Ajiua akimtuhumu mkewe kuzaa na mwanaume mwingine

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo

Muktasari:

Kwa mujibu wa Polisi mtu huyo aljijeruhi kwa kisu na ndugu walipomuona,  walimkimbiza kituo cha afya Bwanga lakini wakati madaktari wakipambana kuokoa maisha yake alipoteza maisha.

Geita.  Mkazi wa kijiji cha Busaka kata ya Bwanga Wilayani Chato Mkoani Geita, anadaiwa kujiua kwa kujichoma kisu kwa kile kinachodaiwa ni ugomvi wa kifamilia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,  Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja marehemu kuwa ni Mpanduji Misigwa(46) tukio lililotokea Aprili 23,2024 saa 11jioni katika kituo cha afya Bwanga kilichopo wilayani Chato mkoani hapa.

Kwa mujibu wa Kamanda Jongo, mtu huyo alijijeruhi mwilini kwa kisu na ndugu walipomuona walimkimbiza kituo cha afya Bwanga,  lakini wakati madaktari wakipambana kuokoa maisha yake alipoteza maisha.

“Taarifa za awali, wanadai ni ugomvi wa kifamilia na ugomvi wa kifamilia una mambo mengi ndio maana tumefungua jalada la uchunguzi likikamilika, tutajua zaidi,” amesema Jongo.

Hata hivyo,  amesema polisi walipata taarifa za mtu huyo baada ya ndugu zake kufika kituoni kutaka PF3, wakidai ndugu yao alikua akijaribu kujiua na walipewa lakini baadaye alipofariki dunia walirudi kutoa taarifa za kifo chake.

“Mgogoro wa kifamilia ni jambo pana labda msongo wa mawazo au wivu wa kimapenzi matukio mengi yanayotokea ya namna hii, yanahusiana na tabia mbaya na inaonekana hakulelewa kwenye maadili hamjui Mungu kwa mtu anayemjua Mungu, ataenda kanisani au msikitini au kwa watu wamshauri badala ya kuchukua uamuzi kama huu,” amesema kamanda huyo.

Ameisihi jamii kuwasaidia watu wanaoonekana kuwa na msongo wa mawazo uliopitioliza kwa kukaa nao karibu ili wasije kujiumiza.

Kwa mujibu wa jirani ambae hakutaka jina lake litajwe,  amedai sio tukio la kwanza la Mpanduji kutaka kujiua.

Anadai alishafanya tena jaribio kama hilo lakini safari hiyo alikunywa sumu na kuwahiwa na ndugu zake akanusurika.

“Mara zote humtuhumu mkewe kuwa amezaa na mwanaume mwingine,” amesimulia jirani huyo.