Mwigulu amtolea uvivu Mpina bungeni

Muktasari:

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amejibu hoja zilizotolewa na wabunge huku akitumia muda mwingi kumpiga vijembe Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina.

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ametumia muda mwingi kumpiga vijembe Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina kuhusiana na hoja yake ya kupinga biashara zisifungwe kwa wamiliki wanaodaiwa kodi.

Dk Mwigulu amesema hayo leo Jumatatu Juni 26, 2023 wakati akihitimisha hoja yake ya bajeti kuu Serikali kwa mwaka 2023/24.

Dk Mwigulu amemweleza Mpina siyo ubingwa wala ustaarabu kupinga kila kitu na kwamba yeye anamwelewa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu suala la kuzifunga biashara.

Amesema kama mbunge hajaelewa ni bora kuuliza wabunge wenzake ili kuepuka aibu ya kupinga kila kitu.

Amesema Rais Samia amependekeza kutofunga biashara kwa sababu katika shughuli ya uzalishaji  wapo watu ambao siyo wamiliki ambao maisha yao yanategemea shughuli husika.

Amesema Serikali inapendekeza badala ya kufunga biashara wakae na mmliki wa biashara kutatua makosa yaliyopo na kwamba mtu ambaye hajasikia basi sheria ichukue mkondo wake.

“Lakini Mpina anaona jambo hilo halina maana anasema tufunge biashara, yeye kwa huruka yake anafurahia watu wakiumia, anakumbuka jinsi alivyokuwa anafanya sherehe kwa kuchoma nyavu bila kudhibiti nyavu zinazoingia. Jinsi alivyokuwa anafurahia kufunga viwanda anakuta mchirizi tu (kwenye kiwanda) anafunga,” amesema.

Amewataka wabunge kuangalia nchi zilizoendelea zilivyojielekeza katika kukuza sekta binafsi.

Aidha, Dk Mwigulu amesema pia Mpina anakataa pendekezo la Serikali kukataa kushikilia mizigo na vifaa vya wafanyabiashara.

Dk Mwigulu ametaka watu wote kuheshimu mitaji ya watu kwa kutoshikilia mali na vifaa vya wafanyabiashara.

“Huwezi kukaa na mitaji ya watu umeshikilia tu. Mtu ametoka akaenda kufuata biashara (bidhaa) hiyo, amekopa lakini wewe unashikilia tu, nyumba ameweka rehani, nyumba inakwenda kuuzwa wewe umeshikilia tu.

“Wewe umekaa tu ofisini na unalipwa mshahara halafu Mheshimiwa Rais anatafuta njia mbadala ya kushughulika na matatizo yasiyokubalika halafu  huyu anayelipwa kwa kodi za watu binafsi anasema jambo hilo sio nzuri,” amesema.

Amemtaka Mpina kutowafikisha mahali ambapo watamchukulia kuwa yuko upande ambao wanaambiwa wapinge kila kitu na kumtaka mambo mengine kutumia mantiki.

Alichokisema Mpina

Hata hivyo, akichangia katika Bajeti Kuu, Mpina amesema kuwa kuna mazingira ambayo yanasababisha biashara ifungwe na kutoa mfano kiwanda ama mgodi unatiririsha sumu kwenye vyanzo vya maji.

“Hizi mamlaka zifanye nini kama si kufunga ili kuokoa maisha ya watu lakini unakuta mtu anafanya biashara hana leseni, anauza bidhaa bandia, feki unamfanya nini kwa hiyo tukiweka vifungu kama hivyo vinaleta mkanganyiko kwa wasimamizi wa sheria…aidha ziondolewe ama atolee ufafanuzi,” amesema.

Mpina amesema mamlaka za usimamizi zimekuwa pia zikifanya vizuri katika usimamizi wa biashara hivyo zisikatishwe tamaa lakini pale mtumishi anapoonekana amekiuka sheria za nchi ashughulikiwe na si kuzituhumu taasisi hizo.