Mshitakiwa akana maelezo yake, adai hajui kilichomuua mkewe

Mshtakiwa Baraka Shija anayedaiwa kumuua mkewe kwa kumpiga na chuma kichwani akiwa katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Geita. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

Katika maelezo yake yaliyosomwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita leo Alhamisi Aprili 18, 2024 baada ya kupokewa kama kielelezo, mshitakiwa amenukuliwa hatua kwa hatua alivyomuoa mkewe kwa mahari ya Sh1 milioni hadi siku alipomshambulia kwa chuma na kumuua

Geita. Mshtakiwa Bahati Shija anayekabiliwa na shitaka la kumuua mkewe, Grace Daud kwa kumpiga na chuma kichwani ya  kukataa kurudiana naye, ameiambia Mahakama hajui sababu za kifo hicho.

Kauli ya mshitakiwa huyo imekuja siku moja baada ya shahidi wa tatu, E.7719 Sajenti Pascal ambaye ni Askari Mpelelezi Wilaya ya Geita aliyerekodi maelezo ya onyo ya mshitakiwa, kueleza namna alivyokiri kumuua mkewe.

Katika maelezo hayo yaliyosomwa Mahakama Kuu Kanda ya Geita leo Alhamisi Aprili 18, 2024 baada ya kupokewa kama kielelezo, mshitakiwa alinukuliwa hatua kwa hatua alivyomuoa mkewe kwa mahari ya Sh1 milioni hadi siku alipomshambulia kwa chuma na kumuua.

Baraka Shija anashtakiwa kwa kosa la kumuua kwa makusudi mkewe, Grace Daudi kinyume na kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, tukio analodaiwa kulitenda Juni 23, 2022.

Akitoa utetezi wake leo Aprili 18,2024 mbele ya Jaji Mfawidhi Kelvin Mhina anayesikiliza kesi hiyo,  mshtakiwa Shija amedai taarifa za kifo cha mkewe alizipata kutoka kwa baba mkwe aliyemtaja kwa jina la Daud Daniel.

Mshitakiwa alijitetea baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi wao na Mahakama kumuona ana kesi ya kujibu hivyo kutakiwa kuwasilisha utetezi wake.

Akiongozwa na wakili wake, Batholomeo Musyangi alidai Juni 24,2022 alipigiwa simu na baba mkwe wake, akihoji aliko mkewe na yeye kumueleza mama yake aliomba aende naye msibani tangu Aprili 20, 2022 na hajarudi nyumbani.

Amedai kuwa, kutokana na maelezo hayo baba mkwe, alimwambia mkewe ameuawa na watu wasiojulikana na kumtaka aende nyumbani lakini kabla ya kwenda walifika askari wawili wakiwa na mgambo na kumkamata.

Akiongozwa na wakili wake huyo, mshitakiwa amedai alipelekwa Kituo cha Polisi Nyakagwe na kuelezwa kosa lake na kukataa kumuua mkewe na polisi kumfunga pingu mikono na miguu kisha kumpiga na kudai pamoja na vitisho hakuwahi kukiri kosa.

Kabla ya mshitakiwa huyo kuanza kujitetea, shahidi wanne wa upande wa Jamhuri,  Dk Mlyakalamu Mataba aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, aliiambia Mahakama kuwa chanzo cha kifo kilitokana na majeraha makubwa kichwani.

Dk Mataba aliieleza Mahakama kuwa majeraha hayo yalisababishwa na kupigwa na kitu kizito na kusababisha kuvuja damu nyingi na kupata maumivu makali ndani ya ubongo.

Shahidi wa sita,  Bahati Makoye aliyekuwa mlinzi wa amani na kuandika maelezo ya ungamo kabla ya kusoma maelezo hayo kortini baada ya Mahakama kuyapokea, alisoma maelezo hayo neno kwa neno kile alichoeleza.

Katika maelezo hayo mshtakiwa amenukuliwa akieleza kuwa, “Juni 23, 2022  nikiwa nyumbani kwa kina Grace nilikokwenda kujua kama tutarudiana, nilienda kuzungumza na mkewe wangu lakini kabla ya kumaliza, aliondoka akaenda kutafuta mboga.

“Nami niliondoka kwenda nyumbani nikiwa njiani nilikutana na mke wangu tukazungumza na kugombana, mke wangu alianza kukimbia ndipo nilimkimbiza na kumpiga na chuma kichwani akaanguka nikampiga tena,” amesema.

Akaendelea kunukuliwa katika maelezo hayo ya ungamo akisema; “kisha nikaacha chuma pembeni yake na kwenda Bugalama kwa mganga wa kienyeji kujificha.”

Baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Mhina anayesikiliza kesi hiyo aliiahirisha hadi Mei 31, 2024 Mahakama itakapotoa hukumu yake.