Mifumo duni inavyochelewesha wagonjwa kupata huduma Muhimbili

Baadhi ya wagonjwa wakisubiria kuendelea na huduma ya usajili, huku baadhi wakisubiri kuingia kwa daktari. Picha na Mpiga picha wetu

Muktasari:

  • Uchunguzi wa Mwananchi Digital umebaini sababu ya danadana kupata huduma hospitali hiyo ya Taifa ni mfumo wa usajili usio rafiki kwa wagonjwa wenye rufaa na wale wasio nazo, pia idadi kubwa ya wagonjwa.

Dar es Salaam. Wagonjwa kukaa muda mrefu wakisubiri kupata huduma ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Uchunguzi wa Mwananchi Digital umebaini sababu ni mfumo wa usajili usio rafiki kwa wagonjwa wenye rufaa na wale wasio nazo, pia idadi kubwa ya wagonjwa.

“Nilipangiwa kufika asubuhi lakini hadi sasa (saa 8 mchana) sijamuona daktari, mfumo wao wa usajili mgumu sana.

“Nimechoka, njaa inaniuma, nikila hapa nitashindwa kurudi nyumbani kwa sababu nina nauli tu,” anasema mgonjwa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, mkazi wa Gongo la Mboto.

Ripoti maalumu: Danadana kupata huduma Muhimbili

Malalamiko ya mgonjwa huyo hayana tofauti na ya mwingine ambaye pia hakuwa tayari kutajwa kwa kuwa bado anahitaji kupatiwa huduma hapo, anayesema:

“Wagonjwa tupo wengi lakini mfumo wa usajili naona una shida, maana kila sehemu ukienda unahamishiwa kwingine na hapo ni usajili tu, bado hujamuona daktari, hii inachelewesha kupata huduma.”

Baadhi ya wagonjwa wakisubiria kuendelea na huduma ya usajili, huku baadhi wakisubiri kuingia kwa daktari. Picha na Mpiga picha wetu

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa MNH, Aminiel Aligaesha anataja changamoto zinazosababisha wagonjwa kukaa muda mrefu kuwa ni baadhi ya wagonjwa kushindwa kuendana na miadi na huduma ya kina inayotolewa na madaktari.

“Kama kliniki yako inatakiwa kuanza saa tatu ianze muda huo, kinachotokea mtu anakuja hapa saa 12 asubuhi kliniki ni saa tatu au sita, sababu anakwambia analetwa kwa lifti ya mume, mke au ndugu. Huyu lazima atasema huduma imechukua muda mrefu,” anasema Aligaesha.

Hata hivyo, anakiri kuna nyakati fulani huduma huchelewa, ingawa wamekuwa wakitoa taarifa kwa wateja, iwapo daktari au mtaalamu husika amepata dharura.


Danadana kupata usajili

Malalamiko ya kuchelewa kupata huduma yanamlazimu mwandishi wetu kupiga kambi Muhimbili kupata ukweli, na hapa anasimulia:

Niliwasili hospitalini na kuanza usajili saa 4.03 asubuhi, walinzi katika jengo la wagonjwa wa nje (OPD) walinielekeza niende chumba namba 80 kilichopo ghorofa ya pili kuanza usajili.

Katika chumba hicho, nilisubiri kwa dakika tano kisha nikaingia, nikapewa fomu ya matibabu, kisha mhudumu akanielekeza niende chumba namba 62 kwa ajili ya matibabu.

Nilipofika huko nilipanga foleni kwenye benchi lililopo nje, nyuma na wagonjwa niliowakuta, wenye sura zinazoashiria uchovu na maumivu.

Nilimfuata mmoja na kumdodosa utaratibu wa pale kwa kuwa nje hakukuwa na mfanyakazi yeyote wa hospitali hiyo kubwa ya Taifa.

Mgonjwa yule mwanamume anayekadiriwa kuwa na umri wa ni miaka 40 hadi 50, alinijibu kuwa utaratibu ni mgumu na yeye amekaa hapo kwa saa tatu akisubiri jina lake liitwe.

“Hapa kuna changamoto ya mfumo, nipo hapa tangu saa 1.43 asubuhi lakini bado sijamuona daktari,” anasema mgonjwa huyo akionekana mwenye maumivu makali.

Mgonjwa yule baada ya kuiona fomu yangu ya bima, alinielekeza niende nje ya chumba namba 74 kupimwa presha na kupewa namba.

Baada ya kufika kilipo chumba hicho, nakutana na foleni nyingine, hivyo nikalazimika kufuata utaratibu ule. Saa 5.58 asubuhi zamu yangu inawadia, mhudumu baada ya kuiona fomu ile, ananirudisha chumba namba 62.

