‘Katiba mpya kujibu aina ya muungano Tanganyika na Zanzibar’

Muktasari:

  • Aprili 26, 1964, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na leo Jumatano, Aprili 26 muungano huo umefikisha miaka 59 tangu ulipoasisiwa nan a marais, Mwalimu Julius Nyerere kwa Tanganyika na Abeid Aman Karume wa Zanzibar ambao wote wamekwisha fariki dunia.

Dar es Salaam. Mwandishi Mkuu wa Gazeti la Mwananchi, Elias Msuya amesema huenda maswali yaliyopo vichwani mwa Watanzania wengi kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar yakajibiwa katika mchakato wa Katiba mpya.

 Miongoni mwa maswali aliyoyaainisha Msuya ni aina ya muungano uliopo baina ya Tanganyika na Zanzibar kama ni wa Serikali mbili, shirikisho au muungano wa Serikali moja

Msuya ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Aprili 26, 2023 wakati akichangia mada kwenye Twitter Space inayosema ‘nini kifanyike kuimarisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ ilioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Mjadala huu umekuja wakati ambapo leo April 26, ni maadhimisho ya kumbukumbu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiwa ni miaka 59 sasa tangu Muungano huo uhasisiwe na Hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na hayati Abeid Amani Karume Rais wa Zanzibar, uliofanyika Aprili 26, 1964.

“Muungano huu umekuwa na maswali mengi kwa nini Zanzibar na Tanzania bara kuna marais. Pia kumekuwa na maswali je, Muungano wetu una maswali ya kuifanya Zanzibar ni mkoa au nchi?  Au Zanzibar ni kama Taiwan ambayo China inaifanya ni sehemu yake.”

“Lakini haya maswali huenda yakajibiwa katika mchakato wa Katiba kwamba tuwe na Muungano wa aina ipi,” amesema Msuya.

Msuya amesema pamoja na muungano uliopo sasa watu wengi wamekuwa wakihoji yanayoenela ikiwamo Zanzibar kuendelea kuwa nchi huru hasa kuwa na kiongozi wake na Tanzania kuwa na Rais wake jambo aliloeleza linaendelea kuibua maswali juu ya muungano uliopo.

Pia, hoja nyingine aliyoibua Msuya ambayo watu wengi wanahoji kuhusuaina ya muungano uliopo ni kwanini watu wanunue vitu Zanzibara na wanapopita bandari ya Dar es Salaama lazima atozwe kodi.

Kwa upande wake, Enzi Talibu Abood, aliyekuwa Mwandishi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Aman Karume amesema historia ya muungano huo umetokana na mapambano ya kisiasa ya Tanganyika na Zanzibar na nchi zote mbili zilifaidika.

“Muungano kimsingi ulikuwa faida yake ni kiusalama zaidi badala ya hizi kero zilizopo,” amesema.

Amesema ili muungano huo udumu ni muhimu viongozi baina ya nchi hizo mbili kukaa meza moja na kujadili kero zilizopo bila kuogopana na si kuangalia kujadili sula a katiba mpya pekee.

“Narudi tena viongozi wakubali kukaa meza moja kuangalia maeneo hasa yale yanayogusa Zanzibar tena waachie wenyewe, sio kudai Katiba Mpya. Kama ambavyo Rais Samia (Suluhu Hassan) alivyokaa na Freeman Mbowe (mwenyekiti wa Chadema) na kuhudhuria mkutano wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha),” amesema.

Ikumbukwe Zanzibar ilipata uhuru wake kutoka kwa Waingereza Disemba 10, 1963, lakini utawala ukabaki kwa Sultan kama Mkuu wa Nchi.

Januari 12, 1964, Sultan alipinduliwa na kuikimbia nchi kulikosababisha kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, dola kamili ya Wazanzibari iliyokuwa na Serikali yake, wimbo wake wa taifa, na Rais wake.

Dola ya Zanzibar haikudumu, Aprili 26, 1964, Muungano ulitangazwa wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunayoijua sasa. Na huo ukawa mwisho wa Zanzibar kama nchi huru.