mujibu wa utafiti wa kitaalamu tohara ina uwezo wa kupunguza maambukizi ya Ukimwi kwa asilimi 60, tofauti na yule ambaye hajafanyiwa tohara kwa hiyo unaweza kuona hapo hatari iliyopo kwa kuwachelewa kufanya tohara.

“Pia, tukumbuke tohara sio sababu ya kufanya ngono zembe," amefafanua Mtaki.

Baadhi ya wakazi wa Musoma waliozungumza na Mwananchi wamesema jitihada zaidi zinahitajika ili kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa tohara kwa wanaume ikihusianishwa na suala zima la maambukizi ya ugonjwa huo.

Mmoja wa wakazi hao, Modesta Wambura amesema mume wake alizuia watoto wasifanyiwe tohara wakiwa na umri mdogo hadi watakapofikisha miaka 16 kwa madai kuwa wakifanyiwa wakiwa wadogo upo uwezekano wa kuwa na uume mdogo.

"Mume wangu alikataa kabisa mimi nilitaka watoto wangu pacha watahiriwe wakiwa na miaka mitatu, alisema wakifanyiwa katika umri maumbile yao yatakuwa madogo na si unajua tena haya mambo katika jamii, uume mdogo ni fedheha," amesema.

Mkazi mwingine, Furaha Webiro amesema awali iliaminika baadhi ya jamii wilayani Rorya hazifanyi tohara lakini kwa sasa hali imebadilika kutokana na mwingiliano wa kijamii na kiuchumi.

"Sasa hivi kuna mchanganyiko wa watu katika kila wilaya,  pia wapo wanaotoka nje ya mkoa hata nje ya nchi wengine wapo kwa ajili ya masuala ya utafutaji kiuchumi," amesema Furaha.

Mzee wa kimila, Marwa Nyarobi amesema kwa mujibu wa taratibu za Kabila la Wakurya, zamani tohara ilikuwa ikifanyika kwa kijana mwenye umri kuanzia miaka 16.

"Tulikuwa tunaamini ukifanya ngono kabla ya tohara basi ungepata matatizo wakati wa kutahiriwa," amesema Nyarobi.