“Wewe unatakiwa ukapimwe presha na kuhudumiwa chumba namba 62, si hapa,” ananijibu huku akiendelea na majukumu ya kuhudumia wagonjwa wengine.

Baada ya kurudi chumba namba 62, sikupanga tena foleni, niliingia ndani moja kwa moja na kukutana na muuguzi aliyenipima presha kisha akanielekeza nisubiri katika chumba kile ambacho kimegawanywa vyumba vidogovidogo vinne vya madaktari.

Baada ya kati ya dakika 10 hadi 15 niliingia kwa daktari.

Saa 6.20 mchana nilionana na daktari ambaye baada ya kushika fomu yangu aliingia kwenye mfumo na kugundua kuwa simo, hivyo alimtaka nesi anielekeze chumba kingine cha usajili wa bima.

Nilifika chumba namba 64, nilipanga foleni na zamu yangu ilipowaidia, mtoa huduma aliniuliza daktari gani naenda kumuona, kwa kuwa sikuwa na jina la daktari, alinitaka nirudi chumba namba 74  kutafuta jina la daktari.

Saa 7.52 mchana nilirudi namba 74, mhudumu alinisikiliza na kunitaka nishuke chini katika jengo lile kwa ajili ya kupata namba kisha nirudi. Nilifanya hivyo, bila ya kuchelewa nilipewa namba kisha nilirudi chumba namba 74, fomu yangu ilikusanywa na kupanga foleni kusubiria kuingia kwa daktari niliyepangiwa.

Saa 9.53 alasiri naingia kuonana na daktari baada ya kutumia takribani saa sita kuhangaikia usajili na foleni za kumuona daktari.

Wakati huduma Muhimbili ikichukua wastani wa saa sita kumuona daktari, tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia utafiti wa Naser Elkum kuhusu muda wa mgonjwa kusubiri kumuona daktari unatakiwa kuwa kati ya dakika moja hadi 35.

Loading...

Loading...

Usemavyo utafiti

Changamoto kama hii imewahi kufanyiwa utafiti Agosti 2018 na Mhadhiri wa Idara ya Takwimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Amina Msengwa, ulioitwa ‘Muda wa kusubiri na mgawo wa rasilimali kwa Idara ya Wagonjwa wa Nje’ uliofanyika katika Hospitali ya Mwananyamala, ambao ulibaini mgonjwa mmoja anatumia zaidi ya saa nne kuhudumiwa.

“Matokeo yanaonyesha wagonjwa katika Hospitali ya Mwananyamala hutumia wastani wa dakika 167 kusubiri kuonana na daktari na muda wa juu zaidi wa kusubiri ni dakika 243 (saa nne),” inasema sehemu ya utafiti huo.

Utafiti mwingine uliofanywa na Mensur Biya, nchini Ethiopia mwaka 2022 unaonyesha Jumatatu inaongaza kwa wagonjwa kutumia muda mrefu kuhudumiwa hospitalini.

“Kati ya wahojiwa waliotembelea hospitali  Jumatatu, asilimia 69.3 walitumia muda mrefu zaidi wa kusubiri, huku siku zingine zikiwa na afadhali,” inasema sehemu ya utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la ‘BMC Health Services Research’.

Wingi wa wagonjwa

Mbali na ugumu wa mifuko, idadi kubwa ya wagonjwa pia ni chanzo cha changamoto hiyo.

Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2023/2024 imetaja ongezeko la asilimia 18.95 la wagonjwa wa nje wanaotibiwa katika hospitali za Taifa, za kanda na maalumu.

“Idadi ya OPD iliongezeka kutoka 1,596,778 kati ya Julai 2021 hadi Machi 2022 ikilinganishwa na wagonjwa 1,899,417 kati ya Julai 2022 hadi Machi 2023,” ilieleza wizara.

Kutokana na ongezeko hilo, kumekuwepo mzigo mzito kwa madaktari, kama anavyeoleza Rais mteule wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Mugisha Mkoronko kuwa daktari mmoja nchini Tanzania, anahudumia wastani wa wagonjwa 20,000 katika maeneo ya mijini.

“Maeneo mengine ni daktari mmoja kwa watu 35,000 au 50,000 inategemeana na eneo husika na idadi ya Watanzania waliopo," anasema Dk Nkoronko.


Loading...

Loading...

Nini kifanyike

Wadau na wataalamu wa huduma za afya nchini wameshauri mifumo ya kielektroniki ya usajili iboreshwe na kuifanya isomane ili kupunguza muda wa mgonjwa kusubi huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na nyinginezo.

Dk Zainabu Abdallah wa Hospitali ya Shirika la Reli Tanzania iliyopo jijini Dodoma, anashauri mifumo ya hosptali nchini, hasa zile kubwa, isomane ili ipunguze adha ya mgonjwa kutumia muda mwingi kujisajili.

