Dk Biteko kusaidia vyombo vya habari vilipwe malimbikizo ya madeni

Baadhi ya wahariri waliohudhuria Mkutano Mkuu wa kitaaluma wa 13 wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioanza leo Aprili 29, 2024 jijini Dodoma na utamalizika kesho. Picha na Ibrahim Yamola

Muktasari:

  •  Mwenyekiti wa TEF, Deodutius Balile asema Serikali nyingi duniani zimeacha kuua waandishi wa habari, bali zinaua uandishi wa habari.

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema atamwomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wakuu wa Serikali wazisihi wizara na taasisi za umma kuanza kulipia madeni ya matangazo wanayodaiwa na vyombo vya habari.

Dk Biteko amesema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa kitaaluma wa 13 wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioanza leo Aprili 29, 2024 jijini Dodoma na utamalizika kesho.

Amesema suala la uwezeshaji wa vyombo vya habari kiuchumi ni jambo muhimu kwa ukuaji na ustawi wa vyombo vya habari na sekta nzima ya habari kwa ujumla wake. 

“Nitamwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wakuu wa Serikali wazisihi wizara na taasisi za umma zitenge bajeti ya kutosha kulipia gharama za matangazo pindi wanapotumia huduma hii kwa vyombo vya habari,” amesema.

Amesema bila matangazo, redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii inakuwa kazi ngumu kuendelea kutoa huduma hiyo ya habari. Kiuhalisia habari ni huduma si biashara.

Amesema hakuna uwezekano wa kutengeneza faida kupitia vyombo vya habari, hivyo inabidi viwezeshwe kwa njia ya matangazo, navyo visaidie kufikisha ujumbe kwa wananchi ili kujenga Taifa imara.

Dk Biteko amesema kwa upande wa matangazo anadhani watapiga hatua kubwa zaidi baada ya mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2023 kama walivyoeleza (wahariri) yaliondoa kikwazo kilichokuwa kikitaka kila tangazo la Serikali kupitia Idara ya Habari Maelezo.

Dk Biteko amesema hatua hiyo ni nzuri ikifikiwa kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na sasa zinazofuata ni za kimanunuzi.

“Hivyo tuingie katika taratibu hizo ili kuona jinsi gani vyombo vya habari vingi kadri inavyowezekana vipate matangazo, lakini kwa kuzingatia taratibu zilizopo kisheria,” amesema.

Amemwelekeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuziandikia taasisi na mamlaka zote zinazodaiwa na vyombo vya habari ili hatua zianze kuchukuliwa.

Waziri Nape amesema ni kweli hali ya kiuchumi ya vyombo vya habari si nzuri kabisa na hali hiyo ndiyo ilimsukuma kuunda kamati ya kulifanyia kazi suala hili.

Amesema kamati imekwishakamilisha kazi.

“Imekuja na mapendekezo mazuri mno, ambayo sisi serikalini tunajipanga kwa utekelezaji wake. Hili la kuzitaka wizara kutenga bajeti ya kutosha ya matangazo, sisi hatuna mgogoro nalo, tutazihimiza kwani tunaliona ni muhimu,” amesema.

Amesema watazungumza na wenzao na kuwashauri katika wizara na idara mbalimbali watenge bajeti ya kutosha itakayowawezesha kulipia huduma za matangazo kwa wakati pale wanapopata huduma hiyo.

Hoja ya madeni ilianza kuzungumzwa na Mwenyekiti wa TEF, Deodutius Balile kuwa  Serikali nyingi duniani zimeacha kuua waandishi wa habari, bali zinaua uandishi wa habari.

Amesema mbinu inayotumika ni kuvinyonga kiuchumi vyombo vya habari visiwe na uwezo wa kulipa waandishi mishahara, posho za wawakilishi (correspondents), bima za afya, kusafirisha waandishi kwenda mikoani na mwisho wa siku waandishi wawe ombaomba.

“Sauti ya masikini huwa hasikiki popote, isipokuwa akiangua kilio. Wahariri tunakaribia kulia,” amesema.

Amesema mwaka 2016 nchini  sheria iliingiza kifungu cha 5(L) kilichokuwa kinaweka mikononi mwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) mamlaka ya kukusanya na kusambaza matangazo kwenye vyombo vya habari kutoka taasisi na idara zote za Serikali.

Amesema hakika waliyaona matumizi ya kifungu hicho na ndicho kilikuwa chanzo cha vifo vya vyombo vya habari nchini.

Amemshukuru Rais Samia kwa kukifuta kifungu hicho katika marekebisho yaliyofanyika kwenye Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2023.

Hata hivyo, amesema wakati yanafanyika marekebisho hayo, tayari vyombo vya habari viliishakuwa hoi.

“Serikali kupitia wizara na taasisi zake, zilishaacha kutenga bajeti ya kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari, baadhi ya watendaji wakiona kuwa hii inawapa nguvu ya kuvidhibiti vyombo vya habari visipige kelele,” amesema.

Amesema katika kipindi hiki Tanzania ipo kwenye Bunge la Bajeti.

“Tunaomba wizara na taasisi za Serikali zitenge na kuongeza bajeti ya kujitangaza au kutangaza shughuli zao kwenye vyombo vya habari, ambako wengi wanataka kupewa huduma ya matangazo, lakini hawataki kuilipia kwa kisingizio kuwa hawana bajeti,” amesema.