Madaktari bingwa 56 kuweka kambi Morogoro

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Daniel Nkulu akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa kutangaza ujio wa madaktari bingwa 56. Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Lengo la kambi hiyo ni kuwafikia wagonjwa 2,000 na kufanya upasuaji kwa watu 100 watakaothibitika kuhitaji huduma hiyo

Morogoro. Madaktari bingwa 56 wanatarajiwa kuweka kambi ya siku tano mkoani Morogoro kutoa tiba kwa wagonjwa 2,000 kati ya hao 100 wakifanyiwa upasuaji.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Daniel Nkungu amesema madaktari hao tayari wamethibitisha kuja kuweka kambi hiyo na watafanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo, figo, pua, koo, masikio, tumbo na njia za mkojo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 30, 2024  Dk Nkungu amesema kila fani ya kibingwa itakuwa na madaktari wanne na magonjwa 14 yatachunguzwa na kufanyiwa matibabu.

Dk Nkungu amewataka wanawake kutumia fursa hiyo ya uwepo wa kambi ya madaktari kujitokeza ili kufanya uchunguzi wa afya zao.

“Wanawake waje kwa wingi kufanya uchunguzi maana wengi wamekuwa na changamoto ya uvimbe tumboni na sehemu zingine tumewasaidia lakini wengine tunakuta wako kwenye hatua ya kansa kabisa, hivyo wakija mapema na kujua hali ya afya zao itawasaidia,” amesema Dk Nkungu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kasiriye Ukio amesema lengo la kambi hiyo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro

“Tunategemea kuwajuza wananchi juu ya matatizo ya msingi ya kiafya yanayotibika na yale yanayohitaji ushauri wa ziada kwa wakati huo,”amesema Dk Ukio.

Mkazi wa Bigwa Manispaa ya Morogoro Andrea Antony amesema ujio wa madaktari hao utasaidia wananchi kupata tiba bila kusafiri

“Hapo mwanzo kupata huduma za kibingwa ilikuwa mpaka usafiri uende jijini Dar es Salaam lakini leo tunapata huduma hapahapa, kiukweli ile kambi itatusaidia wananchi kujua matatizo yetu kiafya na jinsi ya kupata matibabu,” amesema Antony.

Grace Peter, mkazi wa Misufini Manispaa ya Morogoro ameipongeza Serikali kwa kuandaa kambi hiyo ya madaktari bingwa watakaofanya upasuaji na matibabu papo hapo

“Naipongeza Serikali kwa kuleta huduma hii muhimu hapa Morogoro naamini itatusaidia, mfano mimi nina changamoto ya uvimbe tumboni nimeshafanyiwa upasuaji lakini bado ninasumbuliwa ndani kwa ndani hivyo madaktari bingwa wakija nitafika kupata matibabu,” amesema Grace.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Hamdu Shaka Hamdu amesema watahakikisha wananchi wanajitokeza maana wahitaji ni wengi.

“Nikuhakikishie tutahamasisha wananchi kuja kufanya matibabu kwa madaktari bingwa kwenye kambi hii na sisi tutaenda mbali kwa kuwasimamia wananchi wetu ili waje kupata huduma hii muhimu,”amesema Shaka.