“Kuboresha mifumo ya kielektroniki iwe inasomana na kuongeza wahudumu wa afya ili wastani wa daktari kwa mgonjwa upungue.

“Kusomana kwa mifumo kutamfanya mgonjwa awe na mwendelezo mzuri kwa daktari aliyeanza kumtibu na hata siku akibadilishiwa, hatakuwa na sababu ya kuanza kujisajili upya, bali ataendelea alipoishia,” anashauri Dk Zainabu.

Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige anasema njia bora ya kupunguza athari za mgonjwa kusubiri kama kuna dharura, mgonjwa aliyeletwa au anayehitaji tiba ya haraka, ahudumiwe kwanza kabla ya wengine.

“Kama hospitali ina milango mitano, kuwe na daktari katika kila mlango kuona wagonjwa, lakini pia inategemea mtu unaumwa nini. Ukapimwe ulete vipimo bado hakuna viwango katika hili. Kuna kitu kinaitwa ukaguzi wa kliniki hatuna katika nchi yetu, ambao unahusika kuangalia una matatizo gani sehemu yako ya kazi na namna unavyoyatatua,” anasema.

Muonekano wa ndani wa jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kukiwa na idadi kubwa ya wagonjwa wakisubiria huduma. Picha na Mpiga picha wetu

Dk Mzige anasema katika hilo ni lazima kufanyike utafiti, watazame hospitali zinatumia muda gani kuona wagonjwa.

Hata hivyo, anasema baadhi ya madaktari ni wazembe, wanachukua muda mrefu kuhudumia wagonjwa kutokana na mambo mengine ambayo hayahusiani na wagonjwa wenyewe.

Akizungumzia kuhusu mifumo ya usajili, Dk Mzige anasema bado ni duni ikilinganishwa na nchi za Kenya, Uganda na nyingine za Afrika ambazo zina mfumo mzuri wa usajili na wa haraka kuliko Tanzania.

Anasema masuala ya kusajili watu ni eneo muhimu kufuatiliwa kwa kuwa baadhi ya hospitali zimekuwa zikiacha majibu kwenye kompyuta ilhali kuna baadhi ya wagonjwa huhitaji vipimo vyao ili wanapohitaji kuendelea na matibabu waweze kuvitumia.


Muhimbili yajipanga kidijitali

Mbali na maoni ya wadau wa sekta ya afya, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Muhimbili, Aminiel Aligaesha anasema hospitali hiyo yenye matawi Upanga na Mloganzila ipo mbioni kutatua kero hiyo kwa kufanya ujumuishi wa huduma hizo katika mfumo mmoja.

“Tumeanza kwa kuunganisha huduma, mfano jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) tunahudumia watu 1,200 mpaka 1,300 kwa siku, hivyo kuna mifumo tunaiunganisha ili kuokoa muda, vitu vyote tunavifanya kwa kujumuisha huduma na tupo kwenye majaribio ya mfumo kwa sasa,” anasema.

Amesema ili kupambana na hali hiyo, wamekuwa wakiboresha mifumo mara kwa mara, hivi karibuni wanatarajia kuja na mfumo wa mgonjwa kuomba kuonana na daktari akiwa nyumbani.

“Mgonjwa ataomba kutibiwa akiwa nyumbani, unaingia kwenye mfumo unaangalia nataka kwenda kliniki ya macho kuonwa na daktari fulani, saa fulani ambayo tumeiweka kwenye mfumo.

“Utaratibu huu tumeshauanza upo kwenye majaribio, muda si mrefu utaanza kufanya kazi kwa ukubwa wake, hii yote ni kuhakikisha tunapunguza muda wa mtu anapokuja kupata huduma katika hospitali yetu, inajumuisha mnyororo mzima unapoingia mpaka unapotoka,” amesema.


Athari kuchelewa kupata huduma

Akizungumzia athari za mgonjwa kuchelewa kupata huduma, Dk Edgar Rutaigwa anasema inaweza kusababisha hali mbaya zaidi kwa mgonjwa na wakati mwingine kifo.

“Mgonjwa anapochelewa kuhudumiwa na daktari kuna vitu vikubwa viwili vinaweza kutokea, hali yake kuwa mbaya zaidi au kufariki dunia kabla ya huduma kutegemeana na aina ya ugonjwa,” anasema Dk Rutaigwa.

Amesema kwa sasa hospitali nyingi nchini zinamtathmini mgonjwa akiwa mapokezi kwa kumfanyia vipimo vya awali kabla hajaenda kumuona daktari.

Dk Rutaigwa amesema vipimo hivyo vya awali vinamfanya nesi amweke mgonjwa katika makundi matatu ambayo ni dharura, haraka au kawaida.