Matinyi: Kuhusu pasipoti Mechi ya Yanga, Mamelodi waziri alifanya utani

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi

Muktasari:

  • Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema kauli iliyotolewa na Waziri wa Michezo, Dk Damas Ndumbaro kuwa watakaovaa jezi za timu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga kuwa na watatakiwa kuwa pasipoti ulikuwa ni utani kwa lengo la kuhamasisha uzalendo.

Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema kauli iliyotolewa na Waziri wa Michezo, Dk Damas Ndumbaro kuwa watakaovaa jezi za timu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga kuwa na watatakiwa kuwa pasipoti ulikuwa ni utani kwa lengo la kuhamasisha uzalendo.

Matinyi amesema lengo la kauli hiyo ilikuwa ni kuhamasisha uzalendo na hakumaanisha kama kweli watu watazuiliwa kuingia uwanjani kama ilivyochukuliwa.

Matinyi ameyasema hayo leo Jumapili Machi 24, 2024 akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita ndani ya miaka mitatu.

“Alichozungumza Waziri alikuwa anahamasisha uzalendo wa timu zetu na katika lugha zetu za michezo waandishi wa michezo tunafahamu, mimi niliwahi kuwa wakati fulani mwandishi wa michezo na niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa), sisi tukizungumza asilimia 80 ni utani, asilimia 20 tunazungumza vitu vimekaa vimenyooka.

“Ukizungumza habari zinazohusisha Simba na Yanga, ukang’ang’ania kuzungumza kitu kama kilivyoandikwa mahali Fulani, inafika mahali unawachosha watu, hizi ni timu zinazopenda utani, ni timu zinazopokea ujumbe wakati mwingine kwa lugha rahisi. Si kweli kwamba Waziri (Waziri wa Michezo, Dk Damas Ndumbaro) alimaanisha pale itakaguliwa pasipoti.  Anayejua pasipoti halali na isiyo halali ni Idara ya Uhamiaji, hakusema Idara ya Uhamiaji itaenda uwanjani pale,” amesema Matinyi.

Matinyi amesema katika muktadha huo wa ushabiki watu wamelikuza jambo hilo la mzaha mpaka Mamelodi wamesikia wameingia woga.

“Wameandikiwa na TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania) lakini mimi niwasihi Watanzania, tuwe wazalendo na tutarajie Mamelodi watafungwa na Al Ahly nao watafungwa magoli ya kutosha,”amesema Matinyi.